NA ZUHURA JUMA, PEMBA
Waswahili husema… ‘Usipoziba ufa utajenga ukuta’, msemo huu ni maarufu sana katika jamii zetu ambao hutumika kila uchao.
Ni msemo wenye maana kwamba ikiwa hukuondosha changamoto ama tatizo lingali dogo basi utagharamika kuliondosha.
Msemo huu kwa sasa uifanye jamii kuachana na rushwa muhali, kwa kudhibiti udhalilishaji kwa wanawake na watoto, kwani ukiongezeka utaigarimu jamii na Serikali kwa ujumla.
Jamii ni ngumu kuachana na rushwa muhali kwani huyaficha matendo ya hayo na baadae kusuluhishana, jambo ambalo sio sahihi.
Hiyo huchangia kuongezeka kwa udhalilishaji siku hadi siku na kuwaacha watoto kwenye mtihani, kwani huathirika kisaikolojia, kimwili na wengine kukosa elimu ambayo ndio mkombozi wa maisha yao.
Fatma Ali Khamis mkaazi wa chasasa Wete anasema, jamii bado imegubikwa na muhali kiasi ambacho kinawakwaza wale wachache walioamua kusimamia kidete kupiga vita udhalilishaji.
“Ikiwa hatukuondosha muhali ni vigumu kuondosha vitendo hivi kwani jamii nzima inamlinda mfanyaji wa udhalilishaji kuliko mtoto, ambae ndio taifa la kesho”, anasema.
Anafahamisha jamii ilivyooza kwa matendo hayo ingawa wanayamaza kimya kwa kile wanachodai kuwa wakisema watakuwa wametangaziwa aibu, hivyo wanaona ni bora kubaki kimya.
“Kunyamaza kimya kunampa nguvu mtendaji kwa sababu huona anafichiwa maovu yake, hivyo anaendelea kuwabaka wengine na hatimae anamaliza mtaa ama kijiji”, anasema mama huyo.
Khairat Ali Mbarouk wa Mkwajuni Wete anaeleza, watuhumiwa ambao wanafichwa na jamii, wote wana historia ya kuwabaka ama kuwalawiti watoto zaidi ya mmoja, kwani hawahofii kitu chochote.
“Jamii ikiamua jambo haiwezi kufeli, njia wanayoitumia kuwaziba midomo wazazi wanaokimbilia kwenye vyombo vya sheria wangeitumia kudhibiti vitendo hivi, wahalifu wangeogopa na tungeondokana na janga hili”, anafafanua.
Ali Mkubwa Ali mkaazi wa Mtambwe anaeleza, rushwa muhali ni donda ndugu lililoota kwenye jamii ambayo ni vigumu kuondoka, kunahitaji nguvu za ziada kudhibiti.
Anasema, iwapo mzazi atakuwa mstari wa mbele kutetea haki ya mwanawe, kufuatilia na kusimamia kesi ya mtoto wake, anaamini vyombo vya Sheria havina nafasi kubwa ya kumuachia huru mtuhumiwa.
“Vyombo vya Sheria vina mapungufu yake lakini ikiwa tutakuwa mstari wa mbele kutetea na kufuatilia tutavidi nguvu na wala hawatopata nafasi ya kufanya magube, maana jamii ikiamua imeamua, ila bado hatujataka”, anaeleza kaka huyo.
Mkaazi wa Kiungoni Wilaya ya Wete Rashid Abdalla Hamad anaeleza, baadhi ya wazazi hawaripoti kwenye vyombo vya Sheria wakati watoto wao wanapodhalilishwa na wengine wanaoripoti hutishiwa na jamii, jambo ambalo linachangia ongezeko la udhalilishaji.
“Wazazi wengine wanaona wanaporipoti watajitia aibu, hivyo hubaki kimya na mtoto anaendelea kudhalilishwa kwa sababu mfanyaji akiona watu wamenyamaza anaendelea na kazi yake hiyo”, anasema.
Anafahamisha, watoto wanaumia sana kwani kwenye watoto kumi basi saba wanafanyiwa ubakaji na ulawiti hasa vijijini, ingawa jamii inakaa kimya.
WAZAZI WENYE WATOTO WALIOFANYIWA UDHALILISHAJI
Wanasema, rushwa muhali inawaumiza sana katika kusimamia na kufuatilia kesi hizo, ingawa hawatokata tamaa ikiwa vyombo vya sheria vitakua pamoja nao.
Wanafahamisha, iwapo watapata ushirikiano, watakuwa na nguvu ya kufuatilia kesi zao pamoja na kuionesha jamii kwamba muhali hauwezi kusaidia chochote kwenye matukio ya udhalilishaji.
Katika mahojiano na wazee mbali mbali, kilichojitokeza ni wengi kuona jamii bado imegubikwa na muhali ambao unawakwaza wachache wanaoamua kusimamia kidete kupiga vita vitendo vya udhalilishaji katika jamii.
Jamii inawarudisha nyuma katika mapambano dhidi ya udhalilishaji pale inapotafutwa suluhu baada ya mtoto kufanyiwa udhalilishaji.
Mama mmoja, mkaazi wa Msuka Wilaya ya Micheweni anahadithia, alivyosikitishwa na mdogo wake kukaa kimya baada ya watoto wake kubakwa na baba yao wa kambo kwa kuhofia aibu na kuachwa na mumewe.
“Wakati mdogo wangu alipokwenda kujifungua, nilikwenda kukaa na watoto wake Mtambwe Wilaya ya Wete na ndipo mtoto mwenye miaka 15 akanieleza kuwa baba yake wa kambo anavyombaka, sikunyamaza nilikwenda kwenye vyombo vya Sheria kuripoti bila kumwambia mama yao”, alisema.
Baada ya siku kadhaa kupita alimuhadithia mama wa watoto hao, jambo ambalo lilikaribia kumkatisha tamaa kuendelea kufuatilia kesi hiyo, kutokana na kurushiwa maneno aliyokuwa hakuyatarajia.
“Kilichonishangaza na kuniumiza ni pale aliponambia kuwa, dada hukuweza kustahamili? kwa hili umenitia aibu, nilikaa kimya walipobakwa dada zake watatu na wameolewa kwa salama, wewe unalitangaza”, alifahamisha dada huyo.
Kumbe kabla ya mtoto huyo kubakwa, baba huyo wa kambo aliwahi kuwabaka dada zake huku mama yao mzazi akijua jambo hilo, ingawa alificha na kuendelea kuishi na mumewe.
“Kwa hiyo alianza kumbaka mmoja mmoja, akiolewa anachukuwa mwengine mpaka amewamaliza, maana huyu ndo wa mwisho kwa wanawe wa kambo, inauma sana”, anahuzunika.
Anashangaa kumuona mdogo wake bado anaishi na mumewe huyo alimfanyia ukatili kwa wanawe, huku akitaka waendelee kumfichia ubaya wake huo
Kutokana na muhali alionao mdogo wake, anamthamini zaidi mume wake aliyemuharibia watoto wake kuliko wanawe na familia yake, kwani alimuona mbaya dada yake kwa vile amesimama kidete kesi hiyo.
Mama wa mtoto wa kiume wa miaka kumi (10) kutoka shehia ya Bopwe Wete ambaye alilawitiwa anasema, jamii inawaona wabaya wale wanaosimamia kesi za watoto.
“Kwa vile niliamua kwenda kwenye vyombo vya sheria nimenuniwa mtaa mzima, nimekuwa mbaya, nanuka lakini hata siwasikilizi, nawaseme kisha watanyamaza, siwezi kuwathamini watu nikamuumiza mwanangu”, alisema mama huyo.
Kawaida yake akienda safari alikuwa anapita njia ambayo wanaishi mtuhumiwa, lakini amebadilisha kutokana na mama wa mtuhumiwa kumtukana na kumwita majina mabaya kwa sababu tu mwanawe kupelekwa kituo cha Polisi.
Anasisitiza kuwa, hata dunia nzima imsusie hawezi kurudi nyuma mpaka ahakikishe mwanawe amepata haki yake, labda vyombo vya sheria vimbadilikie, ila ikiwa watafuata sheria watakuwa pamoja.
Dada wa mtoto wa miaka 17 wa Shengejuu Wilaya ya Wete, aliebakwa na kupewa ujauzito anaeleza, muhali unawamaliza watoto wao na kuwapa nguvu wafanyaji wa matendo hayo.
Aliembaka mdogo wake ni mwalimu wa madrasa ambae alifukuzwa madrasa katika shehia jirani na kukataliwa kusalisha msikitini kutokana na kumbaka mtoto wa shemeji yake.
Alikimbilia shehia ya kwao na kutokana na jamii kugubikwa na muhali wa kijinga alikabidhiwa madrasa.
“Ni mtu mzima ana mke na watoto, hapo madrasa watoto watano
wameshakimbia kwa yeye na mdogo wangu pia alikimbia, lakini alifikwa na mtihani maana alipokufa baba yetu alikuwa anamjia kichwani hivyo akarudi”, anahadithia.
Anahadithia kuwa, baada ya kuona vile mdogo wake huyo alimwambia mwalimu wake amuandikie kombe (dawa), ili asimuone baba yake usingizini, ndipo alipomuandikia kombe la kuwa kila akimwita amfuate.
“Kwa iyo kuanzia hapo kumbe yule ndungu yangu hakuwa na akili, kila akiitwa na mwalimu wake nakwenda na ndipo akampa ujauzito”, anahadithia dada huyo.
Kama sio muhali mwalimu huyo asingeendelea kuwabaka watoto, kwani dawa yake ingekuwa kila anapokwenda kwa ajili ya kufundisha afukuzwe.
Baba mmoja, mkaazi wa Madungu Chake Chake, ambae mtoto wake wa miaka mitano alibakwa, anasema iwapo jamii haitaondosha muhali udhalilishaji hautaondoka na wataendelea kupiga kelele tu.
“Ikiwa hatutakuwa na muhali juu ya hili, tutafanikiwa kudhibiti vitendo vya udhalilishaji kwa sababu tutazifuatilia kesi zetu na
kuzisimamia”, aliongeza.
Mtoto wake alipofanyiwa ukatili alikusudia kumuua
mtuhumiwa, lakini watoto walimnasihi asifanye hivyo na ndipo alipokimbilia kituo cha Polisi kuripoti.
Hata hivyo anaeleza kwamba, hatokubali kuona mtuhumiwa anaachiwa huru kwa sababu ameshamuharibia mtoto wake maisha.
BAADHI YA WADAU WANAOPINGA UDHALILISHAJI
Mgeni Kombo Khamis ambae ni Mratibu kutoka Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) anasema, ili kuweza kudhibiti janga hilo na watoto kubaki salama, ipo haja kwa jamii kuondoa muhali na kuwa mstari wa mbele kufuatilia kesi za udhalilishaji.
“Jambo jengine ni kwa vyombo vya Sheria vichukue hatua kali kwa watendaji wa makosa, hayo tukiyafuata tutaweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti”, anafahamisha.
Asya Amour Abrahaman kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kiislam Wanawake Wete, anasema mambo yanayochangia kuongezeka udhalilishaji ni jamii kutofuatilia kesi kwenye vyombo vya Sheria pamoja na mahakama kutoa maamuzi yasiyo sahihi.
“Jamii huwa haina tabia ya kufuatilia kesi zao hivyo huvipa mwanya baadhi ya vyombo vya sheria kufanya manyago wanayotaka, maana wakati mwengine utasikia mtuhumiwa kaachwa huru kwa sababu hata isiyo ya msingi”, anasema.
Mwaka jana Jumuiya hiyo imepokea matukio 15 ya udhalilishaji, ambapo nyengine zimeshapatiwa hukumu na nyengine zinaendelea kusikilizwa.
Mratibu wa Jumuiya ya Tumaini Jipya (TUJIPE) Tatu Abdalla Mselem anaeleza, pamoja na kujitahidi kutoa elimu kupitia shehia lakini wamegundua kuwa bado jamii haijaondokana na rushwa muhali.
“Tunaelimisha lakini tunakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwepo rushwa muhali, jamii kutokuwa na uelewa wa kutosha na kuwepo na ushirikiano mdogo katika kumaliza udhalilishaji wa watoto”, anaeleza.
Anasema, mpango wao wa mwaka huu ni kuendelea kutoa elimu ili kuhakikisha wananchi wanapata uelewa na kuunguna pamoja kupiga vita janga hilo linaloiathiri jamii.
Mratibu huyo mwaka uliopita Jumuiya hiyo imepokea kesi kumi (10) za udhalilishaji.
Kituo cha huduma za Sheria Pemba kimesema, wataendelea kutoa elimu kwa jamii, ili ione umuhimu wa kutoa ushahidi mahakamani, kwani ikiwa hakuna ushahidi mahakama haiwezi kumtia hatiani mtendaji wa kosa.
“Hao ambao hawafiki mahakamani kutoa ushahidi, ama wanasema uongo, au wanakuwa kigeugeu, ni kwamba wamegubikwa na muhali na wengine hawajafikiwa na elimu”, kinaeleza kituo.
Kituo cha huduma za sheria Pemba mwaka jana kilipokea kesi 50, ambazo ni kubaka 20, shambulio la aibu sita (6), kutorosha 14, kulawiti tisa (9) na udhalilishaji mkubwa moja (1).
Kesi sita (6) kati ya hizo zimefutwa na 44 zipo mahakamani katika hatua ya kusikilizwa.
Kilisisitiza sheria kufanyiwa marekebisho sheria zinazosimamia masuala ya udhalilishaji ikiwemo sheria ya mtoto.
VYOMBO VYA SHERIA
Fakih Mohamed Yussuf ambae ambae ni Mratibu wa Dwati la Wanawake na Watoto Mkoa wa Kaskazini Pemba wana programu maalumu ya kuelimisha jamii kwa kushirikiana na wadau wengine, ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa kutosha.
“Baadhi wazazi wanakimbilia kituo cha Polisi wakati mtoto anapofanyiwa udhalilishaji, lakini wakirudi tu kwenye jamii wanabadilika, kwani wanakwenda kufanya suluhu.
Wanapowaita tena wazazi wanabadilisha ushahidi ama wanang’ang’ania kesi hizo zifutwe, hivyo inawakwaza katika kumaliza janga hilo.
Tangu Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk; Hussein Mwinye atoe agizo, Jeshi hilo li mepokea kesi 38, 11 zipo mahakamani, 21 zinaendelea na upelelezi na kesi moja (1) imefungwa kutokana na mashahidi kukataa kutoa ushirikiano.
Hakimu ya Mahakama ya Mkoa Wete Abdalla Yahya Shamhun aneleza kuwa tangu ianze mahamahama maalumu wamepokea kesi 11 za udhalilishaji ambazo zinaendelea kusikilizwa.
“Hakuna muda maalumu katika kutoa hukumu, inategemea na upatikanaji wa mashahidi, hivyo inapokaa muda mrefu huwa kila wakiitwa mashahidi hawaji”, anafafanua.
Mwanasheria dhamana kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Mkoa wa Kaskazini Pemba Ali Haidar anasema, katika kuhakikisha wanajitosheleza kiuchunguzi kwenye kesi za udhalilishaji, wamejipanga kutoa mafunzo ya mbinu bora za kiupelelezi kwa maafisa upelelezi.
“Wakati mwengine mtuhumiwa anaachiwa huru kutokana na utofauti kwenye muda baina ya kwenye hati ya mashitaka muhanga, hivyo kasoro hizi ndogo ndogo tunataka tuziondoe, ili ushahidi uwe imara”, anasema.
Wataisaidia mahakama maalumu iliyoanzishwa kuendelea kusisitiza kufuatwa kwa Sheria zilizopo na kuendeleza ushirikiano katika utendaji wa kazi zao na kueleza kuwa wameshatenga wanasheria nane (8) ambao wataendesha kesi za udhalilishaji.
Fat-hiya Mussa Said ambae ni mratibu wa TAMWA Pemba anafahamisha kuwa, muhali bado ni tatizo sugu katika jamii, hivyo juhudi za makusudi zinahitajika kuondosha ili kudhibiti udhalilishaji.
Kuanzia Januari mwaka 2019 hadi Disemba mwaka 2020 Jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba limepokea kesi 281 za udhalilishaji.