RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuna umuhimu wa Serikali kutunga Sera, ili kukiwezesha Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU) kufanya kazi kwa taratibu na mfumo maalum.
Dk. Mwinyi amesema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar, alipokutana na Uongozi wa Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU).
Amesema kuna umuhimu kwa serikali kutunga sera itakayoendana na sheria ili kukiwezesha ZASU kufanya kazi kwa taratibu na mfumo maalum ikiwemo ushughulikiaji wa haki na utatuzi wa matatizo mbali mbali wanayopata mabaharia.
Alisema anakusudia kufanya kikao cha pamoja kitakachowahusisha wadau, wakiwemo viongozi wa Shirika la Meli, Shirika la Bandari pamoja na Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) ikiwa ni njia ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazokwaza uendeshaji wa Chama hicho.
Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali itazifanyia kazi changamoto na mapendekezo mbali mbali yaliowasilishwa, ikiwemo ya kupata taasisi itakayoweza kuingiza fedha ili kukiwezesha chuo cha Mabahari kinachokusudiwa kujengwa nchini kuweza kujiendesha.
Aidha, Dk. Mwinyi alikubali ombi la Uongozi wa Chama hicho la kuwa mlezi wa Chama cha Mabahari Zanzibar (ZASU).
Mapema, Katibu wa Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU) Hussein Nassor Uki, amesema chama hicho kinakabiliwa na changamoto mbali mbali katika uendeshaji wa shughuli zake, ikiwemo ya kuitaka ZMA kuweka sharti kwa kampuni zinazosajili meli zake hapa nchini kutoa nafasi ya angalau mabaharia watano kufanyakazi katika Meli hizo, ikiwa ni hatua ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana waliomo katika sekta hiyo.
Alisema kuna umuhimu wa Serikali kufikiria umuhimu wa kuanzisha mafunzo ya muda mfupi, wakati huu ikiazimia kujenga Chuo maalum cha Mabaharia.
Aidha, alisema kuna haja kwa Serikali kuangalia suala zima la mikataba na maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya ndani vya usafiri, vinavyofanya shughuli zake hapa nchini, ikingatiwa wafanyakazi wa vyombo vyote pamoja na vile vinavyomilikiwa na Shirika la Meli, hawana mikataba.
“Lakini pia tumependekeza kwa ZMA wafanyakazi wa kima cha chini, walipwe angalau shilingi Milioni moja kwa mwezi , hivi sasa baadhi ya kampuni zinawalipa shilingi 300,000/- tu”, alisema.
Alieleza kuwa wakati huu Zanzibar ikielekeza nguvu kuinua uchumi wake kupitia uchumi wa Buluu, kuna umuhimu wa kuanzisha Mahakama ya Mabaharia kama zilivyo nchi nyengine Duniani, ili kuwawezesha Mahabaria kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu ya kazi zao.
Aidha, aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa wanachama wa ZASU kupata fursa ya kushiriki katika Bodi mbali mbali zinazoundwa na wadau wa Chama hicho, ikiwemo ZMA, Shirika la Bandari pamoja na Shirika la Meli, kama ilivyokuwa katika kipindi cha nyuma.
Alisema hatua hiyo itakiwezesha chama hicho kupata muunganiko na mashirika la Kimataifa, ikiwemo Shirika la wafanyakazi wa Usafiri Duniani.
“Kwa kipindi kirefu umekosekana utatu kati ya ZASU, Serikali (ZMA) pamoja na mashirika ya Kimataifa, kiasi ambacho baadhi ya nyakati tunakosa taarifa kwa wakati za ushiriki katika mikutanao muhimu inayoandaliwa”, alisema.
Katibu Nassor alitumia fursa hiyo kumuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi kuwa mlezi wa ZASU, kama ilivyokuwa kwa Muasisi na Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume, sambamba na kuomba kupatiwa gari ili kufanikisha utendaji kazi wa chama hicho.
Chama cha Mabaharia Zanzibar (ZASU) ni chama cha kwanza cha wafanyakazi kilichoanzishwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume mnamo Septemba 22, 1949, kupigania haki na maslahi ya Mabaharia nchini.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar.