Monday, November 25

Urasimu bado ni changamoto kwa upatikanaji wa hatimiliki wakati wa kusajili ardhi ofisi husika.

 

NA ABDI SULEIMAN.

WANAWAKE wa Wilaya ya Micheweni wamelalamikia uwepo wa urasimu wa upatikanaji wa hatimiliki, wakati unapokwenda kusajili ardhi katika ofisi husika.

Wanawake hao wamesema urasimu huo unatokana na gharama kubwa ya ufuatiliaji wa huduma hiyo, mwisho wake mtu hukata tama na kusitisha kufuatilia pamoja na watendaji wa taasisi hizo kutokua tayari kuwasaidia wanawake wasionakipato.

Hayo yameelezwa kwenye mkutano wa kuwajengea uwezo wanawake, juu ya masuala ya ardhi mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya KUKHAWA kupitia mradi wa Haki ya umiliki wa ardhi Pemba, chini ya ufadhili wa the Foundation for Civil Society.

Akitowa malalamiko hayo Asma Salim Ali kutoka shehia ya Makangale, alisema urasimu huo unasababisha gharama kubwa ya ufuatiliji wa huduma, hali ambayo inarudisha juhudi za kutafuta umiliki wa mali zao.

Naye Zuwena Haji kutoka shehia ya kiuyu mbuyuni, alisema wanatamani kumilliki ardhi ambazo wamerithi kutoka kwa wazazi wao, lakini kutokana na baadhi ya kaka na ndugu wakiume katika familia zao, wanaikwepa haki hiyo na kuwasababisha wao kukosa umiliki.

 

Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Jumuiya KUKHAWA Hafidhi Abdi Said, alisema katika utekelezaji wa mradi wamegundua kuwa migogoro inayotokea ya ardhi, inasababishwa na

ucheleweshwaji wa ugawaji wa mirathi katika familia.

Hafidhi aliwataka wanawake waliojengewa uwezo juu ya umiliki wa ardhi, kufukikisha elimu hiyo kwa wanawake wengine katika jamii  zao, ili waweze kujuwa haki zao pamoja na kuona wapi wamerlipokosea mpaka kushindwa kusajili mali zao.

 

“Wanawake bado mpo nyuma kumiliki ardhi, kutokana na sababu mbali mbali, hivyo sisi tumeamua kutoa mafunzo haya ya kuwajengea uwezo, ili waweze kuwa wawakilishi wazuri huko mitaani majumbani kwao.

 

“Mnakutana katika hisa au visimani na madukani, mtusaidie ili elimu tuliyowapa iwafikie wananchi tupate kuona mwanamke nae anamiliki ardhi”alisema.

 

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, Afisa kutoka kamisheni ya ardhi Asha Suleiman Said, aliwataka akinamama hao wakati wanapotaka kumiliki mali na waume zao, kuweka kumbukumbu ya maandishi ili inapotokea kutokuelewa iwe ni rahisi mwanamke kupata haki yake.

Alisema ipo haja ya kumilki ardhi kwa kufanya usajili, kutoka kamisheni ya ardhi kupitia majina ya wanawake wenyewe, ili kuondosha usumbufu ambao huenda ukajitokeza endapo hawatozisajili kwa majina yao.

 

“Wapo watu wanamiliki ardhi kwa njia ya mdomo tu, hii yangu nah ii yangu na karatasi ya sheha tu, hapa vizuri kupata taratibu za serikali katika suala la ardhi”alisema.

Hata hivyo mwanasheria Halfan Amour Muhammed, aliwaasa wasimamizi wa familia kutolipuuza suala la mirathi, ili kuwasaidia wanawake kuwa na umilki wa ardhi kwa ajili ya kujikomboa na umaskini.

 

Mirathi ni sheria katika dini ambayo kwa asilimia kubwa wananchi wa zanzibar ni waislam, kwaio wanaume msiwe chanzo cha kupindisha mirathi. Alisema.