Friday, January 10

“Wanaokataa kutoa ushahidi mahakamani kwa kesi za udhalilishaji dawa yao ipo kikaangoni”.RC Salama

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Salama Mbarouk Khatib amewaonya wazazi wanaokataa kutoa ushahidi mahakamani kwa kesi za udhalilishaji na kusema kwamba dawa yao ipo kikaangoni.

Amesema kuwa, Serikali ya Mkoa huo sasa haitokuwa tayari kuona wazazi wanakataa kutoa ushahidi, kutokana na kuwa wanasababisha kuendelea kudhalilishwa watoto, kwani bila ya ushahidi hakuna hatia kwa watendaji wa makosa hayo.
Akizungumza katika maadhisho ya siku ya mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete mkuu huyo alisema, Serikali ya Mkoa huo haitofumbia macho wazazi wanaokataa kutoa ushahidi wakati mtoto anapodhalilishwa na atashukuliwa hatua za kisheria, ili kuhakikisha vitendo hivyo  wanavidhibiti.
“Hatuwezi kuyafumbia macho matendo ya udhalilishaji kwa sababu yanawaathiri sana watoto wetu, kwa hiyo kama mzazi ana tabia ya kukwepa kutoa ushahidi, ahakikishe yupo kikaangoni kwani hatutomuacha”, alisema Mkuu huyo.
Alieleza kuwa, pia kuna baadhi ya wazazi huwabagua watoto wao, kutowapeleka skuli na kuwaoza waume, jambo ambalo sio sahihi kwani wanawakosesha haki yao ya elimu na kuwadumaza kiali.
“Kwa umoja wetu tuna wajibu wa kuyasimamia haya, ili kuona watoto wote wanapata haki zao za msingi na hawafanyiwi udhalilishaji wa aina yoyote, hii itasaidia kupata taifa bora na lenye wasomi”, alisema RC huyo.
Alifahamisha kuwa, ili kupata maendeleo endelevu ni kuhakikisha kuwa hakuna mtoto atakae achwa nyuma katika upatikanaji wa haki zao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Wete Mgeni Khatib Yahya aliitaka jamii kushirikiana pamoja kuwalea watoto, ili wasikumbwe na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, kwani ndio nguvu kazi ya Taifa.
“Bila ya mashirikiano hatuwezi kumaliza udhalilishaji, kila mmoja kwa nafasi yake apambane vikali kuhakikisha tunaondoa janga hili hatari la maisha ya watoto wetu”, alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Pemba Yakoub Mohamed Shoka alisema, ili kuwalinda na kuwatunza watoto, jamii ihakikishe inamlinda tangu akiwa tumboni kwa kumtunza mama mjamzito.
“Hii ni siku adhimu na muhimu kwetu ambayo inatukumbusha kuwalinda watoto na kuwapatia haki zao za msingi, ikiwemo malezi bora na elimu ambayo ndio ufunguo wa maisha”, alifahamisha Mdhamini huyo.
Mratibu wa shirika la  SOS Pemba Gharib Abdalla Hamad alisema, katika kuwajali na kuwalinda watoto, wamekuwa wakiwapa malezi bora watoto ambao walipoteza malezi bora ya familia au waliopo katika mazingira magumu, kwa kuwasaidia kupata haki zao za msingi kwa mujibu wa Sheria.
Akielezea miongoni mwa majukumu wanayoyafanya ni pamoja na kuimarisha familia, ili watoto waweze kulelewa na kukua ndani ya familia zao, kusaidia kuimairisha mfumo wa ulinzi na hifadhi ya mtoto katika jamii, ili kuwawekea mazingira salama na kuwalinda dhidi ya udhalilishaji.
“Pia tunawasaidia watoto na vijana kuweza kufikia malengo yao, kuwajengea uwezo, ushirikishwaji, kuwaendeleza pamoja na kuongeza ushirikiano kwa wadau mbali mbali wa Serikali na binafsi katika kutoa huduma kwa watoto”, alifafanua Mratibu huyo.
Alisema kuwa, ili kuimarisha ustawi wa watoto ipo haja ya kuzijengea uwezo kamati za shehia zinazoshughulika na kudhibiti udhalilishaji, kuharakishwa kwa upelelezi, kuwapatia msaada wa kisaikolojia wahanga ili waweze kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza, sambamba na kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kupambana na vitendo hivyo.
Alieleza kuwa, asasi za kiraia zinatoa shukrani kwa dk Hussein Mwinyi kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuwalinda watoto, ikiwemo kuruhusu marekebisho ya Sheria ili kuwabana wahalifu wa matendo hayo pamoja na kuanzisha mahakama maalumu.
Katibu Mkuu kutoka Taasisi ya Maafisa Ustawi Zanzibar Saleh Juma Mbarouk aliiomba jamii kutoa ushirikiano mkubwa ili ifikapo mwaka 2030 iwe wamefanikiwa kuondosha kabisa vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto.
Mapema akisoma risala katika mkutano huo, Afisa Wanawake na Watoto Wilaya ya Micheweni Bizume Haji Zume alisema, Idara ya Jinsia na Watoto wana majukumu ya kupokea na kufuatilia malalamiko, kuwasaidia waathirika wa matendo ya udhalilishaji, kuunganisha watoto kwenye mabaraza ya watoto ili wawe na sauti moja na kuwasimamia waratibu wa shehia waweze kuibua kesi za udhalilishaji.
“Tuna uhaba wa vitendea kazi katika kufuatilia malalamiko mbali mbali ya wateja ikiwemo usafiri, pamoja na ufinyu wa bajeti ambayo inawarudisha nyuma katika mapambano haya”, alisema.
Maadhisho hayo ya siku ya mtoto wa Afrika yaliandaliwa na Shirika la SOS, Actionaid, na ZASWA kwa kushirikiana na Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.