Friday, January 10

TALAKA sio sababu ya kusitisha kuwahudumia watoto.

NA FATMA HAMAD PEMBA.

Familia zimetakiwa kuendeleza kutoa huduma wakati wanapoachana na wanandoa wenzao ili kuwakinga watoto wao na udhalilishaji wa kijinsia.

Wito huo umetolewa na Mohd Adam Makame kadhi kutoka Wilaya ya Mkoani  katika mkutano wa kujadili changamoto za utekelezaji wa majukumu ya ufuatiliaji wa matukio ya udhalilisha kwa wadau wa kupinga udhalilishaji wa Mkoa wa Kusini  huko  ukumbi wa Chama cha Wandishi wa habar Wanawake Tanzania [Tamwa] Chake chake Pemba.

Amesema imebainika kuwa maranyingi Wazazi wanapoachana huwa ni pigo na mama na Watoto, kwani huwelemezewa mzigo wa malezi Mama peke yake jambo linalopelekea kukosa huduma stahiki.

Amesema watoto wengi ambao wazazi wao wameachana hujiingiza katika ajira ikiwemo biashara ili kujitafutia mahitaji yao hali ambayo inasababisha kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

Hivyo amewataka wanandoa kuvumiliana katika ndoa zao ili waweze kuishi na wenza wao na kuwalelea watoto wao katika malezi ya pamoja.

Kwa upande mwengine amekishauri chama cha Wandishi wa habari Wanawake Tanzania tamwa kutoa elimu kwa jamii, pindi mwanamke atakapotelekezwa na mwenza wake na ikawa ni mfanya kazi wa Serikali, kufika Serikalini kutoa malalamiko ili aweze kukatwa mshahara wake na kupewa watoto wake waweze kujihudumia kimaisha.

Mratibu wa chama cha wandishi wa habari wanawake Tanzania [Tamwa] ofisi ya Pemba Fathiya Mussa Said  amewapongeza wadau hao kwa juhudi walionazo  juu ya ufuatiliaji wa karibu kesi za udhalilishaji, huku akiwataka kuendeleza mashirikiano ya pamoja jambo ambalo litapunguza matukio hayo.

Jumla ya kesi 30  za udhalilishaji zimeripotiwa katika vituo vya Polisi vya wilaya ya Mkoani Pemba kuanzia Januari hadi June mwaka huu.