SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) Tawi la Pemba, limewataka wananchi kufuata taratibu na sheria pale wanapotaka kukata miti mikubwa iliyokaribu na miundombinu ya umeme, ili kuepusha kulitia hasara shirika hilo.
Hatua hiyo imekua baada ya matukio mbali mbali kujitokeza hivi karibuni ya kukatwa miti mikubwa na baada e kuangukia katika nyaya za umeme na kusababisha hasara kwa shirika.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi Afisa Uhusiano wahuduma kwa wateja ZECO Pemba Haji Khatib Haji, huko katika bonde la msokota Mgelema Wilaya ya Chake Chake, mara baada ya kurudishwa kwa huduma ya umeme kufuatia laini kubwa ya 33KV, kuangukiwa na mti wa mzambarau na kupelekea kukosekana kwa huduma hiyo.
Alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa nne za asubuhi, zeco iliweza kubaini tatizo hilo kwenye muda wa saa 10 za jioni, baada ya kufuatilia katika vituo vyao vidogo vidogo.
Aidha Haji aliwataka wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa ZECO pale wanapotaka kukata miti yao ili kuepusha kulitia hasara shirika, sambamna kuachana na tabia ya kuchukua hatua mikononi mwao.
“Kipindi hiki ni cha upepo mkali unavuma vizuri tukawa na tahadhari kubwa, pale tunapotaka kuchoma moto mashamba yetu au kukata miti mikubwa, vizuri pia mukawasiliana na zeco moja kwa moja ikiwa pana nguo”alisema.
Afisa Huyo aliwasihi wananchi kuendelea kudumisha umoja na mshikamoano, pamoja na kuhakikisha wanakuwa walinzi wazuri katika kulinda miundombinu ya umeme.
Kwa upande wake Miliki wa shmba ambalo limeungua moto na mzambarau kuangukia laini kubwa ya Umeme, Abeid Khamis Abeid alisema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana huku mikarafuu zaidi ya 20 ikiwa imeungua.
”Mimi mwenyewe siwezi kufanya jambo hili hata siku moja, hapa nilipo tumbo linaniuma tizama mikarafuu yangu ilivyoungua moto, hasara gani nilioipata paengine wananchi walitaka kufua asali au mtu kavuta sigara, ila hasara kwakweli ni kubwa iliyotokea”alisema.
Aidha alisema tukio lilitokea majira ya saa nne za asubuhi, huku akiyomba serikali kumuangalia kwa jicho la huruma kwani hasara kubwa ameipata.
Naye Naibu Sheha wa shehia ya Mgelema Amour Ali Zaina, alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo aliweza kuwasiliana na ZECO na kufika na kuona tatizo lililotokea.
Kwa upande wake shuhuda wa tukio hilo Issa Khamis Abeid, alisema alisikia mshindo mkubwa wa mti kuanguka na kukimbilia bondeni ndipo alipokuata mzambarau umeanguna na kutoa taarifa kwa uongozi wa sheha wa shehia.
Aidha alitaka vijana wenzake na wakulima kujaribu kufuata sheria na taratibu zake, ili kuhakikisha madhara mengine hayatokei katika shehia yao pale watu wanapotaka kukata miti.