Monday, November 25

Kucheleweshwa kwa mirathi ni moja ya tatizo ambalo linapelekea migogoro ya ardhi pamoja na kukosa haki ya kumiliki.

NA SAID ABRAHMAN.

MASHEKHE na Maimamu wa miskiti mbali mbali ya Wilaya ya Micheweni, wamesema kuwa tatizo kubwa ambalo linapelekea migogoro ya ardhi pamoja na kukosa haki ya kumiliki wa ardhi ni kutokana na kucheleweshwa kwa mirathi.

Aidha walisema tatizo jengine ni kutozwa kwa ada kubwa wakati wanapotaka kusajili ardhi zao jambo ambalo pia linasababisha kupelekea wananchi kushindwa kumiliki ardhi.

Mashekhe na Maimamu waliyaeleza hayo katika ukumbi wa Shaame Mata Micheweni, wakati wa semina ya siku moja juu ya suala zima la umiliki wa ardhi kwa wanawake, iliyoandaliwa na jumuia ya Kupunguza Umaskini na kuboresha hali za wananchi Pemba(KUKHAWA).

Walisema kuwa endapo mirathi itaweza kuchukuwa nafasi yake, migogoro mingi ya ardhi itaweza kuondoka pamoja kuwanyima haki wanawake katika kuweza kumiliki ardhi.

Hata hivyo Mashekhe hao wameiomba Serikali, kuandaa kamati maalum kwa kila Shehia au Majimboni, itakayoshughulikia mirathi baada ya mwanashehia kufariki.

Sheikh Rashid Habib Rashid wa Msikiti wa Ijumaa Makangale, alisema kuwa endapo miongozo ya Mwenyezi Mungu itaweza kufuatwa, hakuna shaka mambo mbali mbali yataweza kuondoka katika jamii, lakini bado waislamu wameacha miongozo ya Allah na kujichukulia maamuzi wanayojua wao.

“Mwanamme analo fungu kwa wazazi wake kwa yale ambayo wameyaacha, lakini pia na wanawake nao Wana fungu kwa yale ambayo wameyaacha wazazi wao,”alisema.

Sheikh Rashid alieleza kuwa Mtume Muhammad (SAW), aliwataka waislamu endapo atafariki miongoni mwa jamaa zenu jambo la kwanza ni kulipwa kwa madeni yake, kufuata wasia wa Marehemu kama ameuwacha lakini pia kufanywa taratibu za kurithi mali ambazo marehemu ameziwacha.

Nae Sheikh Habib Said Rashid (Konde), alisema ucheleweshwaji wa mirathi bado ni tatizo kubwa katika jamii nyingi, tatizo hilo kama halitosimamiwa ipasavyo halitaondoka milele.

“Mimi binafsi kuna familia ambazo ninazifahamu tokea miaka ya 1990, walipofariki wazazi wao hawajarithi na jengine ambalo lipo wanawake, wamekuwa wakikosa haki zao ni kurithi kwa kupata ushauri ambao usio sahihi na wanaume, wakajichukulia Mali na wanawake wakaachwa patupu,”alifahamisha.

Aidha Sheikh Haroub aliwataka Masheikh na Maimamu hao, kupambana na suala la mirathi kwa kuandaa hutuba Maalum katika miskiti yao na kuacha kuzungumzia suala la ndoa tu.

Nae Afisa kutoka Kamisheni ya Wakfu na maliamana Pemba Abdalla Khamis Shaame, alisema chanzo kikubwa kinachopelekea migogoro ya ardhi katika jamii ni ucheleweshwaji wa mirathi, wanajamii wengi wanaogopa kulizungumza hilo, licha ya kuwa mirathi ni haki ya warithi au mirathi ni lazima afanyiwe yule maiti, aliyekwisha tangulia mbele ya haki tena kwa uharaka zaidi.

Alisema Kamisheni ya Wakfu na maliamana imepewa jukumu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika kusimamia mirathi ila bado wananchi wamekuwa na elimu ndogo juu ya Ofisi hiyo.

Aidha aliwatoa hofu wananchi wote kuwa gharama ambazo zinatolewa na Kamisheni hiyo ni ndogo, hivyo aliwasisitiza Mashekhe hao kuwaelimisha jamii ili waweze kufika katika Ofisini kwao.

Akifungua semina hiyo Mkurugenzi wa KUKHAWA Hafidh Abdi Said, alisema Zanzibar wanawake ni asilimia 51%, ambapo wanaomiliki ardhi ni asilimia 20% na hawa ni wale wanawake ambao kidogo wamekuwa wajanja.

Aidha Hafidh alisema tatizo la wanawake kutomiliki ardhi ni kubwa sana, mbapo yote hayo yanasababishwa na mirathi hivyo ni wajibu kwa wanawake kujitambua kuwa umiliki wa mali ni haki yao.

Nae Haji Mohammed Haji kutoka jumuia ya KUKHAWA, alisema kuwa tokea kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 2016, jumuiya yao imegundua changamoto nyingi ambazo zinamfanya mwanamke ashindwe kumiliki ardhi.

Aidha alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na gharama kubwa ambazo wakati wa kutaka kusajili ardhi, urasimu uliopo kwani wananchi wengi na sio wanawake pekeyao na wanaume pia wanashindwa kufuatilia, kutokana na hali zao za maisha pamoja na kutofanyika kwa mirathi ambapo haifanyiki.

“Mradi huu utawezesha kusaidia upatikanaji wa usajili wa ardhi kwa wanawake lakinj pia utaweza Kupunguza migogoro iliypo ya ardhi,” alisema Haji

Mradi wa kumuwezesha mwanamke kumiliki ardhi unaendeshwa na jumuiya ya KUKHAWA na kufadhiliwa na The foundation for civil society