NA ABDI SULEIMAN.
MKUU wa Wilaya ya Wete Mgeni Khatib Yahya, amewataka walimu wakuu wa skuli za Sekondari zilizomo ndani ya Wilaya hiyo, kuhakikisha wanatumia mbinu mbadala ili kuongeza ufaulu katika skuli zao zilizomo ndani ya Wilaya ya Wete.
Alisema katika matokeo ya mitihani ya kitaifa mwaka jana, Wilaya hiyo matokeo yake hayakuwa mazuri jambo lililoifanya wilaya ya micheweni kuwa juu yao.
Mkuu huyo wa Wilaya aliyaeleza hayo, katika taarifa yake iliyosomwa na Katibu wala wa Wilaya ya Wete Mkufu Faki Ali, wakati wa sherehe ya ugawaji wa zawadi kwa walimu bora wa Sekondari kupitia mradi wa ZISP.
Aidha Mkuu huyo alisema wakati umefika wa kuongeza juhudi za ufundishaji ili kuona wilaya ya wete inarudi katika hadhi yake kielimu.
Mkuu huyo wa Wilaya aliwashauri walimu waliopatiwa mafunzo kupitia mradi wa ZISP, kutumia ujuzi wao kushajihisha walimu wengine, kubadilika katika usomeshaji wao ili kufikia malengo yao.
“Hapa tumeelezwa kuwa tayari walimu 162 wilaya wete, wameshafundishwa kupitia mradi huo sasa kilichobakia tunahitaji kuona mabadiliko makubwa katika sekta hii ya elimu kwenye wilaya yetu”alisema.
Aliwapongeza walimu hao kwa kuwabadilisha wanafunzi, kwani wanafunzi wengi wanapenda masomo ya ati na sio sayansi, lakini ZISP imesweza kuwabadilisha na kuingia katika masomo ya sayansi.
Hata hivyo aliwataka wanafunzi kujikita katika masomo ya sayansi, kwani Tanzania imeingia katika uchumio wa kati hivyo uchumi unahitaji wataalamu zaidi kutoka katika fani za sayansi.
Kwa upande wake afisa Elimu ya Sekondari Mkoa wa Kaskazini Pemba Khamis Said Hamad, alisema skuli Hubs ni vituo vya majaribio ya sayansi na vina kila kitu ambavyo hutumika katika masuala ya sayansi.
Aidha aliwataka walimu kuhakikisha waongeza juhudi zaidi katika ufundishaji wao, kwa kutafuta mbinu mabadala ili kuona mafanikio yanapatikana kupitia mradi huo.
Akisoma katika hafla hiyo Badiura Suleiman Abdalla, alisema lengo la mradi wa ZISPI ni kuongeza ufauli wa wanafunzi wa skuli za sekondari na msingi Zanzibar hasa katika masomo ya sayansi, Kiengereza na Hesabati.
Aliwataka wanafunzi na walimu kuvitumia vituo hivyo ambavyo vipo jirani, katika kujifunza ikiwa ni matunda adhimu yaliyotokana na rais Mstaafu aliyemaliza muda wake Alhaj Dkt. Ali Mohamed Shein.
Mwalim Asha Bakar aliyeibuka mshindi kwa upande wa Lugha kutoka skuli ya Chasasa, alisema moja ya mbinu alizokuwa akizitumia kufundisha wanafunzi ni kutumia masomo ya ziara, pamoja na kushirikiana na walimu wenzake katika siku ambazo hahudhurii darasani.
Mwalim Nassor Salum Nassor kutoka skuli ya Pandani somo la Chemistry, aliwataka wanafunzi kutokuona masomo ya sayansi magumu, kwani hata yeye alisoma fani ya lugha lakini sasa ameingia katika fani ya sayansi.