Monday, November 25

Tanzania yajivunia Mafanikio miaka 40 ya SADC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi akifuatilia kwa makini mjadala unaoendelea katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya Maendeleo Kusini mwa Afrika- SADC Jijini Dar Es Salaam

Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika -SADC, wakisikiliza mada kwa nia ya Mtandao katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere -JNICC Jijini Dar es Salaam unaoendelea kwa siku mbili, huku leo ikiwa ni siku ya kwanza.

Na Beatrice Sanga,

Wakati Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ikiadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, Tanzania ikiwa ni sehemu ya umoja huo inajivunia mambo mbalimbali ikiwepo Kiswahili kutumika kama miongomi mwa lugha kuu za mawasiliano kwa viongozi Wakuu na Mawaziri wa Nchi hizo

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa jumuiya hiyo, Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuingia kwa Kiswahili katika SADC ni uamuzi uliofanywa katika kikao cha 39 cha wakuu wa nchi hizo

“katika kikao cha 39 cha wakuu wa Nchi wa SADC iliamuriwa Kiswahili iwe ni lugha ya nne ya SADC na kitumike katika mikutano ya baraza la mawaziri na mkutano wa wakuu wa nchi, lakini sasa imeamuliwa Kiswahili kitatumika  sio tu katika mikutano hiyo miwili lakini katika mikutano yote ya kisekta yani mikutano ya sekta ya Afya, sekta ya elimu, sekta ya uchukuzi, kwahiyo sasa Kiswahili kitatumika pia katika ngazi ya sekta ambayo ni hatua kubwa iliyofikiwa”, amesema Prof. Kabudi.

Aidha prof kabudi amesema katika kikao chao cha Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo kinachoendelea kwa njia ya mtandao watajadili na kukamilisha mchakato wa utengenezaji wa Sanamu maalumu ya Baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambayo itawekwa katika Jengo la Amani kwenye makao makuu ya Umoja huo Mjini Addis Ababa Nchini Ethiopia  ikiwa ni maamuzi yaliyofanywa  na SADC takribani miaka miwili iliyopita

“kwa miaka takribani miwili sasa,Jumuiya ya SADC iliamua kutengeneza sanamu maalumu ya baba wa Taifa mwalimu Julius kambarage nyerere ambayo itawekwa jengo la Amani, kule Addis Ababa Ethiopia, mchakato unaendelea na tunaamini katika kikao hichi tutakamilisha mchakato wa kumpata mtu atakayeifua hiyo sanamu ya mwalimu Julius kambarage nyerere,” amesema Prof Kabudi.