UONGOZI wa Timu ya Mwenge FC inayoshiriki ligi daraja la kwanza kanda ya Pemba, umepongeza maamuzi ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kumaliza mkwamo uliokuwa unafukuta ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), hali iliyosababisha kurejea ligi ambayo ilisimama kutoka na hali ya sintofahamu baina ya shirikisho na Vilabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika ofisi ya timu hiyo huko Wete, Rais wa Klabu ya Mwenge Ali Macho alisema uwamuzi wa serikali wa kuingilia kati na kuondosha sintofahamu iliyopo, kati za Shirikisho la Mpira na vilabu ni jambo la kupongeza kwa nguvu zote.
Alisema kwa sasa Mwenge wako tayari kushiriki katika ligi hiyo wanachosubiri ni kutolewa kwa ratiba, huku wakikubali kucheza hata mchana ilimradi ligi iweze kumalizika kabla ya Mwezi wa Ramadhamini.
“Viongozi waliokuwepo walikuwa wakiendesha ligi kwa mabavu, sasa kila kitu kipo sawa na sisi tupo tayari kwa ligi na maandalizi tumeshaanza kufanya”alisema.
Aidha aliwataka mashabiki wa klabu ya Mwenge kuendelea kuiunga mkono klabu hiyo, kwani uongozi umeanza maandalizi kwa ajili ya kushiriki ligi hiyo.
Kwa upande Mwengeni Rais huyo wa Mwenge, litumia fursa hiyo kuiomba serikali izisaidie, kiasi cha fedha vilabu vya Pemba vinavyoshiriki ligi hiyo ili kuondokana na changamoto ya usafiri.
Ligi daraja la kwanza Kanda pemba inatarajia kuanza kutimua vumbi Machi 10 mwaka huu katika viwanja mbali mbali.