NA ZUHURA JUMA, PEMBA
MTU mmoja amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kamba huko Shengejuu Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis amemtaja aliyepatwa na mauti hayo kuwa ni kijana Abrahman Juma Mohammed (22) mkaazi wa Shengejuu Wilaya ya Wete.
Kamanda Sadi alifahamisha kuwa, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi majira ya saa 3:45 huko Kijijini kwao Shengejuu.
Kamanda Sadi alieleza kuwa, kabla ya kupatwa na mauti hayo marehemu alikwenda nyumbani kwao baada ya kupata msaada wa vyakula na pesa taslimu shilingi 100,000/- ambavyo vitu hivyo vilitolewa msaada.
“Lakini baada ya kufika nyumbani kwao na kujiangalia vizuri ile bahasha ambayo ilikuwa na zile pesa hakuiona katika mfuko wake wa suruali ambayo alikuwa amevaa na hivyo alianza kulalamika kuwa yeye amepewa vile vyakula pamoja na pesa taslimu shilingi 100,000/- , lakini baada ya bahasha ile ambayo ndani yake ilikuwa pesa hakuiona tena”, alieleza Kamanda Sadi.
Hata hivyo Kamanda Sadi aliongezea kusema kuwa, baada ya hapo jamaa wa karibu wa marehemu huyo walimpa ushauri kutulia ili aweze kufikiria kwa makini ni sehemu gani ambayo anahisi bahasha hiyo ameiweka.
“Baada ya kuondoka hapo ilikuwa ni majira ya saa 10:00 marehemu huyo hakuonekana tena mpaka wakati wa kuftari na ndio familia yake ikaanza kuingia wasiwasi na kuanza kumtafuta bila ya mafanikio, lakini baadae mdogo wake katika kuingia sehemu moja ndani mwao ndipo alipomkutia akiwa ananing’inia na tayari ameshafariki dunia”, alieleza Kamanda Sadi.
Kamanda Sadi alisema kuwa, baada ya kupata taarifa hiyo Jeshi la Polisi lilifanya mawasiliano na uongozi wa hospital ya Wete na kwenda katika tukio hilo na baada ya uchunguzi wa daktari ulibaini kuwa marehemu amefariki kutokana na kukosa pumzi baada ya kujitia kamba shingoni (kujitundika).
Mapema Kamanda Sadi aliwataka wananchi kuacha tabia hii ya kujinyonga pasi na sababu ya msingi ya kufanya hivyo na pale ambapo watakuwa na msongo wa mawazo ni vyema kutulia na sio kuchukua uamuzi usio faa.
Hili ni tukio la kwanza la kujinyonga mtu katika Mkoa wa Kaskazini Pemba tokea mwaka huu uanze.
Wakati huo huo Kamanda Sadi alieleza kuwa kwa wiki iliyopita hali ilikuwa ni shuari na salama katika Mkoa huo na hakukuwa na tukio lolote la kutisha ambalo liliripotiwa ukilinganisha na wiki nyengine.