Thursday, January 16

VIDEO: Ushirikiano wa pamoja kati ya TRA, masheha na madiwani utasaida kuifikia jamii katika kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi.

 

NA KHADIJA KOMBO-PEMBA.

Afisa mdhamini mamlaka ya mapato Tanzania  kwa upande wa Pemba  Habib Saleh Sultan  amesema ushirikiano wa pamoja kati ya TRA  masheha na madiwani unahitajika  katika kuifikia jamii  kwa lengo la  kutoa elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa wananchi.

Afisa mdhamini  huyo amesema hayo wakati alipokuwa  akifungua mkutano siku moja  kwa madiwani na masheha   katika  kuwajenga uwelewa juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari huko katika ukumbi wa Baraza la mji Chake Chake..

Amesema  tegemeo kubwa la  mapato  ya taifa  ni  fedha zitokanazo na kodi kwa wananchi hivyo endapo jamii itapata uwelewa juu ya   umuhimu wa ulipaji wa kodi kwa hiari   kutasaidia kutimiza malengo ya serikali katika kuwaletea  huduma bora wananchi wake na kupiga hatua za maendeleo kwa haraka.

Akifafanua juu ya mamlaka za ulipaji wa kodi kwa upande wa TRA na ZRB  Afisa elimu kwa walipa kodi  Abdalla Seif amesema vyombo hivyo vya ukusanyaji wa kodi nchini vipo kwa mujibu wa  sheria na katiba ya nchi.

Akitoa mada katika mkutano huo Afisa elimu na huduma kwa walipa kodi TRA Zanzibar Dr Shuweikha salim khalfan amesema  ili Serikali  iweze kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa jamii  hutumia fedha  zitokanazo na kodi za wananchi, hivyo   jamii haina budi kufahamu   faida za kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi .

Nao washiriki wa mkutano huo wamesema watahakikisha elimu waliopewa wanaifikisha kwa jamii na kuziomba taasisi zinazosimamia kodi kuhakikisha   wanasimamia vyema kodi hizo ili ziweze kulipwa kwa wakati.

 

KUANGALIA VIDEO BOFYA HAPO CHINI