Monday, November 25

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa yatakiwa kutoa taarifa za hali ya hewa kwa Wakulima

 

NA MWAJUMA JUMA

MENEJA Mradi wa Viungo, Amina Ussi Khamis amesema kuwa ipo haja kwa Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa kutoa taarifa za hali hiyo kwa wakulima ili kuwa na uhakika wa kuzalisha mazao yao hasa ya mboga mboga.

Meneja huyo aliyasema hayo katika mkutano wa wadau kutoka taassisi mbali mbali za Serikali ambao wanahusika katika mfumo wa utoaji tahadhari ya mapema (Early System), huko ofisini kwao Mwanakwerekwe.

Alisema kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikitoa taarifa za hali ya hewa kwa wavuvi lakini kwa upande wa wakulima bado taarifa hizo haziwafikii hali inayopelekea kushindwa kupata mazao yenye ubora.

“Lengo ya kikao hichi ni kutimiza moja ya malengo katika kuhakikisha wanatoa tahadhari ya mapema ya hali ya hewa kulingana na mazao ambayo wanazalisha”, alisema.

Kwa upande wake Afisa Lishe wa mradi huo Annastanzia alisema kuwa usalama wa chakula sio tu katika uzalishaji bali unaanzia katika suala zima la uandaaji.

Alisema waulima hasa wa mboga mboga wanakosa kujua miongo ya hali ya hewa na badala yake hulima kwa mazoea na kupelekea wakati mwengine mazao yao kuharibika.

Hivyo alisema kuna haja ya kuwa na tahadhari ya mapema juu ya hali ya hewa kwa waulima ili waweze kuwa na uhakika wa chakula.

Mradi huo wa viungo ni wa miaka minne ambao unaendeshwa katika wilaya tisa zikiwemo tano za Unguja nan ne za Pemba, chini ya ufadhili wa Jumuiya ya nchi za Ulaya kwa mashirikiano ya TAMWA, PDF na CFP.

Lengo kuu la mradi huo ni kuongeza uhakika wa chakula na kipato cha waulima wadogo wadogo wanaojishughulisha na kilimo cha mboga mboga, matunda na mazao ya viungo, pamoja na kufunguwa fursa katika mnyororo wa thamani, uzalishaji bora na utanuzi wa masoko na bidhaa.