NA ABDI SULEIMAN.
KATIBU mkuu wa Jumuiya ya umoja wa wazazi CCM taifa Mwalimu Queen Mlozi, amewataka akimama Kisiwani Pemba kujiandaa na mapema kuweza kujitokeza kugombani nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi wa chama mwaka huu.
Katibu huyo alisema iwapo wanawake watajitokeza kwa wingi katika nafasi hizo, basi itakua ni jambo jema na kuonenaka kuwa wanawake wamekuwa imara katika nafasi hizo.
Hayo aliyaeleza huko makangale alipokua akizungumza na akinamama mbali mbali, katika ziara ya uhamasishaji wa kujitokeza kwao kugomea nafasi mbali mbali za uongozi.
Alisema wanawake wamekuwa ni waaminifu wakubwa pale wanapopatiwa nafasi hizo, hivo ni vizuri kujitokeza kushika nafasi hizo hata nafasi ambazo wanaume walikuwa wakizikamata.
“Tuangalie jamani hata rais wetu wa nchi Mama Samia ni mwanamke, tayari amekuwa akiwaongoza wanaume wengi katika nafasi hizo”alisema.
Akizungumzia juu ya suala la elimu, katibu huyo aliwataka akinamama kuwa mstari wa mbele katika kushajihisha watoto kusoma masomo ya sayansi, ili kuweza kuwa na wataalamu wengi wa kike na watakaoweza kuwasaidia wanawake wenzao.
Kwaupande wake Mbunge wa Viti maalumu wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, aliwahimiza akinamama kuhakikisha wanaondokana na mfumo dume kuwa wanaume ndio wenye nafasi ya kugombania uongozi.
Aidha mbunge huyo alisema wakati umefika kwa wanawake kuonyesha ujasiri wao, katika kugombani nafasi hizo ili kuwezxa kufikia malengo ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia.
“Tukiwa wengi katika nafasi za uongozi basi hata wanaume watajua kama sasa wanawake nao wanahitaji nafasi hizo, hii itaondosha dhana kuwa ni wanaume tu ndio wenye dhamana hiyo”alisema.
Hata hivyo Mbunge huyo alisihi wanawake hao kuwa mstari wambele katika kukemea vitendo vya unyanyasaji na udhalilishaji wanaofanyia watoto, kwani vimekua vikiwaathiri katika maisha yao.
Hivi karibuni afisa Mawasiliano kutoka chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA)Ofisi ya Pemba, Gasper Charles aliwataka waandishi wa habari kisiwani humo, kuitumia mitandao ya kijamii katika kuwahamasisha wanawake kungombea nafasi za uongozi.
Alifahamisha kuwa TAMWA kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi na demekrasia, utaendelea kuwapatia waandishi wa habari mafunzo mbali mbali ikiwemo matumizi ya mitandao.
Naye mwandishi wa habari mwandamizi Pemba, Ali Mbarouk Omar aliwataka waandishi hao kuwa wabunifu katika kutumia mitandao ya kijamii, kwa kuandisha habari au taarifa mbali mbali zinazowahusu wanawake.
Alisema uwekaji wa taarifa katika mitandao hiyo inakuwa ni rahisi kupata wasomaji wengi zaidi kwa wakati mmoja, kuliko vyombo nyengine vya habari.
Aidha alisema waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuwafikia wanawake, hususana vijini ambako ndiko inakoonekana uwelewa wa baadhi ya mambo kwa wanawake umekua mdogo.
Mafunzo hayo yametolewa kupitia mradi wa kuwajengea uwezo wanawake kudai haki zao za kisiasa na uongozi ambao ni wa miaka minne unaendesjwa kwa pamoja Kati ya TAMWA, ZAFELA, PEGAO na unatarajiwa kukamilika mwaka 2024.
MWISHO.