Tuesday, November 26

Uongozi wa ZSSF Watakiwa Kutambua Madhumuni ya Mfuko Huo ni Kuwasaidia Wastaafu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) akisisitiza jambo wakati alipokuwa na mazungumzo na Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar ZSSF alipokutanana nao leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kutambua kwamba madhumuni ya mfuko huo ni kuwasadia wastaafu ili waweze kuishi vizuri baada ya ustaafu wao.

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) ukiongozwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko huo Nassor Shaaban Ameir.

Katika maelezo yake alisema kwamba kuna utofauti mkubwa wa wastaafu wa hapa nchini na nchi nyengine duniani ambapo kwa upande wa nchi hizo wastaafu baada ya kustaafu kazi ndipo huishi vizuri zaidi kuliko wakiwa kazini.

“Sehemu nyingi za utalii huko nje ya nchi utavikuta vibibi na vibabu wazee, wazee ukiuliza unaambiwa hawa wakati huu ndio wakati wao wa kustarehe, wanalipwa vizuri kwa sababu waliwekeza muda wote wa kazi jambo ambalo ni tofauti na hapa kwetu na mimi nataka hali hiyo ibadilike isiwe kama tulivyo hivi sasa”,alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa watu wamekuwa wakitoa fedha zao na kuziweka katika Mfuko wa ZSSF katika kipindi  chao chote cha kazi ambapo fedha hizo zimekuwa zikiekezwa kwa miaka mingi hivyo, wamekuwa na matarajio makubwa kwamba watapata faida kubwabaada ya kustaafu lakini kinachotoka ni tofauti.

Alisema kwamba moja ya dhamana kubwa uliopewa Mfuko huo wa ZSSF ni kuhakikisha unawekeza vizuri na unatapa faida nzuri ili kuhakikisha wastaafu wanaishi vizuri na sio kupigiwa hesabu kwa Walichochangia wakati wako kazini.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mstaafu wakati yuko kazini amekuwa akichangia hadi anafika muda wa kustaafu wa miaka 60 anakuwa tayari ameshatengeneza faida na kueleza kwamba hakuna sababu ya mstaafu kutopata maslahi mazuri.

“Yote fanyeni lakini kinachotakiwa mwisho wa siku ni kuhakikisha watu waliochangia fedha zao wakistaafu wanalipwa vizuri”, alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba  ni vyema Mfuko huo ukawa na dhamana ya fedha za watu kwa kuekezwa vizuri ili ziweze kupata faida ya miaka yote ya wastaafu waliyoweka fedha zao.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema  kuwa  moja ya njia ya kuwasaidia wasfatu ni kuwapatia makaazi kwani wafanyakazi wa Zanzibar hawana mategemeo ya kupata makaazi mazuri kwa sababu hawana uwezo hivyo, ilikuwa  ni wajibu wa Mfuko huo kujenga nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wateja wao wa Mfuko huo ambao ni wanyonge.

Aliongeza kuwa mafao yanayotokana na ZSSF bado hayajawafurahisha wawekaji na kusisitiza kwamba Mfuko huo ni vyema ukaliangalia suala hilo hasa ikizingatiwa kwamba watu wanawekeza fedha zao katika Mfuko huo ili waje kupata faida.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa utaratibu wa Kikokotoa isiwe sababu ya kutowalipa  wastaafu kima cha fedha kinachostahiki na kueleza kuwa wastaafu ni lazima walipwe vizuri kwani ndio lengo la Mfuko huo kwani wengine wameanza kuweka fedha zao tokea wanaajiriwa wakitokea skuli hadi kustaafu kwao wakiwa na miaka 60.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi  aliutaka uongozi wa Mfuko huo kuwa makini zaidi katika suala zima la uwekezaji wanaoufanya kwa kuhakikisha kwamba miradi wanayowekeza inakuwa na faida kwa Mfuko huo.

Pia, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mfuko huo kusimamia vyema uanzishwaji wa  Mfuko wa Bima ya Afya.

Mapema Uongozi huo ulieleza kwamba lengo la Mfuko huo ni kuwahifadhi wanachama wake wanapopatwa na majanga ambayo husitisha au kupunguza kipato kutokana na sababu mbali mbali kama vile uzee, ulemavu, maradhi, kifo, uzazi, pamoja na majanga mengineyo yanayoidhinishwa na Bodi ya Wadhamini wa Mfuko huo.

Aidha, uongozi huo ulieleza azma ya kukusanya fedha kwa  njia za elektroniki katika viwanja vyake vya kufurahishia watoto Unguja na Pemba ili kuweza kukusanya vyema mapato yake.

Uongozi huo ulieleza kwamba pamoja na kazi za kawaida ambazo Mfuko unatekeleza, pia, unaendelea kufuatilia kwa karibu maagizo mbali mbali anayoyatoa Rais ambayo yanagusa shughuli za uendeshaji wa Mfuko.

Pia, uongozi huo ulieleza azma ya kuangalia uwezekano wa kuanzisha Mafao mapya kama vile mafao ya matibabu na kadhalika sambamba na kuanzisha ujenzi wa nyumba za bei nafuu katika maeneo tofauti kwa kushirikiana na Serikali kulingana na upatikanaji wa ardhi.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar