Monday, November 25

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi MheDk. Hussein Ali Mwinyi Amepongeza Mashirikiano ya Makubwa ya Taasisi za TAKUKURU na ZAECA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na Ujumbe wake walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kwa kujitambulisha mazungumzo hayo na (kushoto kwa Rais) Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Brigedia Jenerali John Mbungo na (kulia kwa Rais) Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza mashirikiano makubwa yanayotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kwa  Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA).

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Brigedia Jenerali John Mbungo akiwa amefuatana na  ujumbe wake.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja ya kuendelezwa kwa mashirikiano hayo hasa ikizingatiwa kwamba (TAKUKURU) ni Taasisi ya siku nyingi na ina uzoefu mkubwa.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina azma ya kuijengea uwezo hivyo, katika masuala ya uchunguzi, mafunzo na shughuli zote zinazofanywa na (TAKUKURU) basi watajifunza kutoka Taasisi hiyo.

“Tunashukuru kwa milango yenu kuwa wazi na tutaomba kuendelea kwa sababu tunataka kukifanya chombo hichi kuwa imara zaidi na hatuna sehemu nyengine ya kupata  uzoefu kama si TAKUKURU ”, alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuwa na muundo kama ule wa (TAKUKURU) ikiwa ni pamoja na kushuka katika ngazi za Mikoa na Wilaya licha ya hali hiyo kuhitaji uwezo mkubwa lakini ni vyema wakaanza ili kazi wanazozifanya ziwe rahisi zaidi badala ya kutegemea ngazi za makao makuu pekee.

Alisema kuwa ni vyema (ZAECA) ikajifunza kutoka Taasisi ya (TAKUKURU) kutokana na mambo mbali mbali ya kuiendesha Taasisi hiyo.

Alitoa shukurani kwa Taasisi ya (TAKUKURU) kwa kuonesha utayari wao wa kuwasaidisa ZAECA, na kusisitiza kwamba katika wakati huu uliopo Taasisi hiyo ina umuhimu wa pekee kwani uzoefu unaonesha duniani kwamba katika kuhakikisha rushwa inadhibitiwa ni lazima kuwepo kwa chombo cha kusimamia uadilifu.

Nae  Brigedia Jenerali John Mbungo, Mkurugenzi Mkuu wa (TAKUKURU) huyo aliyeteuliwa mwaka jana Mei 2020, ambaye mwanzo alikuwa Naibu Mkurugrnzi Mkuu alisema kuwa ujio wake ni kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kuwatembelea washirika wenzao (ZAECA).

Alisema kuwa (TAKUKURU) imekuwa ikishirikiana vyema na (ZAECA) katika mambo mali mbali ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika mafunzo ya weledi hasa ikizingatiwa kwamba (TAKUKURU) ina uzoefu mkubwa kutokana na kutangulia kuanzishwa kwani Taasisi hiyo imeanzishwa mwaka 1975 ambapo (ZAECA) imeanzishwa mwaka 2013.

Alisema kwamba (TAKUKURU) ni Taasisi ya kwanza kuanzishwa katika bara la Afrika, hivyo ina uzoefu mkubwa katika kuendesha shughuli zake.

Pamoja na hayo, Bregedia Jenerali Mbugo alisema kuwa Taasisi hizo mbili zimekuwa zikishiriki vyema katika vikao mbali mbali vya Kimataifa kwa pamoja na kuangalia vipi Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaweza kunufaika na vikao hivyo.

Alisema kuwa wamekuwa wakikaa pamoja na kujadili mambo kadhaa kuhusu vikao hivyo ambapo pia, kwa vile wote ni wanachama wa Mkataba Mkuu wa Kimataifa wa Mapambano dhidi ya Rushwa, hivyo wamekuwa wakihudhuria pamoja vikao hivyo na kuangalia vipi nchi inaweza kunufaika sambamba na kuhudhuria vikao vya Afrika Mashariki ambapo pia ina sehemu ya masuala ya rushwa.

Aidha, alieleza namna wanavyoshiriki pamoja vikao vya nchi za Kusini mwa Afrika ambavyo hukaa pamoja mara baada ya kumaliza vikao hivyo na kujadili kwa pamoja namna ya utekelezaji wa masuala hayo.

 

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wazee Zanzibar (JUWAZA) katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar na kuipongeza Jumuiya hiyo kwa ushirikiano wanaotoa kwa Serikali.

 

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jumuiya hizo zinahitajika kutokana na umhimu wake mkubwa ikiwa ni pamoja na kutoa msaada wake kwa Serikali kwani si mambo yote Serikali inaweza kuyafanya.

 

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Jumuiya hizo kwa azma ya kuhakikisha wazee nao wananufaika.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza mafanikio makubwa yatakayopatikana kutokana na vitambulisho vinavyotolewa kwa ajili ya wazee.

 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Naibu Katibu Mkuu Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Abeida Rashid Abdallah kwa ushirikiano wake mzuri anaouonesha kwa Jumuiya hizo na kumtaka kuendelea.

 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar