NA MWANDISHI WETU.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kwa kushirikiana na Kikosi Maalum kutoka Mkoa wa Kipolisi Ilala Jijini Dar es Salaam limekamata Pikipiki 48 na Bajaji 4 zinazosadikiwa kuwa za wizi ambazo wameuziwa wananchi mbalimbali Zanzibar
Akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Elisante Makiko Mmary amesema kufuatia operesheni Maalum iliyofanywa kuanzia April 28 hadi Mei 03 Mwaka huu wamefanikiwa kukamata Pikipiki 48 na Bajaji 4 zinazosadikiwa kuibiwa Dar es Salaam na maeneo mengine Tanzania Bara ambapo pia waliwakamata jumla ya watuhumiwa saba ambao wanatuhuniwa kupokea na wengine kusaidia kuziuza Pikipiki huku wakijua kwamba zimeibiwa
Aidha Kamanda huyo alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kuwabaini wamiliki halali wa vyombo hivyo kwa kushirikiana na mamlaka nyengine
Sambamba na hilo amewataka wananchi waliowahi kuibiwa vyombo vyao wafike kwenye vituo vya Polisi Jirani wakiwa na nyaraka ili kurahisisha utambuzi wa Vyombo vyao
Katika hatua nyengine Jeshi la Polisi limeendelea kuwaonya wale wote wenye nia ya kushiriki au kufanya uhalifu kuwa Jeshi hilo litawachukulia hatua za kisheria na hivyo kuwataka kuacha mara moja njama hizo na wafuate Sheria na taratibu za Nchi zilizowekwa