NA ABDI SULEIMAN.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar Dk.Sada Mkuya Salum, amesema katika kupambana na kesi za dawa za kulevya nchini, kunahitajika mashirikiano ya pamoja kwa vyombo vyote vya sheria, ikiwemo jeshi la Polisi na Mahakama ili kudhibiti uwingizaji na matumizi ya dawa hizo.
Waziri Mkuya aliyaeleza hayo katika tume ya kitaifa ya kuratib na udhibiti wa dawa za kulevya, mjini Chake Chake ikiwa katika ziara yake ya kwanza Kiswani Pemba, kujitambulisha kwake tokea kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Alisema iwapo mashirikiano hayo hayatakuwepo kwa taasisi hizo, basi kasi ya matumizi ya dawa hizo yatazidi kuongezeka na vijana ndio waathirika wakubwa katika taifa, jambo ambalo litapoteza nguvu kazi ya taifa.
Mkuya alisema kumekuwepo na tabia za kurudisha nyuma juhudi za kupambana na madawa ya kulevya, kutokana na baadhi ya taasisi kushindwa kutoa hukumu ipasavyo, huku washtakiwa wa madawa ya kulevya wakiendelea kudunda mitaani.
“Hivi vita ni vikubwa sana vya madawa ya kulevya, tena wafanyabiashara wa dawa hizi ni watu wenye pesa, lazima juhudi za makusudi zinahitajika katika kudhibiti suala hilo”alisema.
Aidha mkuu huyo alisikitisha na watendaji wa jeshi la Polisi Wilaya ya Micheweni, kushindwa kuripoti matukio ya dawa hizo kwa kipindi cha 2019 na 2020 licha ya wilaya hiyo kuwa na bandari bubu nyingi na milango mikubwa ya uongizaji kutoka nje ya nchi.
Hata hivyo alisema ni mwaka 2018 tu pekee ndio ulioripotiwa dawa za kulevya kukamatwa aina ya Bhang gram 22.69, huku akiwataka watenda kuongeza nguvu katika vita hivyo.
Katika hatua nyengine alisema jeshi la polisi kazi yake ni kufanya operesheni, iwapo halitochukua hatua za makusudi basi wataweza kuchafua picha ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, licha ya kuwa ukanda wa bahari ya Zanzibar ndio njia kuu ya kupitisha madawa hayo kutoka mataifa makubwa.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Ahmed Abubakar Mohamed, alisema uwepo wa bandari bubu ni njia moja wapo ya uwingizaji wa madawa ya kulevya nchini, huku akilitaka jeshi la Polisi kisiwani Pemba kuongeza bidii ya msako wa dawa hizo.
Alisema bandari hizo ni moja ya sehemu hatarishi sana, kwani zimekuwa zikitumiwa vibaya sana katika suala zima la magendo na mambo mengine.
Naye afisa udhibiti na uchunguzi kutoka Tume ya kitaifa ya kuratib na udhibiti wa dawa za kulevya Pemba, Iptisam Fadhili Khamis, alisema kumekuwepo na Makosa kwa watuhumiwa wa matendo hayo kupewa dhamana kinyume na sheria wanapofikishwa katika mahakama.
“Mheshimiwa Waziri hizi kesi ni nzito sana, kumekuwa na tabia kwa watuhumiwa wa kesi hizi wanapofika mahakamani wakati wmengine wanakuwa wameshalewa, chakujiuliza pombe au kinachowafanya wale wanapata wapi na wakuwa mahabusu, sasa mtu huyo ataweza kusema lolote akiwa katika hali hiyoo”alisema.
Aidha alimtaka waziri huyo kuifuatilia kwa kina mahakamani keshi inayomkabili mtuhumiwa aliejulikana kwa jina la Haji Rashid Khami “J”, Khadija J Shaha, Neema na Asia Luciano wa Msingini Chake Chake, alikutwa na kete 422 za Heroin zenye uzito wa 6.61063 gram, kosa la pili kukutwa na Kete 7025 za unga aina ya Heroin yenye uzito wa gram 153.4 na kosa la tatu kukutwa na Bangi nyongo 553 zenye uzito wa gram 548.2, lakini tayari watuhumiwa wa kesi hizo wameshaachiwa.
Naye Ahmed Khamis Kombo afisa Udhibiti na Uchunguzi kutoka Tume hiyo, alimtaka waziri huyo kuhakikisha kicheweni kunafanyika kwa doria za mara kwa mara juu ya kudhibiti matukio hayo.