Tuesday, November 26

Mizozo inayozihusisha China,Urusi ,Iran na Korea kaskazini inatishia amani duniani

Maelezo ya picha, Vikosi vya Urusi vimekuwa vikifanya mazoezi katika eneo la Crimea

Uliwemgu umekuwa na muda mrefu wa utulivu isipokuwa mizozo ya vita katika mataifa machache vilivyohusisha nchi katika mabara tofauti miaka ya hapo nyuma.

Tangu kukamilika kwa vita vya pili vya dunia mwaka wa 1945 hapajawahi kuwa na vita vikubwa vilivyohusisha nchi nyingi kote duniani kuweza kutajwa kama vita vya tatu.

Mzozo wa Kosovo miaka ya 90 na mashambulizi ya baadaye ya Marekani dhidi ya mataifa mbali mbali huko mashariki ya kati iliweza kufika tamati baada ya nchi husika kujipatia uhuru ama Viongozi waliokuwa wakipigwa vita kuondolewa madarakani hususan katika mizozo ya mashariki ya kati.

Hata hivyo kuna uhasama ama migogoro baina ya nchi mbali mbali ambayo wakati mwingine huonekana kutokota na kufika kiwango cha kutishia usalama na amani ya ulimwengu mzima.

Baadhi ya mizozo hiyo imekuwa ikiendelea kwamiaka kadhaa ilahli mingine ina chimbuko la tofauti za kihistoria na kisiasa . Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa pia zimeshindwa kupata suluhisho kwa migogoro hiyo.

Urusi na Ukraine

Kabla ya kuporomoka kwa muungano wa Soviet ya miaka ya 90 Ukraine ilikuwa sehemu ya muungano huo lakini sasa imejipata ikilumbana na Urusi ambayo ndio nchi iliyosalia katika uliokuwa muungano wa Soviet uliokuwa na ushawishi mkubwa duniani na kupambana na Marekani kama mojawapo ya nchi zenye nguvu zaidi duniani.

Rais Zelensky (mbele kushoto) alitembelea vikosi vya Ukrain katika eneo linalozozaniwa Aprili 8-9

CHANZO CHA PICHA,EPA

Maelezo ya picha,Rais Zelensky (mbele kushoto) alitembelea vikosi vya Ukrain katika eneo linalozozaniwa Aprili 8-9

Urusi imekuwa na malengo ya kuchukua kwa njia moja au nyingine baadhi ya sehemu zilizokuwa katika muungano wa Soviet na mwaka wa 2014 ilifaulu kuichukua Crimea kutoka kwa Ukraine.

Malumbano katika mpaka baina ya nchi hizo yameendelea tangu hapo na kwa sasa Urusi imewahami wapiganaji katika eneo la Donbas ambao wanataka kujitenga kutoka kwa Ukraine na kuwa nchi huru.

Je Urusi inajiandaa kuvamia Ukraine?

Kumekuwa na ripoti za wanajeshi wengi wa Urusi kujikusanya katika mpaka wake na Ukraine na nyingi ya ripoti hizo zimekuwa zikitolewa katika mitandao ya kijamii kama vile twitter .

Kremlin haijatoa maelezo juu ya vitengo vinavyohusika. Msemaji wa Rais Vladimir Putin, Dmitry Peskov alisema kuhamisha wanajeshi katika eneo la Urusi ni “jambo la ndani” ambalo halipaswi kumhusu mtu yeyote.

Baadhi ya wanajeshi, pamoja na vitengo huko Crimea, wamekuwa kwenye mazoezi. Lakini Bwana Peskov pia aliituhumu Ukraine kwa “uchochezi”.

Vyanzo vya ujasusi vya Ukraine viliambia BBC kwamba vikosi vya ziada kutoka Urusi ni hadi wanajeshi 14,000. Kwa jumla, kulingana na ofisi ya rais wa Ukraine, Urusi sasa ina wanajeshi 40,000 kwenye mpaka wa mashariki na karibu 40,000 huko Crimea.

Je hili linaweza kuwa ni uvamizi? Inawezekana, lakini wachambuzi wanasema uvamizi mkubwa hauwezekani. Kujipenyeza itakuwa njia iliyojaribiwa na kuaminika zaidi inayoweza kutumiwa na Urusi. Vikosi maalum vya Urusi bila sare rasmi – vilichukua Crimea mnamo 201 kwa mtindo huo.

A Ukrainian soldier mans the machine-gun of a vessel on the Azov Sea on November 28, 2018 in Mariupol, Ukraine

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Wanajeshi wa Ukraine kwenye bandari ya Mariupol bahari ya Azov

Kwa nini Urusi iko vitani na Ukraine?

Tangu kuanguka kwa ukomunisti mnamo 1991, wanajeshi wa Urusi waliingilia mizozo katika maeneo kadhaa ya yaliyokuwa sehemu ya Muungano Kisovieti, haswa huko Chechnya na maeneo mengine ya Caucasus.

Kulikuwa na mapigano makubwa mnamo 2014, kabla ya mapigano kusitishwa mnamo 2015. Kumekuwa na mabadilishano ya wafungwa tangu wakati huo.

Zaidi ya watu 13,000 wamekufa katika mzozo huo. Ukraine inasema 26 ya wanajeshi wake wamekufa huko Donbas hadi sasa mwaka huu, ikilinganishwa na 50 katika mwaka wa 2020. Wanaotaka kujitenga katika eneo hilo wanasema zaidi ya watu wao 20 wamekufa mwaka huu

Mkataba wa amani wa Minsk uliokubaliwa mnamo 2015 bado haujatimizwa. Kwa mfano, bado hakuna mipango ya uchaguzi wa kusimamia kwa njia huru katika maeneo yanayotaka kujitenga

Wengine wanakisi kuwa rais wa Urusi Vladmir Putin pia anataka kumjaribu Rais wa Marekani Joe Biden, ambaye amechukua msimamo mkali juu ya Urusi kuliko mtangulizi wake, Donald Trump.

Picha ya maktaba ikionesha Meli ya kijeshi ya China

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

China na Taiwan

Taiwan maajuzi imelalamikia kuhusu hatua ya Uchina kupepetusha ndege zake nyingi za kivita katika anga yake.

Wizara ya Ulinzi ya Taiwan imesema hadi ndege 25 za Uchina na zilizo na uwezo wa kinyuklia zimepaa katika anga yake.

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mzozo wa muda mrefu kwani Uchina inataka kuiunganisha Taiwan na China bara ili kuwa nchi moja lakini kwa muda mrefu nchi hizo zimekuwa zikijitawala kivyake.

Beijing imeendelea kushikilia kwamba Tawain ni mkoa wake uliojitenga.Taiwan hata hivyo inajichukulia kama nchi huru.

Tukio hilo la hivi karibuni lilitokea siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kusema kuwa Marekani ina wasiwasi juu ya “hatua zinazoendelea kuwa za uchokozi” za China dhidi ya Taiwan.

Kisiwa hicho kina katiba yake, jeshi, na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.

China haijafutilia mbali uwezekano wa matumizi ya nguvu kufanikisha kuungana na Taiwan.

Picha ya Satellite inayoonesha lango la bahari la Taiwan

CHANZO CHA PICHA,GALLO IMAGES

China Taiwan: Unayofaa kujua

  • Uchina na Taiwan wamekuwa na serikali tofauti tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya China mnamo 1949. Beijing imejaribu kwa muda mrefu kupunguza shughuli za kimataifa za Taiwan na zote mbili zimeng’ang’ania kupata ushawishi katika eneo la Pasifiki.
  • Mvutano umeongezeka katika miaka ya hivi karibuni na Beijing haijaondoa uwezekano matumizi ya nguvu kukirudisha kisiwa hicho
  • Ingawa Taiwan inatambuliwa rasmi na mataifa machache tu, serikali yake iliyochaguliwa kidemokrasia ina uhusiano mkubwa wa kibiashara na usiyo rasmi na nchi nyingi
  • Kama mataifa mengi,Marekani haina uhusiano wowote wa kidiplomasia na Taiwan, lakini sheria ya Marekani inahitaji iipe kisiwa hicho njia za kujilinda.

Korea Kaskazini na Korea Kusini

Tangu mgawanyiko wao baada ya Vita vya pili vya dunia , Korea Kaskazini na Korea Kusini zimekuwa na mgongano mkubwa sana .

Japani ilitawala Korea kutoka 1910 hadi Wajapani walipojisalimisha baada ya vita vya pili vya dunia mwaka wa 1945.

Picha ya DMZ

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,Haijulikani ni nini haswa kilichosababisha vurumai hiyo

Baadaye, askari wa Soviet walichukua eneo hilo kaskazini na wanajeshi wa Marekani wakachukua uthibiti wa eneo la kusini.

Mvutano kati ya kaskazini na kusini ulilenga tofauti kati ya demokrasia na ukomunisti.

Korea kusini hata hivyo ilijipata katik mafanikio ya kiviwanda na kufaulu kujipa utajiri mkubwa wa kiuchumi huku Korea kaskazini ikitengwa chini ya familia iliyotawala Korea kaskazini ya Kim.

Tofauti hizo zilizidishwa na hatua ya Kaskazini kuanzisha mpango wa kujipa nguvu za zana za Kinyuklia na kujipata ikitengwa na mataifa mengi yaliyoegemea upande wa Marekani na nchi za Magharibi.

Hadi sasa kuna wanajeshi wa Marekani na mataifa mengine katika mpaka wa nchi hizo mbili kwani licha ya kusistishwa kwa vita na kuafikia mkataba wa kumaliza uhasama bado kuna visa vya mashambulizi vinavyoendelea.

Vikosi vya marekani

Iran na Marekani

Uhusiano wa Marekani na Iran haukuwa mbaya kabla ya mwaka wa 1953.

Lakini matukio yaliyofuata baada ya hapo yamezifanya nchi hizo kujipata katika pande mbili hasimu kw amuda mrefu huku mpango wa Nyuklia wa Iran ukiwa ndio kichocheo kikubwa cha kuvuriga kabisa uwezo wa nchi hizo kuhusiana vizuri na kwa njia ya kidiplomasia. Matukio hayo ni kama ifuatavyo:

1953: Kupinduliwa kwa Mossadeq

Mashirika ya ujasusi ya Marekani na Uingereza yalipanga mapinduzi ya kumuondoa Waziri Mkuu wa Iran aliyechaguliwa kidemokrasia, Mohammad Mossadeq. Kiongozi huyo wa alikuwa ametaka kutaifisha mashirika ya mafuta ya Iran.

1979: Mapinduzi ya Iran

Shah wa Iran aliyeungwa mkono na Marekani, Mohammed Reza Pahlevi, alilazimika kuondoka nchini mnamo Januari 16 kufuatia miezi kadhaa ya maandamano na mgomo dhidi ya utawala wake na wapinzani .

Wiki mbili baadaye, kiongozi wa dini la Kiislamu Ayatollah Khomeini anarudi kutoka uhamishoni. Kufuatia kura ya maoni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatangazwa tarehe 1 Aprili.

1979-81: Mgogoro wa mateka katika Ubalozi wa Marekani

Ubalozi wa Marekani huko Tehran ulivamiwa na waandamanaji mnamo Novemba 1979 na mateka wa Marekani kushikiliwa kwa siku 444.

Mateka 52 wa mwisho waliachiliwa huru mnamo Januari 1981, siku ya kuapishwa kwa Rais wa Marekani Ronald Reagan.

Wamarekani wengine sita waliotoroka ubalozi wanatoroshwa kwa Iran na timu inayojifanya kuwa watengenezaji wa filamu, katika tukio lililoigizwa katika filamu iliyoshinda tuzo ya Oscar,Argo ya mwaka wa 2012.

1988: Ndege ya abiria ya Iran yadunguliwa

Meli ya kivita ya Amerika USS Vincennes yaidungua ndege ya mnamo Julai 3, na kuua watu wote 290 waliokuwamo ndani. Marekani inasema Airbus A300 ilidhaniwa kuwa ndege ya kivita.

Waathiriwa wengi ni mahujaji wa Irani wakielekea Makka.

2000: Hofu ya mpango wa nyuklia na vikwazo

Mnamo 2002 kikundi cha upinzaji cha Irani kinafichua kwamba Iran inaendeleza vifaa vya nyuklia ikiwa ni pamoja na kiwanda cha kuimarisha uranium

Marekani inaishutumu Iran kwa mpango wa siri wa silaha za nyuklia, madai ambayo Iran inakataa. Lakini vikwazo vilivyowekwa na UN, Marekani na EU dhidi ya serikali ya rais Mahmoud Ahmadinejad vinasababisha sarafu ya Iran kupoteza theluthi mbili ya thamani yake katika miaka miwili.

2013-2016: Uhusiano wa karibu na makubaliano ya mpango wa Nyuklia

Mnamo Septemba 2013, mwezi mmoja baada ya rais mpya wa Iran Hassan Rouhani kushika madaraka, yeye na Rais wa Marekani Barack Obama wanazungumza kwa njia ya simu – mazungumzo ya kwanza ya kiwango cha juu zaidi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 30.

Halafu mnamo 2015, baada ya shughuli nyingi za kidiplomasia, Iran inakubali makubaliano ya muda mrefu juu ya mpango wake wa nyuklia na kundi la mataifa yenye nguvu zaidi duniani zinazojulikana kama P5 + 1 – Marekani, Uingereza, Ufaransa, Uchina, Urusi na Ujerumani.

Chini ya makubaliano hayo, Iran inakubali kupunguza shughuli zake za nyuklia na kuruhusu wakaguzi wa kimataifa ili kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

2019: Taharuki kwenye ghuba

Mnamo Mei 2018, Rais wa Marekani Donald Trump aliachana na makubaliano ya nyuklia, kabla ya kurejesha vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran na kutishia kufanya vivyo hivyo kwa nchi na kampuni zinazoendelea kununua mafuta yake.

Uchumi wa Iran ulivurugika na kuathiri hali ya maisha nchini humo.

Uhusiano kati ya Marekani na Iran unazidi kuwa mbaya mnamo Mei 2019, wakati Marekani inapoimarisha vikwazo vinavyolenga usafirishaji wa mafuta ya Iran.

Kwa kujibu, Iran inaanza kampeni ya kukabiliana na shinikizo.

Mnamo Mei na Juni 2019, milipuko ulikumba meli sita za mafuta katika Ghuba ya Oman, na Marekani ikaishtumu Iran.

Mnamo Juni 20, vikosi vya Irani viliangusha droni ya Marekani juu ya anga ya Mlango wa Hormuz. Marekani inasema droni hiyo ilikuwa juu ya maji ya kimataifa, lakini Iran inasema ilikuwa katika anga yake

2020: Mauaji ya Qasem Soleimani

Mnamo 3 Januari 2020, kamanda mkuu wa jeshi la Iran, Jenerali Qasem Soleimani, anauawa katika shambulizi la droni ya Marekani nchini Iraq.

Iran yaapa “kulipiza kisasi vikali” kifo chake na inajiondoa kutoka kwa makubaliano ya nyuklia ya 2015.

Hbari hii kwa hisani ya BBC-