Monday, November 25

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Ametembelea Nyumba za Maafa Tumbe Wilaya ya Micheweni Pemba

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akitembelea moja ya Nyumba za Maafa Tumbe akipata maelezo ya Mradi huo kutoka kwa Katika Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Ndg. Thabit Idarous Faina, alipofanya ziara kutembelea Mradi huo

NA ABDI SULEIMAN.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi, amewataka wananchi watakaokabidhiwa nyumba za vijiji za maafa zilizojengwa Tumbe Kisiwani Pemba na Nungwi kwa Unguja, kuhakikisha nyumba hizo wanazitunza ili zisipoteze haiba yake.

Rais Mwinyi alisema nyumba hizo hivi karibuni zitazinduliwa kwa upande wa Unguja ikiwa ni pamoja na Pemba, ili kuwafanya wananchi waliokusudiwa kuweza kuzitumia.

Dk.Mwinyi aliyaeleza hayo mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua nyumba hizo 15 kwa 30, huko katika kijiji cha Tumbe Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati waziara yake ya siku moja Kisiwani Pemba.

Aidha Rais Mwinyi aliwashukuru wananchi wa shehia ya Tumbe kuonyesha kuwa wapo tayari kwa ushirikiano na serikali yao, huku akisema kwamba changamoto zilizopo katika nyumba hizo zinashuhulikiwa ili kumailizika kwa wakati.

“Tumeambiwa kama suala la maji ni changamoto kwa sasa, ila hivi karibuni litamalizika, fedha za fidia nazo zinashuhulikiwa ndani ya wiki hii zinamalishwa na changamoto ya idadi ndogo ya watu wanaohitaji kuwepo hapa nayo inashuhulikiwa”alisema.

Katika hatua nyengien Dk.Mwinyi aliwashukuru wafadhili waliojenga nyumba hizo, Emirates Red Creasent ya Falme za Kiarabu kwa kazi kubwa walioifanya, kuhakikisha nyumba hizo wameziwekea na huduma za kijamii ikiwemo, kituo cha afya cha kisasa, skuli, msikiti na maduka.

Akizungumzia suala la Amani na Utulivu, Dk. Mwinyi aliwataka wananchi wa Unguja na Pemba, kuendelea kudumisha amani iliyopo, Umoja na mshikamano, kwani lengo la serikali ya Umoja wa Kitaifa ni kuwaunganisha watu, kwa kuachana na mifarakano iliokuweopo.

“Tumefanya hivi ili kuwaweka wananchi katika hali ya amani, utulivu na usalama ili waweze kupata maendeleo yaliokuwa bora kutka kwa viongozi wao”alisema.

Hata hivyo alisema kwa hapa tulipofikia kila kitu kipo kilichobaki ni serikali kupeleka maendeleo, huku akitambua kuwa kuna huduma nyingi za kijamii zinazohitajika, ikiwemo afya, maji, elimu barabara na hususan za vijijini, kwani aliwahidi wananchi wakati wakampeni atahakikisha kuwa huduma zote zinatatuliwa.

Kwa upande wa akinamama aliwahidi kuwa serikali itawapatia mikopo kutoka mabenk, kwani wanapaswa kujipanga vyema katika vikundi vyao, kwa kuwapatia mafunzo, mitaji na masoko, kitu watakachopewa kitakuwa na tija nao.

Kwa upande wake waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, sera uratibu na baraza la Wawakilishi Dk.Khalid Salum Mohamed, alisema nyumba hizo 15 zinazochukua familia 30 kwa wakati mmoja, pia kuna hospitali ya kisasa, soko, maduka 15, msikiti unaochukua watu 350, skuli yenye vyumba tisa.

Alisema chanzo cha ujenzi wa nyumba hizo ni athari zilizotokea mwaka 2017 za mvua kubwa ya masika, ambayo karibu familia 6500 unguja na Pemba ziliathiria, lakini watu wa Mwezi Mwekundu walikuja na kushirikiana na serikali kujenga nyumba za kuwasaidia waathirika hao.

Alisema waathirika ni wengi lakini ilionekana familia 385 ambao nyumba zao ingebidi vivynje kutokana kuwepo katika maeneo hatarishi, Pemba nzima imeoneka kuna familia 41 nyumba hizo na hao wapate makaazi hapa.

Aidha alisema kipo kijiji kama hicho Nungwi Unguja, kwa mujibu wamkataba serikali imelazimika kutengeneza barabara, Kupeleka Umeme na Maji, maji tayari visima vitatu wameshavichimba ili walifeli kutokana na uhaba wa maji, sasa wanachimba chengine na kwenda mita 90 na maji wanatarajia kuyakuta.

Kwa upande wa fidia alisema tayari walishalipa Milioni 16 na milioni 11 watazimaliza ndani ya wiki inayofuata, kati ya milioni 27 walizokua wakidaiwa za fidia.

Hata hivyo nao wananchi waliokuwepo katika eneo hilo, wameipongeza serikali ya awamu ya nane kutokana na kasi yake inavyokwenda, kwani imeonyesha kuwa karibu na wananchi wake.

Wamewataka watendaji walioteuliwa na Dk.Mwinyi, kuhakikisha wanakwenda sambamba na kasi yake na kutokumuangusha katika malengo alioyakusudiwa kuwapatia wananchi wa Zanzibar.