Friday, January 10

Wasisitiza Haja ya Kuendeleza Mashirikiano Yaliopo Kati Pande Mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akifurahia jambo na mgeni wake Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Philip Isdor Mpango alipofika Ikulu Jijinui Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika leo, akiwa Zanzibar kwa ziara ya Kiserikali

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyiamekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philp Esdori Mpango ambapo viongozi hao kwa pamoja walisisitiza haja ya kuendeleza mashirikiano yaliopo kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi hao walifanya mazungumzo hayo leo katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar ambapo mazungumzo hayo pia, yalihudhuriwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Dk. Mpango kuwa anafarajika na juhudi kubwa zinazoendelea za mashirikiano yaliyopo ya Muungano ambapo kila siku zinapokwenda ushirikiano huo unazidi kuimarika.

Rais Dk.Mwinyi alieleza kuwa kutokana na mashirikiano hayo yaliopo yamepelekea changamoto zilizopo zinaweza kushughulikiwa kwa haraka  kwa azma ya kuweza kuijenga nchi katika pande zote mbili za Muungano.

Akieleza kuhusu suala zima la mazingira, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa licha ya kuwa masuala ya Mazingira si ya Muungano lakini jambo hilo lina umuhimu wa kushughulikiwa kwa pamoja kwapande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alieleza kuwa uharibifu wa mazingira si jambo la kubezwa  hasa katika visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo kuna kila sababu ya kuimarisha ushirikiano katika jambo hilo.

Aliongeza kuwa pamekuwepo mashirikiano mazuri kati ya pande mbili hizo hata katika mambo yasiyohusiana na Muungano ambapo hata kwa upande  Wizara za Zanzibar zimeweza kupata fursa ya kujifunza mambo kadhaa kutoka katika upande wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo uzoefu ni mkubwa zaidi.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa mara nyengine tena Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mpango kwa nafasi aliyoshika huku akimpongeza kwa ziara yake anayoifanya ya kuitembelea Unguja na Pemba kwa mara ya kwanza tokea kushika wadhifa huo.

Nae Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philp Esdor Mpango kwa upande wake alitoa shukurani kwa Rais wa Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kwa mapokezi mazuri aliyoyapata tokea alipowasili hapa Zanzibar.

Dk. Mpango alieleza dhamira yake ya kuifanya Zanzibar kuwa ni sehemu yake ya mwanzo ya kufanya ziara rasmi tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo na kueleza jinsi alivyofarajika na mwanzo huo mzuri aliouanza.

Katika maelezo yake, Dk. Mpango alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi pamoja na chama chake cha (CCM), kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar.

Alisema kuwa hatua hiyo imetokana na wananchi kufurahi kwa kiasi kikubwa kwanza kwa kuipokea Ilaini ya CCM, ambapo pia, wameridhishwa na Dira yake wakati wa kampeni za uchaguzi ya kuiletea maendeleo Zanzibar.

Aidha, Makamo wa Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alieleza malengo ya ziara yake fupi ya kuja kumsalimu Rais pamoja na wananchi wa Zanzibar ambapo pia, atapata fursa ya kukutana na watendaji katika taasisi ambazo zinashughulikia masuala ya Muungao.

Alieleza jinsi alivyofursahishwa na hatua  za Rais Dk. Mwinyi katika kukuza uchumi hasa katika kipindi hichi cha uwepo wa maradhi ya COVID 19 bado uchumi wa nchi uko vizuri, wastani wa mfumko wa bei ni mdogo sambamba na kuendeleza vizuri kwa kipato cha wananchi.

Alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza kasi ya uchumi na kutekeleza azma yake ya kusimamia uchumi ambapo maisha ya wananchi yamekuwa yakitegea nguvu za uchumi huo na kueleza kwamba hatua hizo zinatokana na ile azma yake ya kusimamia Mapinduzi ya Uchumihapa Zanzibar.

Aliongeza kuwa hatua za Rais Dk. Mwinyi za kujikita katika uchumi wa buluu ambao unahusisha rasilimali za bahari, uvuvi, ufugaji wa samaki, miundombinu ya bandari, utalii na sekta nyenginezo, zinazonesha imani yake kubwa aliyonayo katika kuiletea maendeleo endelevu Zanzibar.

Dk. Mpango alipongeza hatua za Rais Dk. Mwinyi katika suala zima la utawala boraambao ndio msingi wa maendeleo ambapo amekuwa akipambana na suala zima la rushwa, ufisadi,uzembe kazinisambamba na kuweza kuchukua hatua.

Alisisitiza kwamba Rais Dk. Mwinyi ameweza kufanikiwa katika kuhakikisha matumizi ya fedha za Serikali yanakwenda vizuri na kueleza kwa upande wao wameweza kujifunza kwa juhudi zake hizo huku akieleza jinsi anavyoimarisha huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu, maji safi na salama na sekta nyenginezo pamoja na kutatua changamoto zilzopo katika sekta hizo.

Pia, Dk. Mpango alitioa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa jinsi anavyoendeleza vizuri ushirikianao wa Kimataifa ambapo Washirikia wa Maendeleo wameendelea kuiunga mkono Zanzibar pamoja na  Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi nao wameweza kufarajika na muelekeo wa Rais Dk. Mwinyi.

Alisema kuwa juhudi za makusudi zinaendelea kuchukuliwa katika kuimarisha Muungano na kueleza haja ya kuendelea kuzishughulikia changamoto za Muungano ambapo tayari changamoto kadhaa zimeshapatiwa ufumbuzi na kuahidi katika wakati wa uongozi wake atazishuhulikia zilizobaki na zile zote zitakazoibuka.

“Mheshimiwa Rais kwa kweli nimefarajika hivyo, tumekuja kukutia moyo, kwa kweli tukiangalia kwa mbali tunaona mashua inakwenda upande sahihi katika kuharakisha maendeleo ya wananchi wa Zanzibar”,alisisitiza Dk. Mpango

Pia,Waziri Mpango alieleza hatua za makusudi zinazochukuliwa katika kuhamasisha uekezaji hasa katika sekta ya utalii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wawekezaji  wanaekeza fedha zao hapa nchini.

Akieleza ushirikiano uliopo juu ya mashirikiano na hifadhi ya mazingira Dk. Mpango alieleza haja ya kubadilishana mawazo kwa pande mbili hizo za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika changamoto ya bahari ya kupanda kwa kima cha maji ya bahari iliyopo hivi sasa.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar