Tuesday, November 26

Watu wawili wapelekwa chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 35 kwa makosa ya udhalilishaji.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA.

 

MAHAKAMA ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, imewapeleka chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 35 watu wawili baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya udhalilishaji.

 

Katika mahakama hiyo mtuhumiwa wa kwanza kutiwa hatiani ni Mahmoud Hafidh Khamis mwenye miaka 21 mkaazi wa Uondwe shehia ya Shumba Vyamboni ambaye ametiwa hatiani kwa makosa mawili ya kuwaigilia kinyume na maumbile watoto wawili wa kike, mmoja akiwa na umri wa miaka saba (7) na mwengine miaka mitano (5).

 

Awali kijana huyo alikuwa anakabiliwa na makosa manne, ikiwemo mawili ya kubaka na mawili ya kuingilia watoto wawili kinyume na maumbile.

 

Akisoma hukumu, hakimu wa mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba Abdalla Yahya Shamhun alimuachia huru mtuhumiwa kwa makosa mawili ya kubaka baada ya maelezo ya upande mashahidi kupingana na maelezo ya waathirika.

 

“Maelezo ya mashahidi yamepingana na maelezo ya waathirika, kwamba upande wa mashahidi walidai watoto hao walibakwa, lakini waathirika wenyewe walikana kubakwa, bali walidai waliingiliwa kinyume na maumbile”alisema.

 

“Hivyo kutokana na maelezo hayo kutofautiana, Mahakama imemuachia huru mtuhumiwa kutokana na makosa mawili ya kubaka, ambapo atatiwa hatiani kwa makosa ya kuwaingilia watoto hawa kinyume na maumbile”, alifahamisha.

 

Hata hivyo, mahakama hiyo imemwamuru kutumikia chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 14, kwa kosa la kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa kwanza na kosa la kumuingilia mtoto wa pili nalo atatumikia chuo cha mafunzo kwa kipindi cha miaka 14.

 

“Mahakama inamtia hatia mtuhumiwa kwa makosa mawili ya kuwaingilia kinyume na maumbile watoto hao, ambapo kosa la kwanza atatumikia chuo cha mafunzo miaka 14, halikadhalika na kosa la mtoto wa pili, hivyo adhabu hizo zitaenda sambamba”, alifahamisha.

 

Aidha katika mahakama hiyo hiyo, mshitakiwa Seif Said Seif amepelekwa chuo cha Mafunzo kwa kipindi cha Miaka 7, baada ya kupatikana na kosa la kumbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 10.

 

Kesi hiyo namba 36/2018 ilitokea tarehe isiyojulikana  mwezi wa 10/2007, ambapo akiwa chumbani kwake , Seif Said Seif  alimbaka mtoto huyo na kumsababishia maumivu sehemu zake za siri.

 

“Mahakama imekutia hatiani  baada ya kukubaliana bila ya wingu la shaka juu ya ushahidi uliotolewa na upande  wa mashitaka, hivyo utatumikia chuo cha mafunzo miaka saba pamoja na kulipa fidia kwa mwathirika ya shilingi millioni moja”, alisema.

 

Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib alipongeza wananchi waliokwenda kutoa ushahidi wa kesi hiyo na kuwataka kuendelea kutoa ushahidi wakati wanapohitajika.

 

Hivyo alisema Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia kwa masheha na kuwaomba wajitokeze kwenye mikutano hiyo na waipokee elimu inayotolewa na kuifanyiakazi.