Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe Othman Masoud Othman amezitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na Idara ya Mazingira kufanya upembuzi wa kitaalamu wa athari za mabadiliko ya tabia nchi ili kubaini maeneo ambayo yameathirika baada ya maeneo mengi Visiwani Zanzibar kukumbwa na hali hiyo na kutishia maisha ya wakaazi wake.
Makamu wa Kwanza aliyaeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kuzitembelea Idara zilizo chini ya Afisi yake na kufanya mazungumzo na wakuu wa taasisi hizo Maruhubi Wilaya ya Mjini .
Alisema maeneo mengi yameathiriwa na mabadiliko ya tabianchi na hivyo kuwataka wataalamu hao kutumia uwezo wao ili kuyahami maeneo yaliyoathiriwa yakiwemo makaazi ya watu, maeneo ya kilimo na fukwe.
Akitolea mfano wa baadhi ya maeneo hayo Makamu wa Kwanza wa Rais yakiwemo Kaskazini Pemba eneo la Msuka ambapo tayari maji ya bahari yameshaingia hadi kwenye makaazi ya watu na kuanza kuangusha Minazi na miti mengine.
“Lakini tatizo jengine kubwa hasa kisiwani Pemba bahari imeingia maeneo ya watu na kwa hali hii ardhi yetu inaweza kupungua na wasiwasi mkubwa kama tunaweza kubakia na mikoko mitupu” alisema Makamu huyo.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo Zanzibar kuna haja ya kutumia wataalamu wa ndani na nje kuongeza ardhi ya Zanzibar na kutolea mfano wa Ujenzi wa kufukia bahari uliofanywa na kampuni ya Salim Said Bakhresa katika eneo la Maruhubi.
Mhe.Othman amesema wakati umefika wa kujipanga na kutathmini ikiwemo kuja na mkakati ambao utaonesha mpango mzima wa kuwa na maeneo ambayo yatafanyiwa tathmini ya kimazingira kwa kuyagawa maeneo ya makaazi na ukulima bila kuathiri mazingira.
Alisema bahari nayo inachukuwa ardhi kwa kiasi kikubwa na kuwataka wataalamu wa Idara hiyo itumie na kutafuta wataalamu kwa ajili ya kuongeza Ardhi ya Zanzibar kwa kile alichokieleza kuwa eneo kubwa limeathiriwa na Mabadiliko ya tabianchi.
Aidha alifahamisha kuwa zipo nchi ambazo ziko vizuri kwa utaalamu wa kupanga mji kwa kutumia ardhi ndogo na kuongeza ardhi kulingana na matumizi hivyo ni vyema Zanzibar kukawa na utaalamu huo baadala ya kuomba msada wa fedha.
Alifahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mkazo na muelekeo mkubwa wa kujenga nchi kitaalamu na kuzingatia mahitaji ya baadae kwa maslahi ya wananchi wake na kulinda na kuhifadhi mazingira yake .
Sambamba na hilo alieleza uwepo wa mashamba ya Eka bila kushughulikiwa jambao linalopelekea kuongezeka athari za mabadiliko ya tabia nchi kutokana ardhi hiyo kufanywa jangwa kinyume na matumizi ya awali au kujengwa nyumba zisizozingatia mpango maalum.
Pia alitaka Idara ya Mazingira na Mamlaka ya usimamizi wa mazingira kuwa wabunifu na kuwazawadia wale wanaofanya vizuri katika uhifadhi na utunzaji mazingira pamoja na kufuata sheria za kufanya tathmini ya kimazingira kwa kuandaa Zawadi maalumu kutokana na juhudi zao iwe kwa muekezeji au wananchi na taasisi za Serikali.
Tunzo hii au zawadi sio lazima kutoa gari lakini tunaweka vigezo vyetu vya kuipata hiyo zawadi ambayo itatoa hamasa ya kila mmoja kuyatunza mazingira” alisema.
Alisema haiwezakani taasisi kutoa adhabu tu na kusema iko haja kuwajengea hamasa wale ambao hutunza mazingira kwa kile alichosema wengine wanafanya vizuri kwenye ulinzi wa mazingira.
“Tukifanya hvyo ni Imani yangu itatuleta karibu na jamii na kuona kuwa na wao wanathaminiwa” alisema makamu.
Pia makamu huyo aliwata idara zoote zinazojishuhulisha na mazingira ni vyema kufanyakazi kwa pamoja ili kueta ufanisi wa haraka.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usimamizi wa Mazingira Zanzibar Sheha Mjaja Juma alisema Idara yake imekabiliwa na Changamoto kubwa ya ambalo linawafanya watendaji wengine kukosa sehemu ya kufanya kazi.
Alisema leo afisi hiyo ina gari moja tu na tena iliyochoka wa kile alichokieleza Spana Mkononi.
Makamu wa kwanza katika ziara yake hiyo pia aliweza kufika katika Afisi za Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na udhibiti wa Madawa ya Kulevya.