NA ABDI SULEIMAN.
MRAJISI wa Asasi Zisizo za Kiserikali Zanzibar Ahmed Khalid Abdalla, amewataka wanasheria kuziangalia sheria zinazosimamia ardhi, kama zina mapungufu waishauri serikali ziweze kufanyiwa marekebisho, ili kuondosha migogoro ya ardhi katika jamii.
Alisema iwapo wanasheria wataweza kuzioredhesha na kuonyesha mapungufu ya sheria hizo, na kuziwasilisha katika taasisi husika basi serikali inaweza kuzifanyia marekebisho.
Mrajis huyo alitoa wito huo ukumbi wa KUKHAWA mjini Chake Chake, wakati akifungua kongamano la kijadili changamoto zinazowakabili wanawake katika umiliki wa ardhi, lililowashirikisha wanasheria, wafanyakazi kutoka kamisheni ardhi na Wakfu na Maliamana, lililoandaliwa na jumuiya ya KUKHAWA kupitia mradi wa umiliki wa ardhi kwa wanawake, chini ya ufadhili wa the Foundation for Civil Society.
Alisema eneo muhimu la kuangalia ni kuona, jamii inafahamu kwa kiasi gani sheria za umiliki wa ardhi zinasemaje, ili wadai haki zao kwa kufuata taratibu zinazokubalika, hasa kwa wanawake ambao bado hawajaichangamkia fursa hiyo.
“Tuna migogoro mingi ya ardhi Zanzibar, wanasheria kuangalia wapi tatizo lipo kisheria na kisera, ili tuweze kupunguza migogoro hiyo na jamii kufahamu taratibu na sheria za ardhi”alisema.
“Zaid tuangalie taratibu za kuelimisha jamii, kwa namna gani tunaweza kusaidia wanwwake kumiliki ardhi, NGOs zinajitolea kufanya kazi zao kwa Pemba zaidi katika masuala ya ushauri na utetezi”alisema.
Aidha alisema serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa NGOs, ikiwa na lengo la kuondosha changamoto kwa wananchi, kwani baadhi ya migogoro ya ardhi inasababishwa na mabavu ya mtu.
Hata hivyo aliwataka wanasheria, kutambua kua wao ni watu muhimu sana katika kusukuma mbele maendeleo kwa jamii, huku ofisi ya Mrajis ikiendelea kusajili NGOs ambazo zinafuata mila, silka na desturi za kizanzibari.
Kwa upande wake mratib wa mradi huo Zulekha Maulid Kheir, alisema pemba suala la umiliki wa ardhi kwa wanawake ni dogo sana, kutokana na changamoto wanazokumbana nao, ikiwemo suala ukosefu wa elimu, gharama kubwa za usajili, pamoja na baadhi ya familia kutokufahamiana.
Akichangia katika kongamano hilo, Wakili wakujitegemea Zaharan Mohamed alisema changamoto za umiliki na usajili wa ardhi haziko kwa wanawake tu, bali zipo kwa watu wote tatizo kwa sasa ni upatikanaji wa hati kiliki muda mrefu unachukua.
Alisema tatizo ni elimu ndogo kwa wananchi juu ya suala la usajili na utambuzi wa ardhi, kwa wanawake ikizingatiwa gharama ni kubwa.
Massoud Ali Massoud kutoka Wakfu na Mali amana Pemba, alisema mila na tamaduni kwa baadhi ya familia hurudisha nyuma na kupelekea wanawake kukosa haki zao.