Monday, November 25

“Dhamira yangu ipo pale pale kwa wanafunzi watakaofaulu na kukaa bodingi kulipia nusu ya gharama ya chakula kwa kila mwezi” Mgunge wa Jimbo Gando.

NA ABDI SULEIMAN.

MBUNGE wa Jimbo la Gando Kisiwani Pemba Salum Mussa Omar, amesema kuwa bado dhamira yake ipo pale pale kwa wanafunzi wa jimbo hilo, watakaofaulu na kukaa bodingi kulipia nusu ya gharama ya chakula kwa kila mwanafunzi.

Mbunge huyo alisema adhama hiyo ambayo aliitoa kwa wananchi wakati akiomba kura, bado ipo hivyo wanafunzi wanapaswa kusoma kwa bidii ili kutumia fursa hiyoo.

Aliyaeleza hayo hivi karibuni huko Gando Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati alipokua akizungumza na wanafunzi 22 ambo wamepata divishani ONE kidato cha nne mwaka huu.

Alisema lengo lake ni kuona wanafunzi wanahamasika zaidi katika kusoma, pamoja na kusoma zaidi masomo ya sayansi ili kuweza kuwa wataalamu bora na kutoka jimbo la Gando.

“Nimedhamiria kufanya hivyo ili kuhakikisha Jimbo la Gando linatoa wataalamu wa fani mbali mbali, kupitia katika jimbo letu hili ni jambo ambalo halijawahi kufanywa na mbunge yoyote hapa Zanzibar”alisema.

Aidha aliwataka wanafunzi hao kuhakikisha wanasoma kwa bidii, na kuhakikisha malengo yao yanafikiwa waliotoka nayo majumbani mwao ili kufikia ndoto zao.

“Unapokuwa katika skuli za bodingi changamoto nyingi munakumbana nazo, lakini musikubali kurudi nyuma kutokana na changamoto hizo, chamsingi kufikia malengo yako uliojiwekea”alisema.

Hata hivyo mbunge huyo aliwashauri wanafunzi wanapokua vyuoni na kipindi wanachofunga skuli, kuhakikisha wanarudi maskuli walikotoka kwa lengo la kusaidia wenzao.

Kwa upande wake Haji Mkubwa Haji, alimtaka mbunge huyo kuwaangalia na wanafunzi ambao hawakupata alama moja kwa moja ya kuendelea mbele, nao kuwatumia jicho ili wanafunzi hao waweze kutimiza ndoto zao.

Hamad Mwintumbe Mbarouk kutoka Gando, aliwataka wanafunzi ekeleza zaidi katika masomo, kwani gharama kubwa inatumika katika kulipia gharama za nusu ya chakula.