NA ZUHURA JUMA, PEMBA
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na taasisi mbali mbali zisizo za kiserikali ambazo zina nia ya kuwaletea maendeleo wananchi wa visiwa vya Zanzibar.
Alisema kuwa suala la mashirikiano kwa taasisi hizo kwa upande wa Serikali halina shida,hivyo alizitaka taasisi ambazo zina nia ya kuwekeza nchini zinakaribishwa.
Makamo aliyasema hayo huko katika Kijiji cha Daya Mtambwe wakati alipotembelea kituo Cha kukaushia mazao ya matunda na viungo wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Wilaya ya Wete hapo juzi.
Hemed aliitaka jumuia ya CFP kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar na kuihakikishia kuwa wanaunga mkono juhudi za jumuia hiyo.
“Suala la mashirikiano kwetu sisi halina wasiwasi kwani mmeweza kuisaidia Serikali sana na tutaendelea kuthamini michango yenu mnayoitoa kwa jamii muda wote,”alisema Makamo.
Mapema Makamo aliziagiza Wizara ya Kilimo,Wizara ya Biashara na maendeleo ya viwanda, Wizara inayoshughulikia uwekezaji kwa pamoja kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba na Wilaya ya Wete kushirikiana na viongozi wa jumuia hiyo ili kuhakikisha kazi ya ujenzi wa kiwanda hicho unamalizika na kuweza kufanya kazi yake.
“Jengo hili halitotusaidia kitu ikiwa halitafanya kazi ambayo imekusudiwa, hivyo juhudi kubwa inahitajika ili kuona eneo hili linajengwa kwa haraka,” alisema Makamo.
Sambamba na hayo Makamo alieleza kuwa wakati wa kulitumia jengo hilo ni kuhakikisha linalenga kuwasaidia wananchi na sio vyenginevyo.
“Jumuia zote ambazo tutakubaliana kusimamia mashine hizi nakuombeni sana lazima Serikali ishirikishwe kikamilifu ili tuone mipango inayofanywa hapo ionekane inafanywa kwa utaratibu na sheria zote za nchi,”alieleza Makamo.
Akisoma taarifa fupi ya mradi huo Mkurugenzi wa Community Forest Pemba (CFP) Mbarouk Khamis alieleza kuwa jumuia yake imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Aidha Mbarouk alieleza kuwa mbali na shughuli za kuwaletea maendeleo wananchi wake na kujiongezea kipato,lakini pia CFP imekuwa imekuwa mstari wa mbele kuwahimiza wananchi kutunza mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwashajihisha kupanda miti ya aina mbali mbali ambapo katika mwezi uliopita CFP kwa kushirikiana na Idara ya misitu na jamii ya watu wa Tumbe mashariki iliweza kupanda miti aina ya mikandaa ipatayo 21000.
“Jumuia yetu imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwahamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kuhifadhi mazingira katika maeneo yao,”alieleza Mbarouk.
Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo alifahamisha kuwa ujenzi wa “solardrier”(mashine ya kukaushia mazao) ni sehemu ya mradi wa mabadiliko ya tabianchi ambapo mashine hizo zilifungwa rasmi mwaka 2019 na gharama zake ni zaidi ya Tsh, 25 milioni, ambapo ujenzi wa ofisi unatarajiwa kugharimu zaidi ya Tsh,8 milioni, kiujumla gharama zote ni zaidi ya Tsh 33 milioni.
Mbarouk alisema kuwa ujenzi wa mashine hiyo umekusudia kuboresha kwa kiwango Cha juu na kuongeza thamani mazao ya wakulima wa Kisiwa Cha Pemba na kuwapa uhakika wa mauzo katika masoko ya ndani na nje kwa ujumla.
“Tunategemea ‘solardrier’ hii itakuwa chemchem ya uzalishaji wa mazao ya viungo ‘spice’, matunda na mboga mboga kwa Kisiwa Cha Pemba na kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza pato kwa jamii na Serikali kwa ujumla na kukuza sekta ya utalii hapa nchini,”alieleza Mkurugenzi.
Mbarouk aliwatahadharisha wananchi wa Mtambwe na maeneo mengine kuwa mashine hizo ya jamii, hivyo ni wajibu wao kuzitunza na kufuata maelekezo watayopatiwa na wataalam.
“Hizi mashine sio za watu wa Mtambwe bali ni za jamii kwa ujumla, Ninachowasisitiza ni kuzitunza na kufuata maelekezo ambayo watapatiwa na wataalamu kwa wale ambao watapewa jukumu la kuzisimamia,”alisema Mbarouk.