Monday, November 25

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Azungumzia na Uongozi wa Kanisa la Wasabato Tanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi azungumza na Ujumbe wa Uongozi wa Kanisa la Wasabato Tanzania ukiongozwa na Askofi Mark Walwa Malekana , walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Askofu Mkuu wa Kanisa la Wasabato Tanzania Askofu Mark Walwa Malekana alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi ameuhakikishia uongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikia nao kwani inatambua mchango wao katika kusaidia huduma za jamii hapa nchini.

 

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na uongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania ambao umefika kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kumpongeza Rais kwa kuchaguliwa katika Awamu hii ya Nane ukiongozwa na Askofu Mark Walwa Malekana.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba Serikali ya Mapindzi ya Zanzibar itaendeleza ushirikiano wake kwa Kanisa hilo kutyokana na kuthamini mchango wake mkubwa katika kutoa huduma za jamii hapa nchini.

Alisema kuwa kanisa hilo limeweza kuwajenga kiimani waumini wake katika kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu pamoja na sekta ya afya kwa Unguja na Pemba.

Alieleza kuwa juhudi za Kanisa hilo za kusaidia katika sekta ya afya na sekta ya elimu zitaendelea kuungwa mkono na Serikali anayoiongoza ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inazifanyia kazi changamoto zilizopo.

Alifahamisha kwamba Serikali itakuwa tayari katika kuhakikisha miradi inayoanzishwa na Kanisa hilo ikiwemo ile ya elimu na afya inafikia malengo yaliyokusudiwa katika kutoa huduma kwa jamii.

Aidha, alitoa pongeza kwa Kanisa hilo kwa kusaidia katika kuunga mkono juhudi za Serikali kwenye sekta ya elimu kwa kusaidia uimarishaji wa sekta hiyo katika Skuli ya Ali Khamis Camp iliyopo Pemba kwa kusaidia walimu wa Sayansi pamoja na vitabu.

Pia, alilipongeza Kanisa hilo kwa kusaidia uimarishaji wa sekta ya afya katika Zahanati yake iliyopo Meya katika eneo la Magomeni Jijini Zanzibar ambayo imekuwa ikitoa huduma za afya kwa kipindi kirefu.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliupongeza utayari wa Kanisa hilo wa kutaka kuanzisha Chuo cha Ufundi hatua ambayo itasaidia kuimarisha sekta ya elimu na ufundi hasa kwa vijana.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba kwa vile Zanzibar inahitaji kujenga uchumi madhubuti hivyo imani na utendaji sambamba na mashirikiano ya pamoja  yanahitajika ili kuweza kuijenga Zanzibar yenye maendeleo zaidi.

Nae Askofu Mark Malwa Malekana  ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kusini mwa Tanzaniaakiwa na ujumbe wake wa Maaskofu kutoka Zanzibar na Tanzania Bara,alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa ushindi mkubwa na wananchi wa Zanzibar.

Aidha, Askofu Malekana alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kasi kubwa ya kuiletea maendeleo Zanzibar aliyoanza nayo ikiwa ni pamoja na maono yake ya uchumi wa buluu huku akiahidi kwamba Kanisa lake litaendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kufikia malengo yake iliyojiwekea.

Askofu Malekana alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa likipata mashirikiano mazuri kutoka kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kusisitiza haja ya kuimarishwa zaidi.

Akitoa historia ya Kanisa hilo Askofu Malekana alisema kuwa kwa hapa Zanzibar Kanisa hilo lilianza rasmi mnamo mwaka 1986 ambapo kuanzishwa kwake kuliambatana na utoaji wa huduma za kiroho na za kijamii.

Alisema kuwa katika huduma za kijamii, Kanisa hilo lilianzisha huduma za utabibu kwa kuwa na vituo viwili vya afya Unguja na Pemba pamoja na kuanzisha skuli ya awali na Msingi huko Tomondo na kwa sasa limo katika hatua ya kuanzisha skuli ya Sekondari.

Alisema kuwa elimu inayotolewa na skuli zao inazingatia mitaala na miongozo yote inayotolewa na Wizara ya Elimu pamoja na kutoa elimu bila ya kujali tofauti za kidini au kikabila.

Kwa upande wa Pemba alisema kwamba Kanisa hilo lilitoa vitabu katika skuli ya Ali Khamis Camp vyenye thamani ya TZS milioni nne pamoja na kutuma walimu wawili wa masomo ya Sayansi ambao walikuwa wakihudumiwa na Kanisa kwa miaka mitano mfululizo hatua iliyopelekea kuongeza ufaulu katika skuli  hiyo.

Pamoja na hayo, kiongozi huyo aliitaja Zahanati iliyopo Meya eneo la Magomeni ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa jamii pamoja na kituo cha afya kilichopo Wawi-Pemba ambacho kinaendelea kutoa huduma nzuri.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar