Tuesday, November 26

Kwanini wanasema simu ya mpenzi wako sumu?

Wengi wanajutia au hata kufurahia uamuzi wao wa kujikuta wanachungulia ujumbe na mawasiliano ya wenzao katika simu zao za mkononi lakini matokeo yake ni jambo ambalo hawakulipangia.

Ni kifaa kidogo cha mkononi ambacho kilifaa kurahisisha mawasiliano miongoni mwa watu.

Lakini sasa hivi kama kuna njia rahisi ya kuvunjika kwa ndoa ama sababu kubwa ya kuvunja mahusiano, ni simu ya mkononi imetajwa kuwa nambari moja katika orodha hiyo.

Tafiti nyingi zinaonesha kwamba kiwango cha talaka kinaongezeka kila uchao hasa kwa wenye umri wa makamo kwasababu ya simu ya mkononi ikiwa wazi kwamba imegeuka na kuwa sumu katika ndoa badala ya faraja au furaha.

Lakini je uhalisia ukoje?

m

Ndio hali ambayo Bity Wariama amejikuta kwani kila siku anayoishi akijiambia kwamba laiti angelijua basi hangepambana kwa udi na uvumba kuichukua simu ya mume wake na kuangalia jumbe zake!

Aliposoma na kuona wote waliokuwa wakiwasiliana naye hakutaka kupata majibu alifungisha virago vyake na kuondoka.

Tatizo ni kwamba, sasa miezi kadhaa badaye alipofahamu kwamba kuna wanawake wengi waliokuwa wakiwasiliana na mume wake naye hakuwa na haja bali alikuwa tu akiwajibu kwa minajili ya mazungumzo.

Bity alianza kujuta na kufikia wakati huo, mume wake alikuwa ashaamua kwamba Bity ana akili za kitoto na basi akasonga mbele na maisha yake kwa kupata mke mwingine .

Kwanini mwenza wako achunguze simu yako?

Mara nyingi tu anayemchunguza mwenza wake huwa anamuhisi kwamba sio mwaminifu na cha msingi kwake ni kutafuta ushahidi kuthibitisha madai yake.

Lakini mtu anaweza kumchunguza mume, mkewe, au mchumba wake kwa sababu zingine pia:

  • Mwenzi wako anaweza kukuchunguza kama anashuku pengine wewe ni mlevi na umemficha, unatumia dawa za kulevya au kutumia muda wako na watu ambao kwake yeye ni hatari au wenye ushawishi mbaya mfano aliyekuwa mchumba wako.
  • Mwenza wako anaweza pia akakushuku kuwa unatumia pesa nyingi zaidi ya unavyostahili au hata kuiba katika biashara ya familia.
  • Pia mpenzi wako anawe kuwa ana kushuku tu kwamba wewe unakwenda kazini lakini sio kweli.
  • Wakati mwengine huenda ikawa anatafuta ushahidi utakao uwezesha kutalakiana nawe

Pia ni vyema kujua kwamba kuna watu walioumbwa hivyo – yaani uwe unafanya zuri au baya wao watakushuku tu na kufikia kiwango cha kukera.

Ikiwa kuna wakati mume au mke aliwahi kumdanganya mwenza wake katika mahusiano, moja kwa moja itakuwa inaeleweka kuwa na wasiwasi na kuamua kumchunguza kutaka kujua kama ameacha tabia hiyo au anazuga tu.

Aidha, kuna wale ambao huwa wanajihisi kutokuwa salama.

Kila wakati yeye anashuku kuwa mwenza wake sio muaminifu.

Kuna wengine ambao wanapenda kudhibiti wengine.

Wanatambua kwamba mwenye maarifa ndio mwenye nguvu na wao kujua kile unachofanya kwa siri kuna wafanya wahisi kuwa na nguvu na udhibiti wa maisha yako.

Dalili za mtu mwenye kumsababishia mwingine wasiwasi na simu yake.

simu

Lakini yote tisa, kumi kama wewe unamdanganya mwenza wako mfano katika mahusiano au kitu kingine chochote kile, bila shaka kuna yale ambayo ukifanya yatakuwa ni yenye kuzua maswali mengi machoni pa mwenzio.

  • Kunung’unika kama unazungumza na simu
  • Kutotaka simu yako kushikwa na mwingine kabisa
  • Kuitikia tu wakati ukiwa katikati ya mazungumzo na umemuona mwenza wako
  • Kuweka namba ya simu kwenye simu yao
  • Kuwa na matumizi yasioelezeka
  • Kuwa mkali haraka sana unapoombwa na mwenza wako kuwa katika mazungumzo kwasababu ya baadhi ya mambo ambayo hayamuendei sawa
  • Kujitetea katika wakati wa mazungumzo badala ya kuzungumza hoja
  • Na wakati mwingine hata kuwa tayari kuvunja mahusiano baada ya kujua kuwa mwenza wako ametambua ukweli usiotaka kukiri

Ushauri Nasaha

nn

Hadi leo kuna visa vingi ambavyo marafiki, jamaa katika familia na hata viongozi wa kidini wanapatanisha wana ndoa kisa na mkasa, mmoja alichukua simu ya mwenza wake ili kutaja kujua yaliyomo.

Wengi wanashauri kwamba kila mtu azingatie mambo yake na simu yake.

Simu ya mwenzio usiwe na uchu wa kutaka kujua yaliyomo kwa sababu kwa mfano kama mwanamke, ukitaka kupata ushahidi kwamba kuna mwanamke mwingine anawasiliana na mume wako basi utapata.

Sasa kuna wanawake ambao wamejipa busara ya kusema, ugonjwa ambao haunipi uchungu sina haja ya kujua unaitwaje.

Wao hawana haja ya kuziangalia simu za waume zao kwa sababu wanaogopa kupatwa na mshutuko wa moyo bure.

Lakini pia kunao wenye dhana kwamba iwapo katika ndoa hamfichani lolote au hakuna anayefanya mabaya huko nje, hamna haja ya kuificha simu yako ili mwenzako asione jumbe au simu unazopiga.

Sasa kuna tofauti hapo ya jinsi kila walio katika ndoa wanavyoendesha mambo yao hasa kuhusiana na masuala ya simu ya mkononi.

Na hadi kufikia sasa, simu ya mkononi imesalia kuwa fumbo kubwa katika ndoa, je imekuwa neema au laana?