
Na.Mwandishi Wetu Pemba.
WAZIRI wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mhe.Lela Mohammed Mussa amewataka vijana kuimarisha utamaduni wa kupanda miti hasa sehemu za historia ili kizazi cha baadae kije kurithi matunda sambamba na kuongeza vivutio vya utalii Kisiwani Pemba.
Akizungumza baada ya kushiriki zoezi la kupanda miti huko Maziwangombe wilaya ya Micheweni ikiwa ni madhimisho ya siku ya urithi duniani Mhe Lela amesema vijana kupitia siku hiyo wanapaswa kuendeleza kupanda miti na kuthamini maeneo yenye historia ili kuweza kuibua vivutio vingi vya Utalii Kisiwani Pemba katika kusaidia kuondoa changamoto ya ajira kwa Vijana.
Mapema Afsa Mdhamini wa Wizara ya Utalii na mambo ya kale Pemba Bi.Zuhura Mgeni Othman amesema wizara itaendelea kushirikiana na vijana ili kuifanya Pemba kuwa Kisiwa cha kijani huku Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mhe.Mohamed Mussa Mkobani ameahidi kuwachukulia hatua watakaohusika na kuharibu miti iliyopandwa
Kwa upande wake Ndg. Haji Seif Yusuph Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uhifadhi na Urithi Pemba amesema wanaendelea kushajihsha jamii kupanda miti katika maeneo yanayowazunguka pamoja na kuziimarisha sehemu za utalii ili ziendelea kuchangia kipato cha Taifa.