Monday, November 25

ZFDA imetiliana saini na TBS

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WAKALA wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) imetiliana saini na shirika la Viwango Tanzania TBS ya kufanya kazi kwa pamoja, ili kufanya taasisi hizo ziweze kufanya kazi pande za Tanzania Bara na Zanzibari.

Zoezi Hilo la utiaji saini lilifanyika katika Ukumbi wa hoteli ya Mkoani ambapo kwa upande wa Wakala wa Chakula na Dawa (ZFDA) saini imetiwa na Mkurugenzi Mtendaji Burhan Othman Simai huku Wakala wa Viwango Tanzania (TBS) saini imetiwa na Mkurugenzi Mkuu Dk: Athuman Yussuf Ngenya.

Akizungumza baada ya utiaji saini hiyo, Mwenyekiti wa bodi wa ushauri kutoka(ZFDA) Mayasa Salim Ali aliwataka wafanyabiashara wa Zanzibar kusjili biashara zao kwa ZFDA na kwa Tanzania Bara kwa TBS kwani zile changamoto ambazo walikuwa wakizipata Kati ya Zanzibar na Tanzania Bara zimepatiwa ufumbuzi.

Aidha Mwenyekiti huyo aliwasihi wafanyabiashara kuingiza bidhaa zenye ubora wa Viwango ili kuimarisha afya za wananchi na kulinda mazingira ya Nchi yao.

Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa makubaliano hayo yataimarisha ufanyaji wa biashara nchini na kupata bidhaa zenye ubora wa Viwango na salama kwa matumizi ya binaadamu.

“Makubaliano yetu haya yataweza kuwafanya wafanyabiashara na wajasiriamali hasa wa Zanzibar kuuza bidhaa zao katika masoko yote ya Bara kwani hapa awali walikuwa wakilalamika kuwa hata kama Wana kibali kutoka ZFDA walikuwa hawapati fursa ya kuuza biashara zao Tanzania Bara,”alisema Mayasa.

Mapema Mayasa alisema kuwa ZFDA itakuwa karibu na wafanyabiashara kwa kufuatilia yeyote ambae atakiuka masharti hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kusimamishwa biashara yake.

“Kikubwa wanachotakiwa wafanyabiashara na wajasiriamali kwa ujumla kuwa huru na kufanya biashara nzuri na kufuata taratibu zetu, vibali ni muhimu na tutawakagua na tutawatembelea katika maeneo yao, jambo kubwa ni kujisajili tu,”alifahamisha Mwenyekiti.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dr, Burhan Othman Simai aliipongeza kamati iliyoandaa makubaliano hayo katika kukuza na kuendeleza mashirikiano katika nyanja mbali mbali za udhibiti wa bidhaa za Chakula na Vipodozi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha alizipongeza menejimenti za taasisi hizo kutokana na kuridhia utiwaji saini makubaliano hayo ambayo yatatoa fursa kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili kufanya kazi zao bila ya tatizo lolote.

“Napenda kuwahakikishia kuwa ZFDA itaendelea kutumia uzoefu wake iliyoupata katika ushiriki wa uwiano kupitia mashirikiano ya kikanda (EAC) na Umoja wa Afrika kwa takriban miaka kumi,” alisema Burhan.

Sambamba na hayo Burhan alieleza kuwa atahakikisha ZFDA itatoa kila aina ya mashirikiano ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa kwa kiwango Cha hali juu kama ilivyokusudiwa.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa TBS Athuman Yussuf Ngenya alieleza jukumu kubwa la taasisi hizo mbili ni kuwalinda wananchi wake wanapata Chakula na Vipodozi vilivyobora ambavyo visivyoweza kuleta madhara kwa watumiaji wake.

Aidha Yussuf alifahamisha kuwa wananchi wa nchi mbili hizi wamekuwa na muingiliano mkubwa, hivyo haiwezekani bidhaa ambayo inatengenezwa upande mmoja isiweze kuuzwa upande mwengine, hivyo taasisi hizi zimeona ni vyema kushirikiana pamoja ili kuhakikisha wanawalinda wananchi wao kudhibiti Chakula na Vipodozi kwa sehemu zote.

“Baada ya kuungana kwetu huku wafanyabiashara wa pande zote mbili wategemee mafanikio makubwa ila tunachowasisitiza ni kusajili bidhaa zao kwa upande wa Zanzibar ni ZFDA na bara ni TBS,” aliaeleza Mkurugenzi.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo aliihakikishia ZFDA na Serikali kwa ujumla kwamba watashirikiana vizuri na hakuna shaka TBS wako imara na wako tayari kushirikiana kwa mengine.

Nae Mwakilishi kutoka Wizara ya Viwanda na biashara Tanzania Bara Nouh Mkasanga alizipongeza ZFDA na TBS kwa hatua waliyofikia baada ya kuona changamoto zilizokuwepo kwa wafanya biashara wa nchi hizi.

Nouh alifahamisha kuwa kwa upande wa Wizara yake jukumu kubwa ni kuhakikisha mazingira ya biashara yanaboreshwa ili biashara ziweze kufanyika kwa urahisi na hatimae Uchumi uweze kukuwa kwa kasi zaidi.

“Kwa sababu hati hii ya makubaliano lengo lake ni kurahisisha ufanyaji wa biashara, kwetu sisi ni faraja kubwa na hivyo itapelekea kuharakisha juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya biashara,” alifahamisha Nouh.

Hata hivyo Mwakilishi huyo alisema kuwa kutokana na kauli za Wakurugenzi wa TBS na ZFDA  kwamba bodi mbili hizi zitaweza kutoa mashirikiano makubwa ili kuhakikisha majukumu hayo yanafanyika ipadavyo.

Nae Mwakilishi kutoka Wizara ya afya Pemba Abduu Salim Mohammed alieleza kuwa mashirikano ya yaaaisi hizo mbili itakuwa ni faraja kwa wafanyabiashara wa pande zote mbili kuuza biashara zao katika Mikoa yote ya Tanzania.

“Makubaliano haya naamini yamezingatia hali za pande zote mbili,kwa maana hiyo itapelekea kuleta ule Utanzania halisi,”alisema Abduu.