Na Maulid Yussuf, Wema
Katibu Mkuu kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Muhandisi Zena Ahmed Said amesema watoto wa kike nao wana uwezo wa kufanya mambo makubwa endapo ataitumia vyema fursa ya elimu.
Akizungumza katika sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani katika uwanja wa Skuli ya Dk.Ali Mohammed Shein Mkoa wa Mjini Magharibi amesema mwanamke anaweza kubuni kitu chochote chenye manufaaa endapo atakua na muamko wa kutafuta elimu kwa bidii.
Amesema mwanamke nae anafursa sawa na mtoto wa kiume kwenye haki ya kusoma kwani nao wameonesha ubunifu wao wa kila kitu hasa masomo ya sayansi.
Akizungumzia suala la udhalilishaji katika jamii amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imetoa agizo la kuanzisha mahakama ya kesi za udhalilishaji na tayari imesharekebisha sheria ya kuondosha dhamana kwa mtu yeyote atakayefanya vitendo hivyo.
Amesema jamii ishirikiane na vyombo vya dola kumaliza kabisa vitendo hivyo kwa kuhakikisha wanatoa ushahidi kama unavyo hitajika na kuwasisitiza wanafunzi kuachana na mambo yote ya anasa ili waweze kuvishinda vishawishi wakiwa masomoni.
Amewanasihi wazazi nao kurudi katika mila za malezi ya pamoja ili kuepuka mmomonyoko wa maadili kwa watoto wao sambamba na kuwataka wanawake wote kuhakikisha wanatimiza malengo mahususi ya siku ya wanawake duniani.
Pia amewaasa Wanafunzi kuwa na heshima kwa watu wote ili waweze kufanikiwa kwenye malengo yao ya hapa duniani na kuwawekea mustakbali mzuri wa akhera.
Nae Mkurugenzi Idara ya Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bi Asya Iddi Issa amewasisitiza watoto wa kike kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kuepukana na vishawishi vitakavyo waharibia malengo ya maisha yao.
Akitoa neno la shukurani mwalimu mkuu wa Skuli ya wanawake Ben-bella bi Zainabu Dachi amesema kwa kutumia mbinu mbalimbali za ufundishaji watahakikisha wanamkomboa mwaname aweze kutumia fursa za kushiriki kwenye maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wao wanafunzi wa kike wameiahidi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kusoma kwa bidii hasa masomo ya sayansi ili kuhakikisha Zanzibar inazalisha wataalamu wa kike katika fani mbalimbali.
Pia wameiomba Serikali kuweka adhabu kali kwa wale wote wanaofanya vitendo vya udhalilishaji kwenye jamii ili iwe fundisho.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na walimu na wanafunzi wa skuli ya wasichana Benbella na Dkt Ali Mohamed Shein ni miongoni mwa shamrashamra za siku ya wanawake duniani.