Na Khadija Kombo
Wafanyabiashara wanawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanafanya biashara zao kwa kuzingatia hali za wateja wao hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Asema hayo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Salama Mbarouk Khatib wakati alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara katika ukumbi wa Jamhuri Wete mara baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea maeneo mbali mbali ya Biashara Wilayani humo.
Amesema baadhi ya wafanyabiashara , wanafanya biashara zao kwa kutarajia kupata faida kubwa zaidi bila ya kufikiria wateja wao na hali zao za maisha.
“kuna wateja wa aina mbali mbali wengine ni masikini,wengine fukara,wengine ni watu wazima wasio jiweza lazima mfanyabiashara azingatie na mahitaji ya hao wote,huu ni mwezi Mtukufu wa kuchuma thawabu na sio mali” alisema Mh. Salama.
Pia Mh. Salama amewataka wafanyabiashara hao kuwa na tahadhari zaidi wanapo kwenda watoto kununua bidhaa kuwapa mahitaji yao bila ya usumbufu huku wakihakikisha wanawapatia bidhaa zilizo bora na sio kuwapa vitu visivyo stahiki.
“kuna wafanyabiashara wengine wanapokwenda watoto wanawapa bidhaa ambazo haziridhishi kwa kuona kuwa wao hawahui kuchagua lakini wakumbuke kuwa watoto hao wametumwa na watu wazima ambao hawataridhika kwa kupokea bidhaa hizo.”alisema Mh. Salama
Naye Mkuu wa Wilaya ya Wete bibi Mgeni Yahya Khatib amewataka wafanya biashara kuangalia sana bidhaa zao ili wasije wakauza bidhaa zilizopitiwa na muda kwa kuepusha madhara kwa watumiaji .
“kuna baadhi ya wafanya biashara wakiona bidhaa zao zimepitwa na wakati huzibadilisha vifungashio na kuendelea kuuza jambo ambalo ki biashara sio sahihi” alisema mkuu wa Wilaya huyo.
Kwa upande wao wafanyabiashara wameomba kuondoshwa mdorongo wa tozo ili kuepuka ongezeko la bei za bidhaa na kupelekea kusababisha hali ngumu ya maisha ndani ya jamii.
“tozo zimekuwa nyingi mbali ya TRA,ZRB,na Bandari lakini kuna tozo nyengine zisizopungua sita zikiwemo halmashauri,Baraza lamji na kilimo.” Walisema wafanyabiashara hao.