Na. John Mapepele, Singida
Waziri kuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassimu Majaliwa amezitaka Mamlaka zote za Mikoa kujipanga kikamilifu kutangaza fursa za uwekezaji zinapatikana kwenye mikoa yao kwa kushirikiana Kituo cha Taifa cha Uwezekezaji ili kuhakikisha kuwa fursa zote zilizoainishwa kwenye miongozo ya uwekezaji zinapata wawekezaji makini ili kuongeza mapato na ajira kwa wananchi
Akisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye tukio la uzinduzi wa Mwongozo wa Fursa za Uwekezaji Mkoa wa Singida, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano(5) Serikali imedhamilia kuimarisha ustawi wa wananchi wake kwa kuzalisha ajira milioni nane na kukuza uchumi wake kwa asilimia nane hivyo uwekezaji makini unatakiwa ili kufanikisha azma hiyo.
Amesema ili kuwapata wawekezaji makaini watendaji wote wa Serikali hawana budi kutoa taarifa sahihi za fursa zinazopatikana katika maeneo yao na utaratibu wote wa namna ya kuufuata ili kuweza kuwekeza.
“Ndugu zangu ni muhimu sana tubadilike taarifa za uwekekezaji tunazozitoa ziwe sahihi na ziwe zinafanana, ukienda kwa Mkuu wa Mkoa upate taarifa sawa na ukichukua taarifa hiyo kwa Katibu Tawala wa Mkoa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hapo tutakuwa tumefanikiwa” amesisitiza Profesa Mkumbo.
Amezitaka mamlaka hizo kutowakwamisha wawekezaji kwa kuhakikisha maeneo ya uwekezaji yanapatikana mara moja ili pindi Wawekezaji wanapofika wanapatiwa maeneo hayo na wanahudumiwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuondoa changamoto zozote zinazojitokeza.
Amesema balozi namba moja anayeweza kuleta au kutoleta wawekezazi katika nchi yoyote duniani ni Muwekezaji aliye ndani ya nchi husika hivyo ni muhimu kuwapa huduma bora ili waweze kutuletea wawekezaji wengi zaidi ambapo amesisitiza uwekezaji ufanywe kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo ya Serikali ili nchi yetu iweze kunufaika.
Amekemea tabia ya kupenda kutoa lawama baada ya kuingia mikataba mibovu na wawekezaji na badala yake amewataka watendaji kuwa makini katika mchakato mzima wa majadiliano na kufunga mikataba hiyo na wawekezaji.
Aidha, ameitaka kila Mkoa kuangalia kuangalia maeneo machache ya kipekee ili kufanya uwekezaji wenye tija badala ya kwenda na maeneo mengi ambayo hayana tija.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kubuni mikkakati kabambe ya uwekezaji ambayotayari katika kipindi kifupi imeleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kijamii kwenye nchi yetu.
Amesema Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa ikionekana kama mikoa masikini lakini sasa umekuwa ni miongoni mwa mikoa ambayo inaweza kuongoza kuleta mapato makubwa kwa nchi kutokana na kuboreshwa kwa mazingira na fursa nyingi zilizopo.
Ametaja baadhi ya fursa za uwekezaji zinazopatikana kuwa ni pamoja na madini, kilimo cha Alizeti na Korosho, mafuta asilina na gesi pia elimu.