Wednesday, January 8

USTAHAMILIVU wa kisiasa ni jambo muhimu kwa jamii na ndani yake huzaa matunda.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

USTAHAMILIVU wa kisiasa ni jambo muhimu katika jamii ambalo ndani yake huzaa amani, upendo na utulivu kwa wanajamii.

Mfano wa hilo ni kwamba, viongozi wangekuwa na ustahamilivu na uvimilivu, siasa isingekuwa chungu mithili ya shubiri hasa katika bara la Afrika.

Yapo mataifa mengi duniani sasa yamerudi nyuma baada ya kukosekana kwa uvumilivu wa kisiasa, watu hufarakana na kisha kuzaa mapigano.

Kukosa uvumilivu mataifa mengi huingia katika machafuko na kusababisha vifo, watu hukosa makaazi na wengine kuhamia nchi nyengine wakiwa wakimbizi.

Ingawa kwa Tanzania bado viongozi wa vyama vya siasa wamejengwa na chembe kubwa ya uvumilivu wa kisiasa, jambo linalopelekea kufarakana na kisha kuelewana.

Imani ya dini, uvumilivu wa kuzaliwa, utamaduni wa kuhurumiana, na udugu wa kuzaliwa kwa jamii ya Tanzania na Zanzibar, siasa hufanyika na kupita bila ya kuacha madhara makubwa.

HALI YA ZANZIBAR KISIASA NA UVUMILIVU

Zanzibar ambayo iliingia kwenye mfumo wa vyama vingi tangu mwaka 1992, historia ya uvumilivu na utamaduni wa kuhurumiana ndipo ilipo anzia.

Utamaduni na hamu ya kuingia ikulu kwa kila mwanasiasa kwenye uchaguzi mkuu kwa chaguzi kadhaa zilizopita, kamwe haikuiweka Zanzibar ikiwa salama na kupelekea siuntofamu za hapa na pale.

Kwa wakati huo maridhiano kadhaa yalifanywa hapa Zanzibar, lengo likiwa ni kuwaweka pamoja wananchi wa Zanzibar ambao asili yao ni udugu.

KATIBA YA ZANZIBAR MWAKA 1984

Ndio chombo kinachowaunganisha wazanzibari, ambacho chenyewe kimefanyiwa marekebisho maalumu ili kufyeka makovu, uhasama, siuntofamu zinazojitokeza kila baada ya kumalika kwa chaguzi za kisiasa.

Katiba hiyo ikaelekeza kwenye kifungu chake 39 (3) kuwepo kwa Makamu wa Kwanza ambae atatoka katika chama kilichoshika nafasi ya pili na kuunda Serikali iliyoitwa ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Sambamba na hilo pia kuwepo Makamu wa Pili katika kifungu cha 39 (6) ambae hutoka kwenye chama kilichotoa Raisi lengo ni kuwarejesha pamoja, kujenga umoja, mshikamno na maridhiano ya wazanzibari.

WANANCHI NA MARIDHIANO.

Khalfan Ali Mohamed mkaazi wa Pandani Wete anasema uvumilivu ni muhimu sana katika kuleta amani na umoja kwani, inaondosha mifarakano na mipasuko.

 

Anasema, unapokuwepo uvumilivu ni kwamba, wananchi wamejua nini Demokrasia na siasa na hivyo kuamini kila mmoja ana haki ya kuchagua chama anachokitaka bila ya kumkwaza mwengine.

 

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeleta umoja na mshikamano kwa wananchi na hii inaonesha dhahiri kwamba kumekuwa na uvumilivu wa kisiasa, sasa tunaishi kwa amani”, anaeleza.

 

Anakumbuka kuwa, sheha akiitisha mkutano wa wananchi, baadhi yao hawahudhurii kwa kisingizio cha kuwa wameitwa na Serikali, lakini kwa sasa wanafurika uwanjani kwa sababu ya kuacha itikadi zao za kisiasa.

 

Hamad Hassan Ame mkaazi wa Kengeja Wilaya ya Mkoani anasema, kuna umuhimu mkubwa wa uvumilivu na maridhiano ya kisiasa kwa ajili ya kuleta maendeleo, kama ilivyo azma ya mfumo wa vyama vingi nchi.

 

“Inavyotakiwa chama kitakachoshinda na kukaa madarakani, kikosolewe na pajengwe hoja ya kuweza kurekebisha pale penye mapungufu bila ya mtoa hoja kushughulikiwa”, anafahamisha.

 

Asha Issa Ali wa Chake Chake anasisitiza kutochezewa kwa Katiba ili kulinda amani na kuleta umoja, kwani iwapo itavunjwa, itasababisha nchi kupoteza rasilimali watu na fedha na hatimae Serikali itahitaji fedha nyingi kuirejesha hali.

 

Mkaazi wa Kangagani Wilaya ya Wete Mohamed Rashid Ali anasema, uvumilivu wa kisiasa unazuia mfarakano na nchi inabaki kuwa salama na yenye kupata maendeleo kwa haraka.

 

“Kwa maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar lazima tusiwasahau kuwaweka kwenye historia marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Rais Dk; Hussein Mwinyi sasa kutuweka pamoja”, anasema.

 

Anasema, nchi haiwezi kutulia ikiwa watu hawatovumiliana na inaweza kuvunja mustakbali wa mambo yote yaliyomo kwenye jamii.

 

Anasema, amani ni matunda ya haki, hivyo ipo haja kwa nchi kuendeshwa kwa kuzingatia Sheria na kuhakikisha Katiba inalindwa kama ilivyo azma ya Rais Dk Mwinyi.

 

Awena Salim Kombo wa Kangagani Wilaya ya Wete anaeleza, uvumilivu umeleta umoja, mashirikiano, kwani wananchi wametulia, wanafanya shughuli zao kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao.

 

WANASIASA

 

Hafidh Abdi Said amabe ni Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kusini Pemba anasema, uvumilivu katika siasa na unakuja na subra pale ambapo viongozi watatekeleza yale ambayo wanayaahidi kwenye kampeni.

 

Anachosema yeye kitu wanachokitaka wananchi ni maendeleo na sio kitu chengine, hivyo iwapo yatatekelezwa wanayoyasema kwenye kampeni wataendelea kuvumilia, ili amani itawale nchini.

 

Mwenyekiti Vijana CCM Wilaya ya Wete Ibrahim Mustafa Mussa, anaeleza katika uchaguzi mara nyingi hutokea vurugu ambalo husababishwa pale ambapo mmoja hawakuridhika na matokeo.

 

“Kinachopelekea watu kuwa na ustahamilivu ni kuyakubali matokeo ambayo yatakuja, ikiwa wataridhika kuwa wameshindwa, ndio inasaidia kuwepo amani katika nchi”, anasema.

 

Kuna athari mbali mbali zinaweza kujitokeza iwapo wananchi hawatokuwa na uvumilivu, ikiwa ni pamoja na mgogoro wa sisi kwa sisi, ambao ni hatari katika maisha.

 

Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Kaskazini Pemba Mwinyi Juma Ali anaeleza, kulikuwa na chuki katika jamii ambazo zinahatarisha kila kitu ikiwemo maendeleo ya nchi.

 

“Tumekubali kupokea Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa ajili ya kuiepusha nchi na misukosuko, kwa sababu Rais anakwenda mbio kuzungumzia amani na utulivu”, anasema.

 

Anaeleza, kila mmoja anatakiwa afuate sheria bila ya kushurutishwa, ingawa wananchi wanahitaji zaidi busara, hekima na kuelimishwa juu ya mambo mbali mbali.

 

“Dk: Mwinyi kaonesha mfano kwamba ana nia ya kutuweka pamoja na kuna umuhimu kweli kwa sababu bila ya umoja na mshikamano nchi haiwezi kupiga hatua yoyote ya kimaendeleo”, anasifu Mkurugenzi.

 

VIONGOZI WA DINI

 

Katibu wa Kamati ya Maadili kupitia Baraza la Kiislamu Zanzibar Abdalla Mnubi Abas, anasema jamii inapata kuwa na utulivu na kufanya mambo yao na maisha kuwa mazuri.

 

Kwa sababu wanashuhudia baadhi ya nchi watu wanashindwa kuvumiliana na kusubiriana kwa mambo ya kisiasa na hivyo kuingia katika majanga ya vita na hatimae kuingia kwenye matatizo ya kiuchumi.

 

“Nchi ikiwa haina amani hata nafasi ya kuabudu inakuwa hakuna, hivyo tustahamiliane ili kupata nafasi ya kuabudu na kutekeleza ibada nyengine”, anasema.

 

Allah ameeleza katika Qur-an tukufu kwamba ‘tushikamane katika kamba moja wala tusifarikiane…’ hivyo basi kwa vile wote ni wamoja hakunabudi kushirikiana katika kuhakikisha amani inadumu.

 

Mchungaji wa kanisa RGC Minazini Chake Chake Isack Maganzo Nzilamoshi anasema, uvumilivu kwenye siasa unakuja pale mambo yakienda vizuri na haziwezi kujitokeza changamoto zozote.

 

Dini yao Isack inaeleza kwenye Bibilia kuwa ‘kuweni na amani na watu wote’ …hivyo wanahimizwa amani kwa watu wote sambamba kusisitizwa kumuheshimu kiongozi aliepo madarakani.

 

“Bililia imeeleza kuwa hakuna kiongozi ambae hajapata baraka za Mungu na tunaamini hilo, kwa hiyo tumuheshimu na kuheshimu kila mtu na hilo litasaidia kuleta amani”, anaeleza.

 

ASASI ZA KIRAIA   

 

Tatu Abdalla Mselem ambae ni Mratibu wa Jumuiya ya Tumaini Jipya (TUJIPE) anasema, ili nchi ifanikiwe katika hilo ni lazima siasa ziwe za uvumilivu.

 

“Kwa sababu tukiichukulia siasa kama siasa tutakuwa hatufikii malengo na wala hatuwezi kutekeleza mambo yetu, tuangalie saivi tuna hii Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo inahitaji uvumilivu mkubwa wa kisiasa”, anaeleza.

 

Anafahamisha, kama kila mmoja atainua mbavu zake katika mrengo wake ina maana hapatokuwa na maendeleo, hivyo jamii ikielekea kwenye maendeleo panahitaji uvumilivu wa kisiasa.

 

Ikiwa hakutokuwa na uvumilivu wa kisiasa nchi inaweza kuwa katika hali mbaya sana, kwani hilo wamelishuhudia katika kipindi cha nyuma ambacho hakukuwa na uvumilivu wa kisiasa, hali ilikuwa si shuwari na maendeleo hayapatikani.

 

“Unakuta kila mmoja anavutia kwake, hii yangu, hii yangu, hatimae kamba kukatika katikati na matokeo yake hakuna maendeleo ya kweli, hivyo kila mmoja aone anaweza kushiriki katika shughuli za kimaendeleo”, anasema.

 

Khalfan Amour Mohamed kutoka Jumuiya kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa Akili Pemba, anafafanua kuwa kunapokuwa na uvumilivu wa kisiasa inaleta upendo kwa wananchi kama ilivyo sasa.

 

“Kama hakuna uvumilivu wa kisiasa, itakuwa hatupendani na hapo ndipo amani itatoweka, hivyo tukivumiliana tutashirikiana bila kujali itikadi zetu za kisiasa”, anasema.

 

Anaeleza, pia jamii inajengeka kuwepo ile dhana ya usawa kwa wote hasa katika huduma za kijamii, kwa sababu unapokuwepo usawa pia watu hupendana na kuishi ushirikiano.

 

Jeshi la Polisi linaamini kuwa, nguvu na ustahamilivu wa kisiasa uliofanywa na marehemu maalim Seif Sharif Hamad na Rais dk Hussein Mwinyi ni maamuzi ya viongozi wakuu ambayo yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa.

 

Richard Tadei Mchomvu ambae ni Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba anafahamisha kuwa, kwa upande mwengine siasa ni shughuli ya kijamii inayofanywa na wanajamii ambao wanatofautiana mitazamo na falsafa, hivyo ili iende vizuri lazima jamii iwe na uvumilivu.

 

“Vyama vya siasa vina kanuni na taratibu zake ambazo wanapewa, hivyo jambo la msingi ni kujipanga ili kuzifuata na kuwaelekeza wananchi wake”, anasema Kaimu huyo.

 

Anasema, Jeshi la Polisi lina nafasi kubwa ya kusimamia sheria ili nchi ibaki kuwa salama na wananchi waishi kwa amani na utulivu kama ilivyo sasa.

 

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud anasema amani na umoja ni kitu cha msingi katika nchi, kwani huwaweka wananchi pamoja na kufanya shughuli mbali mbali za kimaendeleo.

 

“Binadamu tunatakiwa tuvumiliane katika kila jambo na huo ndio ubinadamu, uchaguzi umemaliza sasa tufanye shughuli za kimandeleo, siasa isitufanye tukaharibu haiba ya nchi yetu”, anaeleza.

 

Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeundwa kwa mujibu wa sheria ambapo ina lengo la kuwaweka wananchi pamoja kwa ajili ya kushirikiana katika shughuli mbali mbali ili kuiletea nchi maendeleo.

 

Rais wa Zanzibar dk Hussein Mwinyi wakati akimuapisha mrithi wa Maalim Seif, Othman Massoud Othman kuwa Makamo wa kwanza amesema, umuhimu wa uvumilivu na maridhiano ya kisiasa ndio chachu ya kufikia maendeleo ya kweli.

 

“Maridhiano haya tuliyoyafikia Zanzibar ni sehemu ya kufikia Zanzibar yenye neema, uimarishaji wa uchumi wa buluu na tutatekeleza tuliyoyaahidi kwa ujasiri”, anasema.

 

Akiwahutubia wananchi waliofika kumpokea juzi uwanja wa ndege Pemba, Makamo wa kwanza wa Rais Zanzibar Othman Massoud Othman amesema Serikali ya Umoja wa kitaifa ndio suluhisho la wazanzibari.

 

Anasema, atafanya kila njia kuhakikisha maridhiano hayo yanakuwa endelevu na kuleta maslahi mapana ya wazanzibari kama ilivyokuwa azma ya waasisi wa maridhiano hayo ya dk; Hussein Mwinyi na marehemu Maalim Seif.