NA ABDI SULEIMAN.
MWENGE wa Uhuru umewasili Kisiwani Pemba leo, ukitokea Mkoa wa Mjini Magharibi na kukabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba na kuanza kukimbizwa katika Wilaya ya Mkoani.
Makabidhiano hayo yaliyofanyika katika uwanja wa ndege wa Karume Pemba, huku Viongozi mbali mbali wa serikali wakihudhuria mapokezi hayo, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Kusini na Kaskazini.
Akikabidhi mwenge huo pamoja na Wakimbizaji wake Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrissa Kitwana Mustafa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba mheshimiwa Mattar Zahor Massoud, alisema Mwenge wa uhuru kitaifa 2021 katika mkoa wake umeweza kuzindua, kukagua, kutembelea miradi 21 ya maendeleo.
Alisema katika kufikia adhma ya mwenge huo 2021 mkoa huo umepenga kukusanya jumla ya shilingi 13,000,000/=, ambapo shilingi 9,950,000/=zimekusanywa sawa na asilimia 77, fedha hizo zimechangia jumla ya miradi 13 ya maendeleo.
Akizungumzia ujumbe wa mbenge huo mwaka 2021, alisema TEHAMA kwa maendeleo ya taifa na unalenga kuwakumbusha wananchi kutumia TEHAMA kwa usahihi chini ya kauli isemayo “TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu itumike kwa usahihi na uwajibikaji”.
Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2021 Luteni Josephine Paul Mwambashi, aliutaka uongozi wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuyafanyia kazi mapendekezo walioyataoa ili kuweza kufikia maendeleo.
Aidha akiongozi huyo aliwataka wananchi wa mkoa wa Kusini Pemba, kushirikiana katika kipindi hiki ambacho Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika mkoa huo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema hana shaka yoyote katika Ukimbizaji wa mwenge huo, kwani Mkoa wake umejipanga vyema kufanikisha zoezi hilo.
Aidha mkuu huyo wa Mkoa aliweza kuukabidhi mwenge huo kwa ,Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Issa Juma Ali, kwa kuanza mbio zake kwa kukagua, kufungua na kuweka jiwe la msingi Miradi tisa ya maendeleo.
Miradi ambayo inatarajiwa kufunguliwa, kukaguliwa na kutembelewa na mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, kwa Wilaya hiyo ni Maji safi na salama, miradi itakayokaguliwa ni mazingira, ufugaji mseto, kilimo cha tangawizi, kalaviti, nyumba bora na ujenzi wa kituo cha afya, kwa upande wa mradi utakaowekewa jiwe la msingi ni ujenzi wa banda la skuli mkanyageni na kituo cha cha Tehama kufungua mafunzo, yenye thamani ya shilingi Milioni 240,926,047/=,.