Monday, November 25

Mh Hemed:Serikali haitomvumilia Mkandarasi atakaeshindwa kufuata sheria na taratibu

 

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alionya kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitomvumilia Mkandarasi yeyote wa Kigeni aliyepewa jukumu la kusimamia Miradi ya Ujenzi na akashindwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa hapa Nchini.

Akiendelea na ziara yake ya kwa siku ya Tatu kutembelea Wilaya za Zanzibar akiwa Wilaya ya Kaskazini A kukagua Maendeleo na changamoto zinazowakabili Wananchi wa Wilaya hizo hapo kituo cha mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji Kibokwa Mh. Hemed haitasita kumuondosha Nchini ndani ya Saa 24 Mkandarasi mkorofi.

Alisema kitendo cha baadhi ya Viongozi wa Kampuni ya Sino inayohusika na ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Umwagiliaji Kibokwa  cha kuwasumbua na kuwanyanyasa Wafanyakazi wake Wazalendo hakiridhiwi kabisa na Serikali.

Katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo Mheshimiwa Hemed ameuagiza Uongozi wa Kampuni hiyo yenye makao Maku yake Nchini Jamuhuri ya Watu wa China kuwalipa Wafanyakazi wake wote Stahiki zao ndani ya kipindi cha Wiki Moja zoezi ambalo liende sambamba na uwasilishaji wa vielelezo vyote vya Mikataba kwa Mkuu Wa Mkoa wa Kaskazini katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Hemed amewahakikishia afanyakazi Wazalendo wa Kampuni hiyo kwamba hawataonewa tena kuanzia sasa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia suala hilo bila ya kumuonea Mtu au Taasisi ya aina yoyote.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa Wafanyakazi hao baadhi yao kuacha tabia ya udokozi ikiwemo kunyonya mafuta ya vyombo vya Moto vyenginevyo Serikali kupitia vyombo vya Dola haitasita kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kufukuzwa Kazi.

Mapema  Kamishna wa Kazi Zanzibar Bibi Fatma Iddi Ali alisema Kampuni ya Ujenzi ya Sino imekuwa na matatizo mengi yanayopelekea kutokea sintofahamu kati yake na Wafanyakazi inayosabishwa na usiri wa mikataba.

Bibi Fatma Alisema sheria ya Kazi ziko wazi katika kuona Muajiriwa na Mfanyakazi wake wanafikia makubaliano katika suala zima la malipo yaani mishahara jambo ambalo kwa Kampuni ya Sino imeshindwa kukamilisha suala hilo la Kiheria.

Akiendelea na ziara yake kwa kuwatembelea Wananchi wa Miradi ya uanikaji wa Dagaa Fungurefu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla  alizipongeza Wizara ya Maendeleo ya Biashara na Viwanda na ile ya Uchumi wa Buluu kwa jitihada zilizochukuwa katika kuona Mradi wa Dagaa unajengewa mazingira ya kudumu.

Mh. Hemed alieleza kwamba jitihada hizo zilizoainisha kuanzishwa kwa mradi Maalum wa Kuimarisha Kituo hicho kitakachokuwa na uwezo wa kutoa ajira zaidi ya Hamsini Elfu zinafaa kupongezwa na wadau wote wa maendeleo.

Aliwahakikishia Wananchi hao wa Fungurefu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia vilivyo katika kuona harakati za Wananchi hao katika kujikimu kimaisha kupitia Miradi yao zinatengamaa.

Akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Kidagoni na Nungwi baada ya kupokea kero zao Makamuwa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwakumbusha Wananchi hao hasa Akina Bada kuzingatia Maadili ili kukabiliana na tabia chafu inayoathiri ukanda huo.

Alisema vitendo viovu vinaweza kuzuiwa endapo Wananchi wenyewe watakusudia kupambana nayo kwa kuzingatia uadilifu.

Alihimiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Vikundi vya Ulinzi shirikishi ili kupungua changamoto ya kuporomoka kwa maadili katika kuendeleza mila slka na Utamaduni wa asili.

Akitoa Taafira ya Maendeleo ya Wilaya ya Kaskazini A hapo ukumbi wa Mikutano wa Jeshi la Kujenga Uchumi {JKU} Upenja Mkuu wa Wilaya hiyo Nd. Sadifa Juma Khamis alisema doria za mara kwa mara zinazoendelea kufanya ndani ya Wilaya hiyo ndizo zilizopelekea kuifanya Wilaya hiyo kuendelea kuwa katika hali ya Amani na Utulivu.

Nd. Sadifa alisema Doria hizo hufanywa kwa lengo la kupunguza vitendo viovu kama vile uasharati ambapo Wanawake Wanane walikamatwa pamoja na Gari 15 zilishikiliwa kwa kujihusisha na Uchimbaji Mchanga, wakati matukio 44 ya udhalilishaji yaliripotiwa.

Akigusia matatizo ya ArdhiNd. Sadifa alisema matukio 148 yaliripotiwa na Kumi kati yake yameshapatiwa ufumbuzi huku Masheha Wawili wameshawajibishwa kwa kufukuzwa Kazi kuhusika na migogoro hiyo ya Ardhi kunakotokana na tatizo la umiliki. Mipaka pamoja na kupoanda kwa thamani ya Ardhi.

Naye kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema wakati umefika sasa kwa Wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wajipange upya wakati huu wa mpito wa Taifa kuelekea katika Uchumi wa Buluu ili fursa zitakazotokana na Sekta hiyo ziweze kuwanufaisha.

Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema migogoro ya Ardhi inayotokea ndani ya Mkoa huo akitolea Mfano wa Kijiji cha Nungwi inaweza kuviza muelekeo huo na akawataka Wananchi kuwa na subra wakati Serikali ikijipanga kuhakikisha Kijiji hicho kinachoelekea kuwa Mji Mdogo kipate mfumo sahihi wa Mipango Miji.

Alisema Serikali ya Mkoa wa Kaskazini haitasita kuchukuwa jitihada zaidi katika kuona Wananchi wake wanapata Elimu ya kutosha ili kuwafanya Wananchi wake wanakwenda sambamba na mfumo mzima unaotoakiwa na Serikali.

Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alibahatika pia kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Bandari ya Mkokotoni unaogharamiwa na Serikali yenyewe kupitia Shirika la Bandari Zanzibar ambao uko hatua nzuri katika Ujenzi wake.

Alionyesha kuridhikwa kwake kwa vile mabadiliko ya nyongeza ya Mita 30 zikitanguliwa na zile za mwanzo Mia 170 za Bara bara kuelekea Baharini hatiaathiri gharama za ujenzi huo ambazo Serikali Kuu isingefurahia wakati kipindi hichi inajitahidi kuona mapato yake yanaendelea kudhibitiwa.

Halkadhalika Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionyesha kutoridhika kwake na kusita kwa ujenzi wa Kituo cha Afya kiliopo katika Kijiji cha kidagoni ambapo alilazimika kuchangisha mchango wa papo kwa papo uliosaidia kuibua zaidi ya Shilingi Milioni 26,200,000/- zilizoambatana na ahadi ya Mifuko 15o ya saruji na bati zote zitakazoezekea Jengo hilo.