NA MWANDISHI WETU.
Kazi ni kipimo cha utu .Bila shughuli ya kukupatia kipato maisha yanaweza kuwa magumu; iwe ni shughuli rasmi ya ajira ama iwe ni kazi yoyote ya kuongeza kipato . Fedha ni ustawi wa jamii ambayo inawezesha watu kujikimu kimaisha ; iwe ni fedha ya ajira rasmi ama ya kujiajiri
Tatizo kubwa linaloikabili jamii yetu ni kukosekana kwa mifumo inayowawezesha vijana kuajiriwa ama kujiajiri . Wakati mwengine si kukosekana tu kwa mifumo, bali ni kuwa na mifumo ambayo haiwawezeshi vijana kupata fursa . Kwa mfano vijana wengi wanamaliza elimu ya juu lakini kwa waliowengi haiwawezeshi kuwa na fikra tunduizi za kupata fursa za kuajiriwa ama kujiajiri wenyewe
Hebu na tuanze na mfumo wetu wa elimu.Kwa kiwango kikubwa cha elimu ambayo wanafundishwa vijana wetu, aidha ni elimu ya kukariri ama si elimu inayowawezesha kuwa na mawazo ya uzalishaji au kuanzisha vitu vya ubunifu . Tatizo kubwa hapa ni kwamba tunan’gania mitaala ile ile ambayo ilitengenezwa kuwapa watoto fikra za miaka sitini iliyopita ndio ile ile wanayopewa kwenye karne hii ya sayansi na technologia. Kamwe hatuangalii fursa na mahitaji ya dunia ya sasa na tukaingiza kwenye mitaala yetu kuleta mabadiliko . Si jambo la kushangaza mtaala wa phisikia ukawakaririsha watoto jinsi ya jua na mwezi linavyopatwa kama vile vijana haha watapata fursa ya kufanya kazi za kituo cha angani cha NASA cha wamarekani . Ni jambo la kushangaza . Bado kuna wa masomo yale yale ya fikra za zamani.Mzigo tu wa kuwabebesha madaftari mengi yenye athari ndogo kwa maisha ya baadae .
Ipo haja ya elimu yetu kuangalia fursa na rasilimali tulizonazo na kuanzisha mitaala inayoakisi fursa hizo . Zanzibar ni ya bahari , ni ya utalii na uzalishaji wa viungo vya kila aina . Jee mitaala yetu imejikita vipi kuwafundisha vijana rasilimali hii tuliyonayo . Nitaanza kwa kutoa mifano .
Serikali ya awamu ya nane imelipigia chapuo suala la uchumi wa buluu- Blue economy . Juhudi zimekwenda mbali la kuanzisha Wizara maalum inayoshughulikia uchumi wa buluu. Pengine dhana hii imechukuliwa vibaya kwa ufahamu wa wananchi kama ni utani . Hali ngumu iliyopo ya wananchi ndio ni utani na mzaha wa kuingia kwenye uchumi wa buluu. Ashaakum , pamoja na utani huu zipo fursa nyingi sana za kuitumia bahari kama ni rasilimali mujarab wa kubadilisha maisha ya Wazanzibar kwa kuchochea uwekezaji na kuzalisha ajira na mapato makubwa ya Serikali .
Lakini jee tumewekeza kwenye rasilimali watu juu ya ujuzi wa kutambua fursa ya Zanzibar na uchumi huu wa buluu? Nadhani tulichelewa kidogo. Kama tungalikua makini mitaala yetu ingeakisi kuwafunza vijana ni nini uchumi wa buluu pamoja na kuzichimbua fursa zilizomo katika uchumi huu . Tungalianza na mazao ya bahari. Kuwafunza vijana uvuvi bora wa samaki, tafiti za uvuvi,usarifu wa mazao ya bahari pamoja na ujasiriamali unaotokana na bahari kama vile uanzishwaji wa viwanda vya samaki , mwani na majongoo . Tungaliwafunza elimu ya sayansi ya bahari – marine science , jinsi ya kutunza mazingira endelevu ya bahari – marine ecosystem na mengine. Katika kuyatafakari haya ,tungaliangalia pia uwezeshaji na uwekezaji wa baharini. Kwa miaka mingi tunaangalia uwezekano wa uwepo wa mafuta ambayo kwa mujibu wa tafiti upo uwezekano mkubwa wa uwepo wa mafuta katika ukanda wa bahari. Jee elimu yetu imejikita vipi kuingiza mitaala hii ya kuwafunza vijana wetu usarifu wa uchimbaji wa mafuta pengine na gesi kama rasilimali inayoweza kuvikomboa visiwa hivi .
Bahari pia ni lango kuu la biashara . Jee tunawafunza vipi vijana wetu kuona fursa zinazotokana na uwekezaji wa baharini yaani inter -marine trade? Tulifapaswa kuingalia mitaala ya elimu ya juu hasa ile ya uchumi, ujasiriamali, manunuzi , mahusiano ya biashara za kimataifa na uwekezaji ukawafunza vijana elimu hii kwa kuangalia fursa hii adhimu .
Zanzibar ni ya utalii pia. Kwa asilimia kubwa ni utalii wa mwambao wa bahari unaowavutia wageni wengi .Pamoja na uwepo wa vivutie vingi vya utalii kama vile uwepo wa mji mkongwe , utalii wa utamaduni na viungo lakini kwa asilimia kubwa utalii unaowavutia wageni wengi ni utalii wa bahari – sea show tourist destination . Tuna bahati kubwa sana kwamba Zanzibar ni maarufu sana duniani na wala haihitaji nguvu nyingi za kuitangaza kwa utalii . Inasifika kwa fukwe nzuri za kuvutia na hoteli nzuri za mapumziko na uzamiaji wakuangalia dahari ya baharini – snorke diving . Lakini la kujiuliza ni kwa kiasi gani tumewafunza vijana wetu juu ya fursa hii ya utalii.Mitaala yetu ingalijikita kwenye mapishi – food cuisine , huduma za watalii – tourism hospitality , pamoja na uendeshaji wa biashara ya utalii – tourist related investment kama makampuni ya usafirishaji , uanzishwaji wa migahawa ya kisasa , maduka ya kitalii na mengine. Tunaweza pia kuanzisha stadi za kuwafunza vijana jinsi ya kuendesha michezo inayokuza utalii kama vile michezo ya baharini – water sports , matamasha ya kiutamaduni, mbio za kwenye fukwe – Zanzibar Beach rally . . Haya yangesaidia sana kuongeza wageni na kuzalisha kipato na ajira kwa vijana
Yapo malalamiko makubwa sana kuwa nafasi nyingi za ajira kwenye mahoteli zinahodhiwa na wageni hasa Wakenya na kutoka Tanzania bara . Ni kweli kwa sababu kwa mfano ,Kenya iliwekeza sana kwenye élimu ya utalii na wanavuna matunda ya vijana wengi kuwa na wajuzi wa kitaaluma wa kujikita kwenye stadi hizi za elimu ya utalii ; mapishi, uhudumu,utawala na sayansi ya jamii inayohitajika kwenye kusimamia sekta ya utalii
Visiwa vyetu ni maarufu sana duniani kwa uzalishaji wa viungo . Kwa mfano karafuu ni miongoni mwa zao linalochangia kwa kiasi kikubwa kuingiza fedha za kigeni . Jee mitaala yetu inamfundisha nani elimu ya biashara ya zao la karafuu .Nani wanafunzwa usarifu wa bidhaa zinazotokana na karafuu kwani miaka yote tumekua tukisafirisha bidhaa ghafi ya karafuu na si kile kinachotokana na karafuu ? Nani anafunzwa shuleni elimu ya upandaji wa mikarafuu kama vile utunzaji wa mbegu bora , uanzishwaji wa vitalu bora, mashamba darasa ya mikarafuu na jinsi ya kuuhudumia mkarafuu utoe mazao bora ? Hii ndio elimu ilipaswa kuwemo katika mitaala yetu lakini imebezwa
Wakati tunaendesha zao la karafuu kwa zaidi ya miaka mia mbili sasa, ni jambo la kushangaza sana kuona kwamba hatuna viwanda vya kutosha vya kuchakata bidhaa zinazotokana na karafuu badala yake inasafirishwa kama mali ghafi tu jambo ambalo linapunguza mnyororo wa thamani wa bidhaa . Ingawa bado mahitaji ya kusafirisha mali ghafi ya karafuu ni kubwa lakini bado uwezekano wa kusarifu zao hilo kwa kuangalia ubunifu wa bidhaa mbadala – by product – upo . Furia hii haijatumiwa vizuri na pengine haijaonekana haja ya kutumia fursa hii kama m’badala wa kuongeza uzalishaji na kukuza pato la wananchi na Taifa kwa jumla
Nchi kama China na Malaysia zimepata mafanikio makubwa ya maendeleo kwa kubadilisha mitaala. Kwa mfano kuna hadi elimu inayotolewa tu kwa baadhi ya majimbo kutokana na fursa zilizopo katika eneo husika _ Zonal Education . Kwa kwa mfano , kisiwa cha Pemba ni maarufu kwa uzalishaji wa mazao kama ndizi , mihogo , mabungo na maembe . Jee fursa hizi tumezitumia vipi kuwafunza vijana wetu kilimo cha mazao ya mkakati? Kwa mfano , mazao yanayozalishwa Pemba soko lake ni usafirishwaji tu hadi Unguja. Lakini jee tumewafunza vipi vijana wetu kuangalia uwekezaji wa kimkakati wa kilimo ili mazao yanayozalishwa Pemba yaongezeke pamoja na kutafuta fursa za usafirishwaji wa mazao hayo kwenye soko la nje?
Tulitegemea haya yawe ni msingi wa kuanzishwa mitaala mipya ya vyuo vikuu vyetu ;SUZA , Subeit na vyengine . Tulitegemea pia vyuo vyetu vya amali ambavyo vimeanzishwa vijikite kwenye elimu hii ambayo ndio mkombozi kwa vijana . Kuwapa fikra mpya , mawazo ya ubunifu kwa kuziangalia fursa na rasilimali zilizopo . Lakini bado tunasuasua katika hili . Tunategemea vyuo hivi visomeshe vijana wetu kwa weledi masomo ambayo yanaweza kuchochea ajira na uzalishaji kwa kuangalia rasilimali na fursa tulizonazo .
Kila mwaka kuna maelfu ya vijana wanaomaliza mashahada lakini wanabakia tu mtaani hakuna fursa za kujiajiri ama kuajiriwa . Wanakariri elimu ya nadharia ya uchumi huku mtaani hawajausoma uchumi kulingana na fursa na rasilimali walizonazo . Wanasoma tu masuala ya uongozi wa fedha, usimamizi wa rasilimali watu , ma shahada ya sheria na matakwimu bila ya hata kujua watapata fursa wapi za agira kwa kile ambacho wanakisoma . Hizi shahada za kawaida za uchumi wa jumla , sheria na manunuzi , pamoja na usimamizi wa rasilimali watu kwa kutumia nadharia na ukariri wa mitaala ile ile ya zamani , itaongeza tu mzigo wa wahitimu wasiokuwa na ajira na uwezo wa kujiajiri wenyewe. Kamwe Serikali haina uwezo wa kujiajiri vijana wote wanaomaliza shahada za vyuo vikuu. Kwa mfano , inakisiwa kwa mwaka tu kwa hapa Zanzibar kuna zaidi ya vijana elfu kumi na nane ambao wanamaliza shahada za kwanza .Hii ni idadi kubwa ya vijana ambao wanamaliza elimu ya juu na kubakia mtaani .Tuangalie fursa za kuwafunza taaluma zinazowasaidia kupata ajira
Nini cha kufanya walau tuwe na mwelekeo wa siku zijazo kuhusu mitaala na fursa zilizopo za kuongeza ajira na kipato cha nchi. Tunahitaki kuweka kipaumbele cha masomo ya mkakati . Masomo yatakayolenga kwenye uzalishaji wa rasilimali tulizonazo . Kuna haja ya kuweka kipaumbele kuwa na mifumo ya elimu na mitaala inayoongeza fursa na mawazo mapya ya uwezeshaji na uwekezaji . Uwepo muendelezo wa kuwapatia fursa vijana hawa kuandaa mawazo ya ubunifu na kuwaunganisha na mitaji , iwe ni kwa mikopo ya benki au iwe ni miradi ya mkakati inayosimiwa na Serikali
Ipo haja ya vyuo vikuu vyetu kuweka vipaumbele vya masomo ya kimkakati .Kubadilisha mitaala ya vyuo hivi au kuanzisha mitaala ya kimkamkati ya kuwafunza elimu ya manufaa na si ile tu élimu ya kukariri ya kusomesha kipenyo cha kutafuta x na y wakati huku mtaani si élimu inayohitajika
Tunatoa fikra hizi mbadala ambazo zinaweza kusaidia kuchochea mijadala katika jamii Tuwe na fikra mpya za kuangalia uwezekano wa kuwa na elimu yenye manufaa . Taifa la Tanzania na Zanzibar kwa jumla ni Taifa la Vijana , zaidi ya asilimia sitini ni tabaka tegemezi na si tabaka la uzalishaji . Tuna kiwango kikubwa cha vijana na watoto ambao ni tegemeo la kesho. Nguvu hii ni kubwa ya uzalishaji wa baadae ikiwa fursa hizi za élimu wanazopatiwa mashuleni na vyuo vikuu vinaweza kuchangia uwekezaji na uzalishaji kwa kutumia rasilimali zilizopo .
Kuwa na tabaka kubwa sana tegemezi ni mzigo mkubwa kwa Taifa . Tunahitaji kujenga uwezo wa vijana kiujuzi kwa kuwapa stadi na mawazo mbadala ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii
Mara nyingi tumekuwa tukihubiri amani . Lakini amani ya mwanzo huanzia na kuwa chochote mfukoni ambacho kinajenga jamii inayojiweza kiuchumi na kuchangia ustawi wa maisha ya kawaida ya mwananchi . Nchi zilizopiga hatua kubwa za maendeleo za hivi karibuni kama vile China na Malaysia zilianza kuwa na mipango ya kubadilika . Mabadiliko walionza nayo ni mifumo ya uwekezaji ikiwemo elimu yaani kuwa na mitaala ya uzalishaji . Fursa za kiuchumi zikatengenezwa kwa kuangalia uwezeshaji wa kimkakakati kwa kutumia rasilimali zilizopo ama zinazoweza kupatikana .
Asasi ya waandishi wa habari Pemba inaamini juu ya mijadala inayojenga – constructive dialogue kama ni zao la ustawi na amani ya kwa uwezeshaji wa vijana kwani vijana wasiokuwa na fursa na shughuli za kufanya ni rahisi kushawishika kwa kufanya maovu na kujiingiza katika vitendo ambayp vinaweza kuvuruga amani ya nchi . Kwa kuzingatia haya , kwa kushirikiana na shirinka la INTERNEWS tunachochea mijadala ya kijamii ambayo inaweza kubadilisha fikra zetu na kujenga jamiii yenye maendelea , amani na mshikamano .
Tuanze na mitaala yetu