RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wale wote waliohusika na kasoro zilitolewa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ili kasoro hizo zisije kurudiwa tena.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo mara baada ya kukabidhiwa Ripoti za Hesabu za Serikali kwa mwaka 2019 -2020, huko katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, hafla ambayo imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa fedha nyingi za Serikali zinapotea kwa kiasi kikubwa na iwapo hali hiyo itaendelea maendeleo hayatoweza kupatikana katika kuijenga nchi.
Alisema kuwa lengo na madhumuni ya kupokea ripoti hiyo hadharani ni katika suala zima la kuhimiza uwajibikaji na utawala bora kwani ni lazima Serikali iwe wazi na kujulikana changamoto ndipo itakapowezekana kukabiliana na matatizo kama hayo.
Aliongeza kwamba katika Taasisi za ukusanyaji wa fedha bado kuna upotevu wa udhaifu wa mifumo na hata dhamira ovu ya watendaji katika ukusanyaji wa fedha za Serikali.
Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba mbali ya suala la ukusanyaji pia katika Taasisi hizo kunaonekana kwamba kuna udhaifu wa matumizi ambalo nalo limepelekea upotevu mkubwa wa fedha za Serikali ambapo hata kile kidogo kinachokusanywa hakitumiki vizuri.
Alisema kuwa hali hiyo ni vyema ikawafanya wote wakatafakari na kufanya ama kuchukua hatua za msingi za kudhibiti hali hiyo.
Hivyo, Dk. Mwinyi alisema kuwa haiwezekani ionekane kumepokewa tu taarifa hiyo bali ni lazima hatua zinazohitajika zikachukuliwa hasa ikizingatiwa kwamba fedha hizo zinahitajika katika kuimarisha miradi ya maendeleo.
Alisema kuwa ni lazima ripoti hiyo ikafanyiwa kazi ili ripoti ya mwakani kusije kujitokeza kasoro kama hizo na endapo zikiwepo itaonesha wazi kwamba kumeshindwa kutekeleza wajibu na kwa upande wake alisema kwamba hatokubali kuonekana kashindwa kutekeleza wajibu wake.
Alisema kwamba viongozi hao wote waliokuwepo katika hafla hiyo wanahusika na kusema kwamba kwamba ni uwajibikaji ni lazima uanze juu ili kwenda mpaka chini na kusema kwamba hatofurahi kusikia mtu kafanya makosa na kiongozi kushindwa kumuwajibisha.
“Nitafurahi kusikia fulani nimemfukuza au nimemsimamisha ama ninakuletea Rais uchukue hatua kwa sababu ya hili hili lakini sitokubali kusikia fulani kafanya makosa yuko chini ya Taasisi yako hata kusema hujasema huwezi kuepuka lawama katika hili, sasa leo tunapokea ripoti ambayo kwa kiwango kikubwa wengi wetu tumeyakuta lakini nasema kwa siku za usoni tutawajibika moja kwa moja na kitakachosemwa hapa” Alisema Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kusikitishwa kwake pale watendaji wa Serikali wanaposhindwa kutoa ushirikiano kwa Wakaguzi wa Serikali na kusema kwamba jambo hilo ni kukengeuka Katiba ya Zanzibar.
Kutokana na jambo hilo kutokea wakati Mkaguzi Mkuu akifanya kazi zake na kuwa miongoni mwa changamoto alizozieleza, Rais Dk. Mwinyi alimtaka Mkaguzi huyo kuendelea na zoezi hilo na kuzitaka Taasisi zote zilizofanya hivyo zitoe ushirikiano na wahuisika wote washirikishwe hata wale waliokuwa hawapo ofisini kwa waliokwua likizo ama kustaafu.
Alimtaka Mkaguzi Mkuu wa Setikali kazi hizo ianze kesho (Jumaatatu 24 May 2021) na kusisitiza kwamba zoezi hilo ni lazima likamilike.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo kinachofuata ni kupelekwa Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kutolewa maoni na kutumia fursa hiyo kuwakabidhi ripoti hiyo viongozi kadhaa akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alimkabidhi ripoti hiyo Waziri wa Nchi Afisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera,Uratibu na Baraza la Wakilishi Dk. Khalid Salum Mohammed, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said
Mapema akitoa maelezo ya ripoti hiyo Kaimu Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Zanzibar Dk.Othman Abbas Ali alisema kuwa amekabidhi ripoti hiyo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Ibara ya 112 pamoja na sheria nyengine zinazompasa kufanya hivyo.
Alisema kuwa ripoti hiyo yenye vitabu sita, ambavyo vina jumla ya tripoti 169 ambayo inaishia kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30 mwaka 2020 ambapo ripoti hiyo imejikita katika Kitabu cha ripoti ya Ukaguzi ya Serikali Kuu, Kitabu cha ripoti ya Ukaguzi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Kitabu cha ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma na Taasisi zinazojitegemea, Kitabu cha Ukaguzi cha Mfuko wa Maendeleo ya Majimbo, Kitabu cha Ukaguzi wa Mifumo ya TEHAMA, Kitabu cha ripoti ya Ukaguzi Maalum unaohusu utekelezaji wa maagizo ya Rais wakati wa kuwaapisha Viongozi Wakuu.
Aidha, Dk. Ali alisema kuwa kwa mwaka wa fedha jumla ya Hati 102 za Ukaguzi zimetolewa na Mkaguzi huyo ambapo hati zinazoridhisha ni 76 sawa na asilimia 74.51, Hati zisizoridhisha ni 12 sawa na asilimia 11.76, Hati zenye shaka ni 12 sawa na asilimia 11.76 na Hati mbaya ni 2 sawa na asilimia 1.84.
Pia, Dk. Ali alitoa wito kwa Menejimenti, Bodi za Wakurugenzi na Maafisa Wahasibu wa Taasisi za Serikali kuhakikisha wanatimiza matakwa ya Kikatiba na Kisheria kwa kuhakikisha kwamba wanawasilisha hesabu kila mwaka kwa ajili ya kutolewa maoni ya kiukaguzi na wale wanaotakiwa kuzirekebisha taarifa zao basi wazipeleke ndani ya muda ili aweze kuzikagua na kuzitolea maoni kwa lengo la kutimiza matakwa ya Ibara ya 112 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Aliongeza kuwa ukaguzi alioufanya umebaini katika Hesabu za Mfuko Mkuu wa Serikali umebaini kuwepo kwa baadhi ya mapungufu katika uandaaji na uwasilishwaji wa hesabu jumuishi kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30,2020.
Sambamba na hayo, Dk. Ali alisema kuwa katika ukaguzi uliofanyika kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa kupata majibu ya baadhi ya ripoti za ukaguzi kutoka kwa Taasisi zilizokaguliwa jambo ambalo linapelekea kuzisubiria Taasisi kwa ajili ya ukamilishaji wa uandishi wa ripoti kuu ya ukaguzi.
Pia, aliitaja changamoto ya kutokujibiwa kwa hoja za ukaguzi kwa baadhi ya Taasisi zilizokaguliwa na kupelekea dosari zilizobainika katika ukaguzi kuchukuliwa moja kwa moja kama ni hoja ya ukaguzi na kuingizwa katika kitabu cha ripoti kuu ya ukaguzi, Kukosekana kwa baadhi ya taarifa zakifedha kutoka Idara ya Hazina kwa lengo la kutathmini usahihi na ukamilifu wa ripoti za kifedha zinazozalishwa na mfumo wa IFMIS ili kuweza kujiridhisha kama mfumo unaisaidia Serikali katika kuhakikisha uwajibikaji na uwazi unakuwepo katika ukusanyaji wa mapato, matumizi ya fedha.
Dk. Ali alieleza Changamoto ya kutokuwiana kwa taarifa za fedha za Mfumo Mkuu wa Usimamizi wa Fedha za Serikali (IFMIS) na taarifa za fedha zinazoandaliwa na Mawizara pamoja na Taasisi mbalimbali za Serikali ambazo taarifa hizo huwasilishwa kwa ajili ya ukaguzi.
Sambamba na hayo, aliitaja changamoto ya kukosekana kwa muongozo wa viwango vya uandaaji na ufungaji wa taarifa za hesabu za mwisho mwa mwaka vinavyoandaliwa na kutolewa na Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali Zanzibar jambo ambalo linapelekea kwa baadhi ya Mashirika na Mamlaka mbalimbali za Serikali kufunga hesabu zao bila ya kuzingatia viwango vya ufungaji wa hesabu kitaifa na Kimataifa na kupelekea hesabu hizo kutokuonesha sura sahihi na halisi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar