Sunday, November 24

“Hatukatai agizo la Serikali la kuhama kwenye nyumba, lakini hatujui sehemu ya kwenda kuishi”Wakaazi wa nyumba za maendeleo Kengeja.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI wanaoishi nyumba za maendeleo Kengeja wilaya ya Mkoani Pemba kwa miaka 44 sasa, wamesema hawakatai agizo la Serikali la kuhama kwenye nyumba hizo kwa sababu ya uchakavu, lakini hawajui sehemu ya kwenda kuishi.

Walisema, hali duni ya maisha walionao ndiyo iliyosababisha nyumba hizo kuchakaa kwa muda, hivyo kwa sasa wanahitaji kupewa makaazi na Serikali, ndipo wahame kwenye nyumba hizo.

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo walisema, kutokana na hali zao za kipato, wanashindwa kuzitengeneza nyumba hizo hasa ukizingatia ni za gorofa, hivyo ni vyema Serikali kuu ikaingilia kati kadhia hiyo.

Walisema, wanathamini na kuheshimu agizo ‘notice’ iliyotolewa na serikali ya kuwataka hawahame, ingawa kwa sasa hawajui eneo gani wahamie.

“Sisi hatutaki tukae kwenye hizi nyumba kwa sababu tuna hofu isije ikatuangukia, imebomoka ila pahala, inavija, usingizi hatupati hasa kukiwa na mvua”, walisema wakaazi hao.

Mmoja kati ya wananchi hao, Mohamed Said Machano alisema, anaishi kwenye nyumba hizo kwa zaidi ya miaka 40 sasa na akitolewa hapo hajui wapi akahamie na familia yake.

Alisema kuwa, amepokea barua kutoka Serikalini ikimuelekeza kutaka ahame na kusema kwamba hapingani na agizo hilo lakini hajajua wapi akahamie.

“Ni kweli nimepokea barua kutoka kwa mamlaka husika kwamba nihame kwenye hili jengo, lakini Serikali haijatuandalia mazingira mengine ya kwenda kuishi’’, alieleza.

Nae Mohamed Jafu Khamis alisema, alihamia ndani ya nyumba hiyo akiwa na wazee wake tangu mwaka 1977, ambapo miaka 15 iliyopita baada ya nyumba hizo za ghorofa kuvujika, walipeleka kilio Serikalini.

Alieleza, baada ya hapo Idara ya Majenzi ilipeleka bati 1000 kwa ajili ya kuezekwa, ingawa baada ya muda waliziondoa na kuziacha nyumba hizo zikivuja.

“Tatizo la uchakavu wa nyumba hizi ni kutokana na kupenya maji yanayotuwama juu ya varanda, maana hayana miundombinu ya kumwagika chini, sasa ndio inayoharibu nyumba”, alieleza.

Nae Asha Makame Kombo alisema, ataendelea kubakia ndani ya nyumba hiyo, hadi pale serikali itakapompatia eneo jengine la kuishi na watoto wake.

“Ni kweli taarifa za kunitaka kuhama ndani ya nyumba hii ya maendeleo hapa Kengeja ninayo, lakini najiuliza niende wapi, maana hapa niliolewa zaidi ya miaka 40 iliyopita, sina pakwenda’’, alieleza.

Alieleza kuwa, baadhi ya wenzake wameshama kwa vile walikuwa na eneo jengine la kwenda, ingawa yeye alitegemea hapo, hivyo kama kuna amri ya kuhama, kwanza apewe eneo la kujihifadhi.

Kwa upande wake Mtumwa Khamis Juma, anasema ataendelea kutoa maji yanayoingia ndani ya nyumba anayoishi, kwani hana mpango wa kuhama kwa sasa.

“Mvua ikinyesha yote huishia ndani ya vyumba ninayolala na watoto wangu, lakini kama nikihama hapa niende wapi au nikaishi chini ya mti, maana idadi ya watoto na wajukuu nilio nao, ndio mtihani’’, alifafanua.

Mwananchi Juma Khamis Ali, alisema ingawa wazazi wake wameshafariki na kumuachia nyumba hiyo ya urithi, hajui akaishi wapi, maana walikondolewa na Serikali, sasa kuna makaazi ya askari wa Magereza.

“Mama na baba yangu walihamishwa kijijini kwetu Makomba ili kupisha ujenzi wa makaazi wa nyumba na gereza, na tulikuwa na nyumba na mashamba, sasa kama Serikali inanihamisha humu, inipe makaazi mengine’’, alieleza.

Ali Khamis Kheir miaka mwenye miaka 80 alisema, ikiwa Serikali inawataka wahame, kwanza wawatengee maeneo ya kijihifadhi na familia zao.

“Sisi wengine kule ambako tulikubali kupisha makaazi ya magereza, tulikuwa na viwanja zaidi ya kimoja, na tukakubali kuletwa hapa, sasa kama pameshachakaa tupewe makaazi mengine’’, alisema Ali Kheir.

Aidha wananchi hao, walimuomba rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuwatembelea, ili kuona hali zao.

Walisema, nyumba hizo za ghorofa ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, ambazo ziliasisiwa na rais wa kwanza wa Zanzibar, marehemu Abeid Amani Karume, hivyo ni vyema zikaendelezwa.

Sheha wa shehia ya Kengeja Mohamed Kassim, alikiri kupokea nakla ya barua hiyo, ambayo inawataka wananchi wake kuhama kwenye nyumba hizo.

“Sisi kama shehia tunapokea maagizo, hivyo suala la wapi wakae wananchi hao, ni jukumu la serikali kuu’’, alieleza sheha huyo.

Aprili 6, mwaka huu wananchi hao 27 wanaoishi kwenye nyumba hizo, walipokea taarifa ‘notice’ ya kutakiwa kuhama kutokana na uchakavu wa nyumba hizo unaohatarisha maisha yao.

Barua hiyo yenye kumbu kumbu namba EA.133/172/01/46 ilioonesha kutoka kwa Afisa Mdhamini wa wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makaazi Pemba Bakar Ali Bakar.

Sehemu ya barua hiyo, imewataka wananchi hao kuhama kwa vile ndani ya nyumba hizo, kumekosekana huduma za kibinadamu kama vile maji safi na salama na uchakavu wa majengo hayo.

Nyumba hizo za maendeleo zenye ‘block’ tatu, zina uwezo wa kuishi familia 48, na tayari famila 21 zimeshahama majengo hayo kwa muda, na zilizokabidhiwa barua za kuhama hadi sasa ni familia 27, ambao walihahamia hapo mwaka 1977.

Nae Afisa Mdhamini wa wizara ya Ardhi, Maendeleo ya Makaazi Pemba Bakar Ali Bakar ni kweli waliwaandikia wakaazi hao barua za kuhama kwenye nyumba hizo, kwani tayari zimeshakuwa chakavu, ingawa kunatafuta utaratibu wa kuwatafutia sehemu.

Aawali wananchi hao walikabidhiwa nyumba hizo kama fidia, baada ya kuhamishwa kwenye makaazi yao ya asili eneo la Makomba shehia ya Kengeja, ili kupisha ujenzi wa chuo cha mafunzo na nyumba za askari, na kukabidhiwa na rais wa awamu ya pili Aboud Jumbe Mwinyi.