Salum Vuai
INATISHA SANA! Inasikitisha kusikia ubadhirifu wa kutisha wa fedha na mali za umma uliofanywa/unaofanywa na baadhi ya watendaji wakuu wa serikali zote mbili nchini Tanzania.
Viongozi na watendaji hao ni wale wanaoangalia zaidi maslahi binafsi kuliko ya wananchi wanaolipa kodi na ada mbalimbali kwa kile wanachoaminishwa zitarudi kwao wenyewe kwa kuletewa maendeleo.
Wanapokuwa kwenye viriri vya mikutano ya kisiasa au warsha na makongamano, hujivisha joho la UZALENDO, kumaanisha kwamba wao ni wapenda na wajenga nchi waliotukuka.
Kauli za kuwasisitiza watu wawe wazalendo kwa nchi yao, ndio wimbo mashuhuri unaoghaniwa na vinywa vyao huku wakiweka vibwagizo vya kuwasema vibaya wale wanaowaona hawazitakii mema Tanzania na Zanzibar pengine kwa mitazamo na maoni yao juu ya namna bora ya kuendesha nchi.
Wapo waliofikwa na vituko na vitakuro vya kupakwa matope sambamba na kutengwa wakipachikwa jina la SI WENZETU kwa kutafautiana mawazo tu na ‘WAZALENDO WA KWELI’.
Wanaoyatenda hayo wanasahau kwamba mtu anaweza kuwadanganya baadhi ya watu kwa wakati fulani, lakini hawezi kuwadanganya watu wote wakati wote. Na leo tunayaona mambo ya ndovu kumla mwanawe.
La kusikitisha zaidi watu wanashindwa kuviheshimu hata vitabu vya dini ambavyo huvishika wakati wanapoapishwa kwa ajili ya kutumia nyadhifa wanazokabidhiwa.
Hata jina la Mwenyezi Mungu ambaye humtaja mwisho wa viapo vyao kwa kalima za ‘EWE MWENYEZI MUNGU NAOMBA UNISAIDIE’, husahaulika mara tu wanapokalia viti vya enzi.
Kiona mbali haina haja kurudia madudu yaliyowekwa hadharani katika ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi karibuni kwani karibu sote tumeyasikia.
Aidha yale yaliyojiri ndani ya vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadhi ya taasisi na mashirika ya umma kuhusu matumizi mabaya ya fedha na wizi unaofanywa kwa kupandikiza wafanyakazi hewa, ni mambo yanayowasuta wateule wanaoapa kwa kushika vitabu vya dini wakiahdi kuwa waadilifu na waaminifu.
Huenda ikawa hilo ni gao tu kiganjani, bali yapo mengi ambayo bado yamefichika na yanahitaji kufanyiwa kazi ili kusafisha nyumba.
Ni kichekesho kwamba miongoni mwa wanaojihusisha na tabia hiyo ya kuibomoa nchi ni Ma-Al haj waliotekeleza ibada ya Hijja, lakini wakirudi husahau kuwa huko walikwenda kufuta madhambi yao ya nyuma kwa lengo la kutorudia tena.
Je, haya yanayotendwa ndio uzalendo wanaojigamba wenzetu kuwa nao kulinganisha na wengine wasiopendezwa na vitendo vya hujuma dhidi ya hazina ya serikali?
Kwa sababu hizi na nyengine, Kiona mbali inashauri huko twendako serikali ifikirie kuacha utaratibu wa kuwaapisha viongozi wateule kwa kutumia Kuran na Biblia, kwani ni dhahiri baadhi ya watu sio wasafi wa kuvishika na kuviheshimu vitabu hivyo.
Iwapo ni lazima mtu anapoapishwa ashike kitabu, basi ama iwe katiba za nchi yetu au kuandiliwe maandishi maalum lakini sio tena kulikejeli jina la Mwenyezi Mungu kwa kumuomba awasaidie huku wenyewe wakiwa na nia ovu nyoyoni mwao.
Ifahamike kwamba Mungu hachezewi na haishangazi haya tunayoyashuhudia sasa ikawa ni matokeo ya ghadhabu zake kwa wale wanaoapa lakini baadae wakageuka mchwa wanaoimong’onyoa ndani kwa ndani nyumba tunayoijenga.