NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MRATIBU wa huduma za Chanjo kwa mama, wasichana na watoto Pemba Bakar Hamad Bakar amesema, chanjo ni mkakati muafaka wa kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vitokanavyo na maradhi ya kuambukiza.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Maabara Wawi Chake Chake Mratibu huyo ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya Chanjo Barani Afrika alisema, chanjo pia hupunguza gharama kubwa za matibabu ambazo familia na Taifa ingetumia kutibu magonjwa.
Alisema kuwa, mkakati huo wa chanjo ni njia bora ya kudhibiti na kutokomeza maradhi na vifo vitokanavyo na saratani ya shingo ya kizazi, polio, surua, rubela, donda koo, kifaduro, T.B, kuharisha, nimonia, homa ya ini na mafua makali.
Alisema, ipo haja kwa waandishi kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo kwa watoto, kwani inasaidia kumkinga na magonjwa ambali ambali ambayo yangeweza kumsababishia kifo ama ulemavu wa maisha.
“Tuitumie wiki ya Chanjo kutoa elimu kwa jamii, kwa sababu kuna baadhi ya watoto hawapelekwi hospitali kupatiwa chanjo na wengine hukatishwa njiani, jambo ambalo linaweza kusababisha wakakumbwa na maradhi”, alisema mratibu huyo.
Akitaja malengo ya mkakati huo kuwa ni, kuwafikia kila mtoto kwa usawa, kupunguza magonjwa yanayozuilika, kutumia teknologia mpya katika kuboresha huduma za chanjo hasa maeneo ya mnyororo baridi, ukusanyaji takwimu na mawasiliano.
Kwa upande wake Meneja Chanjo Zanzibar Yussuf Haji Makame alisema, wanafanya juhudi mbali mbali katika kuhakikisha wananchi wanapata uelewa kupitia vyombo vya habari, pamoja na elimu ya afya kwa wahudumu wa afya.
“Nyinyi waandishi mutusaidie kutoa elimu kwa jamii, wiki hii ya chanjo waitumie kuwaleta watoto wao kupata chanjo, tunaamini kuwa elimu itawafikia walio wengi”, alisema.
Akielezea mafanikio ya chanjo Meneja huyo alisema, ni kutokomeza ugonjwa wa ndui, kudhibiti magonjwa ya donda koo, kifaduro na pepopunda, kudhibiti ugonjwa wa surua na kuweka wodi yake kwenye hospitali.
“Pia tumefanikiwa kupunguza vifo na magonjwa dhidi ya nimonia na kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, pia mwaka 2015 Tanzania ilithibitishwa kimataifa kwamba hakuna mzunguko wa virusi pori vya polio nchini”, alisema Meneja huyo.
Mapema akifungua mkutano huo, Afisa Mdhamini Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Yakoub Mohamed Shoka alisema, kwa vile wanadamu wanapaswa kukumbushwa, hivyo siku hizo zimewekwa maalumu kwa ajili ya kuangalia watu ambao hawafiki kwenye vituo vya afya kupata chanjo na ambao hawajakamilisha, ili wapatiwe katika vituo vya afya.
Alieleza kuwa, lengo la mkutano huo kwa waandishi wa habari ni kutoa taaluma ya umuhimu wa chanjo kwa watoto na wale wote walio katika lengo la kupatiwa chanjo.
“Ni utaratibu mzuri kwa sababu kila kazi haikosi mapungufu, pale ambapo pamepungua tujitahidi kuifanyia kazi kwa kuwahamasisha kinababa na kinamama kuwapeleka watoto wao kupata chanjo na kuweza kuwakinga na magonjwa”, alisema.
Kwa upande wao waandishi wa habari walisema kuwa, watajitahidi kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo kwa lengo la kuboresha afya zao.
Wiki ya Chanjo huadhimishwa kila ifikapo Aprili 26 hadi 30 ya kila mwaka, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu kwa Zanzibar ni ‘CHANJO HUWEKA JAMII PAMOJA, KAPATE CHANJO’