Saturday, March 15

Kombe la CAF: Je Ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri una maana gani kwa soka ya Afrika mashariki?

Maelezo ya picha, Mmiliki mwenza wa Simba SC Mohammed Dewji anijtahidi kuona klabu hiyo inakuwa ndani na nje ya uwanja

Ushindi wa bao 1-0 ambao Simba iliupata katika Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Al Ahly, Jumatano hii, ni wazi kwamba umeiweka klabu hiyo katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Bao pekee la dakika ya 31 lililofungwa na mshambuliaji Luis Miquissone limeifanya Simba kuongoza msimamo wa kundi A ikiwa na pointi sita na sasa inahitaji angalau pointi nne tu katika mechi nne zilizo mbele yake dhidi ya timu za Al Merrikh ya Sudan, AS Vita Club (DR Congo) na Al Ahly ili ijihakikishie tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya mashindano hayo makubwa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Ikiwa hilo litatimia, Simba itakuwa imeandika rekodi ya kuwa timu pekee ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kuweza kuingia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, tangu mfumo wa mashindano hayo ulipobadilika mwaka 2017 ambapo kuliwekwa hatua moja ya mtoano baada ya ile ya makundi kumalizika ikawa ya robo fainali, ikifuatiwa na nusu fainali na kisha fainali.

Hivyo ushindi wa juzi wa Simba ni jambo la kujivunia sio tu kwa mashabiki wa timu hiyo au Watanzania bali pia Afrika Mashariki kiujumla inapaswa kutembea kifua mbele kwa kile kilichofanywa na wawakilishi wao pekee wa eneo hili.

Klabu ya Simba nchini Tanzania

Ni ushindi wenye maana kubwa kwa Ukanda wa Afrika Mashariki kwani unatoa taswira ya mambo mbalimbali lakini pia unaweza kuwa chachu ya maendeleo ya mchezo wa mpira wa miguu katika nchi zake ikiwa tafakuri ya kina itafanyika lakini pia wahusika wakafanyia kazi yale wanayohitajika kutekeleza ili kuinua soka kwenye ukanda huo.

Soka linahitaji uwekezaji

Darasa kubwa ambalo ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly unatoa kwa nchi za Afrika Mashariki ni kwamba maendeleo ya mpira wa miguu ni lazima yaendane na uwekezaji wa kutosha wa fedha vinginevyo suala la klabu zetu za ukanda huu kufanya vizuri litabaki kuwa ndoto.

Ili timu iweze kufanya vizuri katika mashindano ya klabu Afrika kama ilivyo kwa Simba sasa ni lazima iwe na misuli imara ya kiuchumi ambayo itaiwezesha klabu husika angalau kuweza kupambana na timu kutoka kanda nyingi hasa ile ya Kaskazini mwa Afrika ambayo klabu zake zina nguvu kubwa kiuchumi.

Uwezo wa kifedha unaipa timu fursa ya kuwa na wachezaji bora wa daraja la juu au la kati ambao angalau wanaweza kuhimili ushindani dhidi ya timu kubwa zenye mafanikio katika medani ya soka kama vile Al Ahly, Esperance, CR Belouzdad, Wydad Casablanca, Mamelodi Sundowns, Raja Casablanca na nyinginezo.

Ushahidi wa hili tunaweza kuuona kwa Simba ambayo ndani ya kipindi cha miaka minne ambayo imekuwa chini ya uongozi wa mwekezaji, Tajiri Mohamed Dewji ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo, imetumia kiasi kisichopungua Shilingi 5 bilioni kugharamia usajili wa nyota kutoka mataifa mbalimbali nje na ndani ya Afrika lakini pia kuongeza mikataba ya wachezaji muhimu wa timu hiyo ambao wamekuwa chachu kwao kufanya vyema kimataifa.

Haiishii tu katika kusajili bali pia nguvu ya kiuchumi ndio imekuwa ikipelekea klabu ziweze kulipa na kutoa kwa wakati huduma stahiki za wachezaji kama vile mishahara, posho, matibabu, usafiri na malazi jambo ambalo limekuwa likiongeza morali na hamasa katika timu.

Simba imewahimiza mashabiki zaidi wajitokeze na kuinga mkono timu hiyo

CHANZO CHA PICHA,MAHMOUD BIN ZUBEIRY

Maelezo ya picha,Simba imewahimiza mashabiki zaidi wajitokeze na kuinga mkono timu hiyo

Kwa mfano katika mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambao Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya AS Vita Club ya DR Congo, uongozi wa timu hiyo ulitoa kitita cha zaidi ya Shilingi milioni 200 za Kitanzania kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo kama bonasi ya ushindi.

Kwa bahati mbaya, soka la Afrika Mashariki limekuwa likikabiliwa na ukata jambo ambalo limekuwa likidhohofisha klabu nyingi na kupelekea zishindwe kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa tofati na klabu kutoka kanda nyingine.

Tunaweza kuthibitisha hili kutoka kwa klabu kubwa nchini Kenya, Gor Mahia ambayo ililazimika kusafiri kwenda Zambia, siku ya mechi yake ya marudiano kuikabili NAPSA Stars ya huko, kutokana na kuchelewa kupata fedha za kugharamia tiketi za usafiri wa ndege ambao ungewapeleka na kuwarudisha na kuwarudisha nyumbani.

Vipaji sio tatizo

Kwa upande mwingine, ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly juzi umedhihirisha kwamba Afrika Mashariki ina utajiri wa vipaji vya soka ambavyo kama vikiendelezwa na kutunzwa vyema, ukanda huu unaweza kuwa tishio kubwa kwa siku za usoni.

Kuanza kwa idadi kubwa ya wachezaji kutoka nchi za Afrika Mashariki kwenye kikosi cha kwanza cha Simba katika mechi ile kunaweza kuwa uthibitisho tosha wa jinsi eneo hili lilivyo na neema ya kundi kubwa la vijana wenye vipaji vya mchezo huo.

Katika kikosi cha Simba kilichoanza dhidi ya Al Ahly, wachezaji wanaotoka katika ukanda wa Afrika Mashariki walikuwa saba (7) ambao ni sawa na 63.64% ya kikosi kizima huku wanne tu ndio wakiwa hawatoki katika nchi za ukanda huu.

Wachezi wa simba

CHANZO CHA PICHA,CAF

Wachezaji hao kutoka katika nchi za Afrika Mashariki ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Hassan Dilunga na Mzamiru Yassin ambao ni Watanzania, Joash Onyango (Kenya) na Lwanga Taddeo (Uganda) wakati kutoka mataifa mengine ni Chris Mugalu (DR Congo), Clatous Chama (Zambia), Luis Miquissone (Msumbiji) na Pascal Wawa (Ivory Coast).

Afrika Mashariki inaamka

Haikuwa rahisi kwa timu za Ukanda huu kufanya vyema katika hatua za makundi ya klabu Afrika kabla ya mwaka 2017 na nyingi zilikuwa zikiishia hatua za mwanzoni ambazo ni ama ile ya awali au raundi ya kwanza lakini katika kipindi cha miaka minne sasa, klabu za Afrika Mashariki zimeonekana kujitutumua na kujaribu kuonyesha kama zinaanza kuchoka kuwa wasindikizaji.

Ukiondoa Simba ambayo hii ni mara ya pili ndani ya miaka minne kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Gor Mahia wamefanya hivyo mara mbili (2018, 2018/2019) katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mara moja waliweza kufika robo fainali, Yanga ya Tanzania imefanya hivyo mara moja sawa na Rayon Sports ya Rwanda (2018) lakini pia KCCA ya Uganda imefanya hivyo mara moja (2018)

Lakini pamoja na hilo bado hakuna timu iliyoweza kutinga hatua ya nusu fainali na robo fainali inabakia kuwa hatua kubwa ambayo zimewahi kuifikia.

Ukiondoa hatua ambayo klabu za Afrika Mashariki zimefika, tumeshuhudia pia nchi mojawapo ya ukanda huu ikipata fursa ya kuwakilishwa na klabu nne katika mashindano ya klabu Afrika ambapo ilikuwa ni katika msimu wa 2018/2019 pale Tanzania ilipowakilishwa na timu za Simba na Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku Azam FC na KMC zikipeperusha bendera katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Ligi ya Tanzania inazidi kuwa na mvuto

Ushindi wa Simba dhidi ya Al Ahly juzi ni wazi kwamba utazidi kuongeza mvuto wa ligi ya Tanzania na kuifanya izidi kuwa kinara wa kufuatiliwa kwa ukaribu katika mataifa mbalimbali kulinganisha na ligi za nchi nyingine ambazo zipo ndani ya ukanda huu.

Simba ikicheza dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana mnamo 2018 "Simba Week"

CHANZO CHA PICHA,MAHMOUD BIN ZUBEIRY

Maelezo ya picha,Simba ikicheza dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana mnamo 2018 “Simba Week”

Hii itachagiza ongezeko la idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali ambao bila shaka watakuwa chachu ya kuimarisha viwango vya wachezaji wazawa lakini pia itavutia idadi kubwa ya wadhamini ambao watawekeza fedha zitakazosaidia klabu kujiendesha na kuboresha viwango vya wachezaji.

Lakini pia hiyo itasaidia kuwaweka sokoni wachezaji wa klabu mbalimbali zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara jambo linaloweza kuwa na faida kubwa kwao kuimarisha vipato vyao lakini pia kuongeza pato la nchi na hata klabu ambazo zinaweza kuongeza makusanyo yao kutokana na mauzo ya wachezaji husika kwenda katika klabu nyingine za nje ama ndani ya bara la Afrika.

Ni wazi kwamba ligi ya Tanzania kwa sasa ndio inaongoza kwa klabu kulipa mishahara mikubwa kwa wachezaji jambo ambalo limekuwa likivutia nyota wengi kukimbilia klabu mbalimbali zinazoshiriki ligi hii.