Thursday, January 9

“Kufungwa kwa Timu ya Simba ni maandalizi finyu”. wadau wa soka.

NA SAID ABRAHMAN.

 

BAADA ya timu ya Simba kupokea kichapo Cha 4-0 dhidi ya Kaizer Chief ya Afrika ya Kusini, wadau wa soka nchini wameeleza kuwa tatizo ambalo limejitokeza kwa timu hiyo ni maandalizi finyu kwa timu hiyo.

 

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi  huko Wete, mchezaji mkongwe wa timu ya Jamhuri S.Club na timu ya taifa ya Zanzibar Herous Abdalla Ali Hemed (Kidala), aliaeleza kuwa timu ya Simba haikuwa na mazoezi ya kutosha katika kuelekea mpambano wao huo.

 

Kidala ambae kwa sasa anajishughulisha na soka kwa vijana chipukizi kuwa timu hiyo ilikuwa inahitaji kupata angalau michezo miwili ya kujipima nguvu kabla ya kukutana na nguli hao wa Afrika ya Kusini.

 

Kidala alieleza kuwa mchezo ambao ulikuwa upigwe Kati ya Simba na Yanga ambao uliahirishwa ilikuwa tosha kwa Simba kujipima nguvu ili kuona kasoro zilizomo katika kikosi hicho kabla ya Safari yao na kuweza kuweka sawa.

 

“Timu ya Simba sio yakufungwa mabao yote yale ila kuna kasoro fulani fulani ambazo zimejitokeza ikiwa ni maandalizi mazuri hayakufanywa yakutosha, kwani timu yetu iliweza kukosa mechi za kujipima nguvu na ilikaa wiki mbili haina hata mchezo mmoja mkubwa iliyocheza,”alisema Kidala.

 

Hata hivyo Kidala aliiomba Serikali kupitia vyama vya michezo nchini kuandaa kamati maalum ambayo itakayoweza kuratibu timu ambazo zinashiriki michezo ya kimataifa.

 

“Ombi langu kwa Serikali kuweza kuandaa kamati ambayo itakayoweza kushughulikia michezo yote ya kimataifa ambayo timu zetu zitakuwa zikishiriki na kamati hii iweze kusimamia michezo yote ya kimataifa na iweze kushirikiana vizuri na vilabu vyetu,” alisema Kidala.

 

“Katika mchezo huu Serikali iliweza kuiwachia Simba kama Simba na hakukuwa na mashirikiano ya kutosha ambayo yangeifanya Simba iweze kufaulu katika mchezo ule,”alisema Kidala.

 

Sambamba na hayo Mwanamichezo huyo alieleza kuwa kwa mchezo uliobaki ambao unatarajiwa kupigwa katika Kiwanja Cha Mkapa jijini Dar es salaama ana matumaini makubwa ya Simba kushinda mchezo na hivyo kupata nafasi yakuendelea na mashindano hayo.

 

” Nakumbuka katika miaka ya 1970 au 1980, Simba hii hii iliweza kufanya maajabu makubwa kwani ilifungwa na timu ya Mfulila wanderous magoli manne (4) kwa sifuri nyumbani lakini Simba iliweza kuifunga timu hiyo magoli matano (5) tena nyumbani kwao,kwa hiyo hili sio geni kubwa ni ari kwa mwalimu na wachezaji tu,”alifahamisha Kidala.

 

Kidala aliwataka Wana michezo wote wa Tanzania kuungana pamoja na kuisapoti timu yao na kuacha kuwatupia lawama wachezaji kwani kipindi hichi sio Cha kulaumu bali ni kutafakari na kuona wapi wamekosea ili marekebisho yafanyike na ushindi uweze kupatikana.