Friday, January 10

FAIANALI ZA UMITASHUMTA MITA 200 NA 1500 KUFANYIKA KESHO MTWARA

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Fainali ya mbio za mita 200 na mita 1500 katika mashindano ya UMITASHUMTA kwa wavulana na wasichana inatarajiwa kufanyika kesho katika uwanja wa Chuo cha Ualimu Mtwara.

Sambamba na fainali hiyo ya riadha pia kutafanyika mbio za mita 400 hatua ya nusu fainali kwa wavulana na wasichana na pia mbio za kupokezana kijiti 4 x 400 hatua ya nusu fainali nayo imepangwa kufanyika kesho.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa fainali ya kurusha mkuki, Mratibu Msaidizi wa Kamati ya Riadha ya UMITASHUMTA Taifa Neema Chongolo amesema michezo ya riadha inatarajiwa kuhitimishwa alhamis ambapo washindi wa michezo ya nusu fainali watakimbia hatua ya fainali.

Miongoni mwa michezo iliyochezwa jana, ni mchezo wa kurusha mkuki ambapo kijana Juma Mdawasi kutoka shule ya msingi Midoli wilayani Babati aliweza kushinda kwa upande wa wavulana baada ya kurusha Mkuki umbali wa mita 42 na kuwaacha mbali wanafunzi wenzake.

Kwa upande wa riadha kulifanyika mbio za mita 100 hatua ya nusu fainali kwa wavulana na wasichana, mbio za mita 400 kwa wavulana na wasichana na mbio za kupokezana kijiti 4 x 100 hatua ya mchujo.  

Michezo mingine iliyofanyika jana jioni katika hatua ya robo fainali ni mchezo wa soka wavulana ambapo timu  ya mkoa wa Geita ilipambana na Shinyanga, Dar es salaam ilimenyana na Tanga, Mara dhidi ya Rukwa na Tabora dhidi ya Mtwara.

Kwa upande wa soka maalum wavulana Kilimanjaro walichuana na Kigoma, Dar es salaam dhidi ya Tabora, Mtwara ilipambana na Njombe na Singida dhidi ya Shinyanga.

Katika soka wasichana Tabora ilichuana na Lindi, Dar es salaam dhidi ya Singida, Geita dhidi ya Mara na Mwanza dhidi ya Kagera.

Katika mpira wa wavu Mbeya ilicheza dhidi ya Mwanza, Dar es salaam dhidi ya Katavi, Mtwara dhidi ya Mara na Pwani walicheza na Dodoma.

Kwa mpira wa mikono timu zilizoingia robo fainali kwa wasichana ni Mara, Songwe, Morogoro,Katavi, shinyanga Tanga, Singida na Geita.

Katika mpira wa mikono wavulana, Rukwa ilicheza dhidi ya Mwanza,  Tabora dhidi ya Morogoro, Pwani dhidi Manyara na Tanga dhidi ya Mbeya.

Robo fainali ya Netiboli ilizikutanisha Morogoro dhidi Mwanza, Tanga dhidi ya Songwe, Mara dhidi ya Geita na Dar es salaam dhidi ya Kigoma.

Fainali za UMITASHUMTA mwaka huu zitahitimishwa tarehe 18 juni 2021 ambapo michezo mbalimbali itakamilika siku hiyo kwa washindi wa jumla kukabidhiwa vikombe na medali za dhahabu, fedha na shaba.