Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza na Wafanyakazi na Viongozi wa Taasisi zilioko katika Ofisi yake wakati wa ziara kutembelea Taasisi hizo
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Idara za Ofisi ya Makamu wa Kwanza baada ya kumaliza mkutano na Viongozi hao.
Na.Raya Hamad OMWKR.
MAKAMU wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI hapa nchini, lakini hali ya maradhi hayo ni kubwa.
Makamu wa Kwanza Rais, alieleza hayo jana katika Ofisi za Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC), katika mfululizo wa ziara za kutembelea ofisi zilizomo chini ya Ofisi yake, kwa lengo la kujuana na kuangalia utendaji katika ofisi hizo.
Makamu huyo alisema, jitihada mbali mbali zinahitajika katika kukabiliana na maambukizi ya maradhi hayo, pamoja na kuwepo changamoto mbali mbali.
Alifahamisha kuwa kiwango cha watu 6,000 waliobainika kuishi na virusi vya UKIMWI ni kikubwa, ambapo maambukizi yanaweza kuongezeka pasipowekwa mikakati madhubuti.
Alisema, pamoja na mafanikio ya ZAC katika kukabiliana na kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI, lakini mafanikio hayo bado yana changamoto zake, iwapo hukubadili mbinu watu hawatakupima kwa jana, bali watakupima kwa leo na kesho yako.
“Na katika jambo hili kila ukifanikiwa watu wanaona tatizo limeondoka kwa mafanikio, lakini yanakuja na mengine, hatukuwa na corona leo hadhiti zote kwa mfalme covid19, watu wanasahau habari za UKIMWI na mengine yote”, alifahamisha Makamu wa Kwanza wa Rais.
“Nadhani hili litusaidie katika kutazama mbinu mpya tunazoweza kuzitumia, za kuwakumbusha watu kwa sababu kwa Zanzibar yetu ukisema watu 6,000 au 0.4 au 0.5 watasema hapo hamna kitu sasa wataogelea wanavyopenda”, aliongeza.
Alisema, unapomwambia mtu watu 6,000 maana yake ni sawa na Jimbo zima kwa Zanzibar, na hiyo inaweza kumshitua mtu zaidi kuliko kumpa kwa asilimia, si kwa nia ya kutisha lakini inaweza kuonyesha kuwa kuna tatizo ili watu waweze kuchukua tahadhari.
“Ikiwa kama kuna watu 6,000 maana yake katika majimbo 50 ya Zanzibar ni sawa na jimbo zima, lina titizo hilo”, alifahamisha.
Hivyo aliimba ZAC kufanya kila jitihada za kuwafikia watu popote pale walipo, ili kutoa elimu juu ya athari za maradhi hayo ili jitihada za kuepukana nazo ziweze kuchukuliwa.
Mapema, Mkurugenzi wa Tume wa UKIMWI Zanzibar (ZAC), Dk. Ahmed Mohammed Khatib, alimueleza Makamu wa Kwanza wa Rais kwamba, Tume hiyo tokea kuanzishwa kwake imepata mafanikio ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI, licha ya changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo.
Katika mafanikio hayo, ni pamoja na kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI kuwa chini ya asilimia moja, ambapo kwa utafiti wa mwaka 2016/2017 ambao unaonyesha kun asilimia 0.4 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, ambapo upande wa Unguja ni asilimia 0.5 na Pemba 0.2 ambao ni sawa na watu 6,000.
Wakati huo huo, Makamu wa Kwanza wa Rais, alitembelea Idara ya Watu wenye Ulemavu Migombani na kufanya mazungumzo nao, na kuwataka kushirikiana na Wizarailiyo chini ya Ofisi yake, ili kufanyakazi kwa ufanisi.