Monday, November 25

Waumini wa Kiislamu Watakiwa Kuitumia Misikiti Kutatua Changamoto za Kadhaa za Jamii.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiondoa kipazia kwa ajili ya ufunguzi wa Masjid Taqwa Gombani ya Kale Pemba akiwa na Mwakilishi wa Mfadhili wa ujenzi huo Bw. Humoud Mohammed,hafla hiyo imefanyika leo 12-3-2021

 

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk, Hussein Ali Mwinyi, ameutaka uongozi wa Masjid Taqwaa ulioko Gombani ya kale Chake chake Pemba, kuutumia msikiti huo kwa kutatua changamoto kadhaa za kijamii likiwemo la udhalilishaji na ukatili wa wanawake na watoto.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo mara baada ya kuufungua msikiti huo, wakati akizungumza na waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wengine, alipokuwa kisiwani Pemba kwenye ziara ya kutwa moja.

Alieleza, bado miskiti kadhaa haijatumika ipasavyo na walio wengi wanadhani ni kwa ajili ya swala tano pekee, jambo ambalo huwepo matatizo katika jamii na kushindwa kupatiwa ufumbuzi.

Alisema lazima sasa miskiti ukiwemo huo alioufungua iwe kama idara mbali mbali zitakazojadili changamoto kama suala la kuwasaidia wajane, wenye ulemavu na udhalilishaji ili yaondoke katika jamii.

Hivyo, Dk. Mwinyi alisema haitakuwa busara kuona mskiti huo uliojengwa kwa gharama kubwa, usitumike kupanga mipango na mikakati mbali mbali ya kuisadia jamii iliyopo katika eneo hilo.

“Katika karne hii tuliyonayo, bado miskiti haijatumika na tuliowengi tukishamaliza kuswali swala tano, ndio kazi imekwisha kumbe tunamakundi kama ya wajane ambayo yanachangamoto mbali mbali,’’alieleza.

Katika hatua nyingine Rais huyo wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, alisema serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha ahadi alizoziweka anazitekeleza hatua kwa hatua.

Alieleza kuwa, anaelewa vyema changamoto zilizomo ndani ya jamii kwenye sekta ya miundombinu ya barabara, afya, maji safi na salama pamoja na elimu, hivyo atahakikisha anaimarisha.

Aliwataka waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wengine kumuombea dua kila wakati ili afanikishe malengo na kutekeleza ahadi zake alizowaahidi wananchi hao.

“Naomba niwakumbushe kuwa, nakumbuka kuwa nna ahadi kwenu ambazo niliwaahidi, hivyo malengo na dhamira nnayo, kwa hiyo  niombeeni dua ili nifanikishe hayo,’’alieleza.

Kuhusu amani na utulivu, uliopo Rais huyo wa Zanzibar, alisema serikali itafanya kila juhudi kuhakikisha inadumu, ili wananchi wafanye shughuli zao za maendeleo kwa ufanisi.

Alisema, ataendelea kusisitiza jambo hilo kila anapokutana na wananchi, kwani ndio msingi wa kila jambo, katika nchi na jamii kwa ujumla.

“Hata khatibu wetu wakati anatupa daawa alieleza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwetu na kutumia aya mbali mbali, sasa na mimi nitaendelea kulisisiti jambo hilo,’’alifafanua.

Akizungumzia hofu waliyokuwa nayo baadhi ya wananchi wa Zanzibar mara baada ya kifo cha Makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad Febuari 17, juu ya kuendelezwa maridhiano, aliwatoa hofu.

Alisema kwa bahati nzuri amepatikana Makamu wa kwanza wa rais ambae tayari ameshakaa nae na kumuahidi kuendeleza maridhiano na umoja wa wazanzibari kama ilivyo azma ya serikali iliyopo.

“Wananchi wala musiwe na hofu, kuwa muasisi wa maridhiano haya ameshatangulia mbele ya haki, bali tumepata Makamu mwengine wa kwanza na yuko vizuri katika kuimarisha umoja, mshikamano na kutunza amani,’’alisema.

Mapema Katibu wa Mufti Zanzibar sheikh Khalid Ali Mfaume, alisema kuna malipo makubwa kwa aliyejenga msikiti, ikiwa ni pamoja na kuwa na makaazi kwenye pepo ya Allah.

Alisema kilichobakia sasa baada waumini wa dini ya kiislamu wa Gombani kujengewa msikiti huo, ni kuutunza na kuanzisha idara ambazo zitaijenga jamii.

“Lazima kuwe na Idara ambazo zitatunza mskiti, kushughulikia suala la taaluma pamoja na kuwa na vikao vya kutatua changamoto kadhaa zilizomo ndani ya jamii,’’alieleza.

Akizungumza kwa niaba ya mfadhili wa msikiti huo, sheikh Mohamed Suleiman Khalfan, alisema wameamua kuujenge msikiti huo baada ya uliyokuwepo kuwa na nafasi finyu kwa waislamu.

“Leo (jana) tumefurahishwa mno na ujio wa rais wa Zanzibar katika ufunguzi wetu, maana alikuwa na uwezo wa kuwatuma wasaidizi wake, hii inaonesha imani yake kwenye mambo yak heir,’’alieleza.

Akisoma risala ya wauimini wa dini ya kiislamu wa Gombani pamoja na wananchi wengine, Ustadh Hamad Mussa Rashid alisema jina la ‘Taqwaa’ la mskiti huo liliasisiwa na Mufti wa sasa wa sheikh Saleh Omar Qaabi mwaka 1988.

Alisema wakati huo palikuwa na msikiti mdogo, ambao baadae waliomba ufadhili ili kujengewe mkubwa, kutokana na wakati huo kuzidiwa na waumini.

“Leo kwetu wananchi na waumini wa dini ya kiislamu hapa Gombani na Chake chake, tumefarajika mno kuona tunahamia kwenye msikiti ambao umeshaondosha tatizo la sehemu ya kufanyia ibada,’’alieleza.

Alisema msikiti huo ambao unatarajiwa kuwa na ghorofa mbili, juu na ghorofa ya kwanza ni kwa ajili ya ibada ya swala na ghorofa ya pili kwa ajili ya madrasa ya watoto wao.

Akisoma hutuba mbili ya swala ya Ijumaa sheikh Khalifa Mrisho Omar, alisema rais Alhajj Dk. Mwinyi amekuwa na sifa nzuri ya kujali shida na matatizo ya wananchi wake.

“Kiongozi wetu huyu amekuwa na sifa za kipekee, kwa kule kuwa karibu na wananchi na kujali na kufuatilia kwa karibu changamoto zetu,’’alieleza.

Ujenzi wa masjid taqwaa ambao ulianza Febuari 2, mwaka 2019 kwenye eneo lake la chini ambalo limejengawa sasa unauwezo wa kusaliwa na waumini 840 wanawake na wanaume, na umegharimu shilingi milioni 600.

Hata hivyo  ukimaliza ghorofa zote mbili, utakuwa na uwezo wa kusaliwa na waumini 2000, huku Rais wa Zanzibar akiahidi nae kuchangia katika uendelezaji wa ujenzi wa mskiti huo.