Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud, ameyasema hayo wakati akizungumza katika maadhimisho ya pili ya wiki ya msaada wa kisheria yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil kikwajuni mjini Unguja.
Mheshimiwa Othman amesema suala la msaada wa kisheria sio suala la huduma tu za kisheria bali kimataifa limekubalika na kutambulika kuwa ni nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo katika taifa na kupunguza umasikini.
“kuanzisha mfumo rasmi wa msaada wa kisheria nchini ni sehemu ya juhudi ya serikali kutambuwa kuwa Zanzibar inahitaji kuweka mifumo inayoendana na maendeleo ya kidunia katika fani na nyanja zote”. alieleza
Mhe. Othman amesema mbali na Umoja wa mataifa umuhimu wa msaada wa kisheria umetambuliwa pia na maazimio mbali mbali ya nchi za Afrika kwa lengo la kutilia mkazo suala la msaada wa kisheria katika nyanja mbali mbali.
Amesisitiza pia kwa kusema, “sheria ya msaada wa kisheria namba 13 ya mwaka 2018 pamoja na kanuni zake za mwaka 2019 ni mkombozi mkubwa kwa watu wasiokuwa na uwezo wakiwemo wanawake na watoto”.
Hivyo ameisistiza idara hiyo kupitia vizuri miongozo hiyo kwa lengo la kuona msaada wa kisheria unapatikana bila ya matatizo yoyote.
Kwa upande mwengine Mhe. Othman amewahimiza watoa huduma za msaada wa kisheria kuzingatia haki za makundi mbali mbali ya binaadamu pamoja na matatizo mengine yaliyomo katika jami ikiwemo migogoro ya ardhi na unyanyasaji wa kijinsia ili iwe ni kiashiria kikuu cha kupatikana kwa haki katika jamii ya zanzibar.
Sambama na hayo amezipongeza taasisi za serikali na zisizo za serikali kwa juhudi wanazozichukua katika kuwafikia wananchi na kuwafahamisha juu ya upatikanaji wa msaada wa kisheria.
Akitoa maelezo mafupi kuhusu maadhimisho hayo Mkurugenzi wa idara ya msaada kisheria Bi. Hanifa Ramadhan Said amesema Idara imejipanga kuanzisha wasaidizi wa kisheria katika kila wilaya kwa lengo la kuona upatikanaji wa msaada wa kisheria unakuwa mwepesi ili wananchi waweze kupata haki zao.
Ameeleza lengo la kauli mbiu ya mwaka huu ni kuona mwanammke anakomboka kiuchumi na kupata sehemu ya kumuezesha kisheria pamoja na kuona huduma za kisheria zinatolewa maeneo mbali mbali.
Meneja Mkuu wa mradi wa LSF Deogratias Bwire ameahidi kuendelea kutoa mashirikiano kwa idara ya msaada wa kisheria ili kuendeleza kazi za wasaidizi wa kisheria kwa lengo la kuwanufaisha wananchi juu matatizo yanoyohusu sheria.
Tunzo mbali mbali zimetolewa kwa wasaidizi wa sheria hasa kwa waliofanya vizuri katika kesi za udhalilishaji, vyombo vya habari pamoja na waandishi walioshiriki katika kuandikia masuala ya kisheria pamoja na masheha.
kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni msaada wa kisheria ni chachu ya kumuwezesha mwanammke kiuchumi.