NA ZUHURA JUMA, PEMBA
OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Mkoa wa Kaskazini Pemba inatayarisha mafunzo maalumu ya mbinu bora za upelelezi kwa maafisa wake waliopo katika wilaya mbili za mkoa huo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwanasheria Dhamana wa mkoa huo, Ali Haidar, alisema kuwa, ipo haja kwa maafisa upelelezi kupatiwa mafunzo hayo na hasa kwa kesi za udhalilishaji.
Alisema, anaamini mafunzo hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa watuhumiwa kutiwa hatiani kwani ushahidi hautokuwa na mapungufu ambayo wakati mwengine husababisha mtuhumiwa kuachiwa huru.
“Wakati mwengine mtuhumiwa anaachiwa huru kutokana na muda tu ulioandikwa kwenye hati ya mashitaka kutokuwa sawa na ule aliosema aliyebakwa’, alieleza.
Alisema, kutokana kuwepo kasoro hizo ndogo ndogo ofisi yao imeona vyema kuwa na mafunzo yatayoyabainisha dosari ziliopo na kuweka njia nzuri ya kuepukana nayo.
Alsema, kwa hivi sasa kazi ya uchunguzi inafanywa kwa haraka, kati ya siku moja hadi mbili, lakini vizuri ifanyike juhudi ili huo upelelezi ufanyike kwa uweledi zaidi.
Mafunzo hayo pia yatalenga juu ya makosa maalumu ya udhalilishaji, ili wapelelezi waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuepuka malalamiko katika jamii.
Akizungumzia mahakama ya udhalilishaji iliyoanzishwa karibuni alisema, anatarajia itaisaidia kuendelea kuwepo ushirikiano mzuri kati ya ofisi yao na mahakama, ili kesi za udhalilishajo zishugulikiwe vizuri kisheria.
Alisema, Pemba imeshatenga wanasheria wanane kuendesha kesi za udhalilishaji na hii itasaidia kesi hizo kushughulikiwa haraka na kupatiwa uamuzi mapema.
Mwanasheria Dhamana huyo alisema, changamoto zinazoweza kuikabili mahakama maalumu, ni namna ya kuwalinda mashahidi hasa waliofanyiwa udhalishaji wakati wa kuendesha kesi na pia ni nauli au posho kwa mashahidi wanaofika mahakamani.
Hata hivyo, pamoja na changamoto hizo, alisema inafurahisha kuona ipo mipango kila sekta, ili kuiwezesha mahakama hii kufanya kazi yake vizuri.
Mratibu wa Jumuiya ya Tumaini Jipya (TUJIPE) iliyopo Chake Chake, Tatu Abdalla Mselem, alisema ipo haja kwa Serikali kuangalia namna ya kuzuia matumizi mabaya ya mitandao, kuzuia kuuzwa kwa vilainishi vinavyotumika kufanya mambo machafu na uingizaji wa dawa za kulevya.
Haya yote yanachangia ongezeko la vya udhalilishaji na hasa wa watoto. Alisema, tatizo jengine ni ya jamii kugubikwa na rushwa muhali, mashirikiano madogo katika baaadhi ya sehemu katika kumaliza udhalilishaji na jamii kukosa uelewa wa kutosha kuhusu madhara ya kesi hizo.
“Mwaka huu tumejipanga kuelimisha jamii madhara ya ushalilishaji na namna ya kuripoti maovu haya, tutapita shehia kwa shehia”, aliongeza.
Mwaka jana ofisi ya TUJIPE ilipokea malalamiko ya matukio 10 ya udhalilishaji. Mratibu wa Dwati la Wanawake na Watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba, Fakih Mohamed Yussuf, alisema wana programu maalumu ya kuelimisha jamii.
Kazi hii inafanywa kwa kushirikiana na wadau wengine, kikiwemo Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba.
Tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, atoe agizo dhidi ya udhalilishaji wamepokea kesi 38 za udhalilishaji.
“Kati yao, kesi 11 zipo mahakamani, 21 zinaendelea na upelelezi na moja imefungwa kutokana na mashahidi kukataa kutoa ushirikiano”, alisema mratibu huyo.
Kuanzia Januari 2019 hadi Disemba 2020 Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limepokea jumla ya kesi 281 za udhalilishaji.