Monday, November 25

Jamii ifuate njia sahihi za Mwenyezi Mungu na kuachana na imani potofu kuwa mwanamke hana nafasi ya kumiliki ardhi: Msaidizi katibu Ofisi ya Mufti Pemba.

MSAIDIZI Katibu Mufti Pemba Shekhe Said Ahmed Mohammed, akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la umiliki wa ardhi kwa wanawake, huko katika ukumbi wa ofisi ya Katiba na sheria Gombani Chake Chake Pemba
MWENYEKITI wa jumuia PECEO Ali Mohammed Chande akifunga kongamano la umiliki wa ardhi kwa wanawake huko katika ukumbi wa ofisi ya Katiba na sheria Gombani Chake Chake Pemba
KATIBU wa jumuia ya PECEO Juma Said, akizungumza na wadau mbali mbali katika ufunguzi wa kongamano la umiliki wa ardhi kwa wanawake, huko katika ukumbi wa ofisi ya Katiba na sheria Gombani Chake Chake Pemba

PICHA NA SAID ABDULRAHMAN, PEMBA

 

NA SAID ABRAHMAN.

 

JAMII imeshauriwa kuacha mazoea na badala yake, kufuata njia sahihi za Mwenyezi Mungu ambazo zitaweza kupelekea kuondokana na imani potofu, kuwa mwanamke hana nafasi katika jamii ya  kumiliki ardhi.

 

Hayo yameelezwa na Msaidizi katibu Ofisi ya Mufti ofisi ya Pemba Sheikh Said Ahmad Mohammed, wakati alipokua akizindua  mradi wa miezi sita wa uhamasishaji wa upatikanaji wa hati miliki za ardhi kwa wanawake, unaoendeshwa na Jumuiya ya kuwauhamasishaji wa upatikanaji wa hati miliki za ardhi kwa wanawake, unaoendeshwa na Jumuiya ya kuwezesha jamii Pemba (PECEO), hafla ya uzinduzi iliofanyika mjini Chake Chake.

Shekh Said alisema njia sahihi ni pale mmoja katika famialia anapofariki, mirathi ikachukua nafasi yake na wala isicheleweshe, ili kuwapata haki zao ikiwemo wanawake.

 

Alifahamisha kuwa, Serikali imeweka utaratibu Maalum wa kuunda taasisi inayoshughulikia jambo hilo, hivyo jamii inapaswa kutumia taasisi hiyo, katika masuala mazima ya mirathi na itapelekea kuondoa migogoro iliyopo kwa jamii.

 

Aidha aliwataka Masheha kutambua kuwa wao ni wadau wakubwa katika kufanikisha suala la mirathi, sio vibaya mmoja katika shehia yake ananapofariki na kwenda kuishauri familia, ili suala la mirathi liweze kufanyika kwa haraka na kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza.

 

“Hapo zamani zama za ujahilia wanawake walikuwa hawana uthubutu wa mirathi, wala kumiliki mali ikiwa ni pamoja na ardhi jambo lililokua likipelekea kukosa haki zao za msingi”alisema.

 

Aidha Shekhe Saidi alisikitishwa na Matendo, ambayo yanafanywa na jamii ya kutumia madaraka au nafasi zao vibaya, kwa kuona mwanamke hana haki ya kurithi mali na kuacha mienendo ya kiislamu na kurudia katika zama za ujahilia.

 

Alisema suala la migogoro ya ardhi ndani ya jamii, la kuwanyima mirathi wanawake ni jambo ambalo linafanywa ndani ya jamii husika inayowazunguruka.

 

“katika kipindi hiki suala la migogoro ya ardhi imeongezeka na kuleta changamoto kubwa, ambazo zimekuwa zinamkabili mwanamke, changamoto zinasababishwa na mazoea tuliyonayo ya kutoshughulikia mirathi, wakati miongoni mwetu anapofariki na kuacha mali, kupelekea wanawake wengi kukosa haki zao”alisema.

 

Mapema Mratibu wa jumuia ya PECEO Juma Said, alifahamisha kuwa lengo la mradi huo ni kuwahamasisha wanawake na jamii kwa ujumla, ili waweze kutambua kuwa nao wana haki ya kumiliki ardhi.

 

“PECEO imeweza kuanzisha mabaraza ya wanawake ya ardhi, katika Shehia 10 za Wilaya ya Mkoani, wenyeviti wa mabaraza hayo ni Masheha wa Shehia husika, lengo ni kutaka kuona changamoto zipi ambazo mwanamke anakabiliana nazo katika kumiliki ardhi”alisema Juma.

 

Alisema baada ya kugundua changamoto nyingi zinawapata wanawake katika masuala ya umiliki wa ardhi, wafadhili wao waliamua kuwapatia tena mwendelezo wa mradi, ili kuzitatua changamoto hizo.

 

Akitoa mada katika ufunguzi huo, Mwanasheria kutoka Ofisi ya Katiba na sheria Pemba Bakar Omar, alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo katika jamii ni uwelewa mdogo kwa wananchi kutumia na kumiliki ardhi.

 

“Wanawake wengi katika jamii zetu wanapofiliwa na waume zao, ndugu wa karibu wanadhulumiwa haki zao ikiwemo kukosa kupata mirathi yao ya ardhi”alisema.

 

Alisema kuwepo kwa urasimu wa ardhi kwa wanawake wanapoomba sehemu ya ardhi, katika mamlaka husika huzungushwa sana ili aweze kushindwa.

 

Nae Salma Omar Ali kutoka Kamisheni ya Wakfu na Mali ya amana Pemba, alizitaka taasisi zinazoshughulikia ardhi kutoa elimu kwa uwazi kwa wanawake ili waweze kujua haki zao.

 

Aidha Salma aliwataka Masheha kutoa taaluma kwa jamii, hasa pale mtu anapofiwa na mumewe ili waweze kupata haki zao kwa haraka na sio kuwahangaisha hangaisha.

 

Akifunga kongamano hilo Mwenyekiti wa bodi wa PECEO Ali Mohammed Chande, alisema kuwa lengo la mradi huo ni kuwasaidia wanawake ili kuweza kutambua haki yao, katika mirathi na wao waweze kufanikiwa.

 

Hata hivyo Chande alisema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa wanaume wengi ni kuwasumbua wanawake, hivyo ni wajibu wao kuwapatia elimu juu ya umuhimu wa mirathi.

 

Mradi wa umiliki wa ardhi kwa wanawake, unaoendeshwa na Jumuiya PECEO kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society.