Tuesday, November 26

Lengo la mradi wa viungo Zanzibar ni kuongeza ubora na wingi wa bidhaa zinazotokana na matunda, mboga na viungo.

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

 

MRADI wa viungo Zanzibar umedhamiria kufungua fursa zaidi kwa wakulima wa kilimo cha viungo, mboga na matunda visiwani humo.

 

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa biashara na Masoko kutoka Misitu asili (CFP) Pemba Omar Mtarika Msellem katika mkutano wa wadau wa biashara na kilimo uliofanyika katika Chama cha Waandishi wa habari wanawake Tanzania (TAMWA) Pemba.

 

Alisema, lengo kuu la mradi huo ni kuongeza ubora na wingi wa bidhaa zinazotokana na matunda, mboga na viungo, ili kuwaimarisha wakulima wa bidhaa hizo visiwani Zanzibar.

 

‘’Lengo kubwa la mradi huu ni kufungua fursa kwa wakulima ambao wanajishughulisha na na kilimo cha matunda, mboga pamoja na viungo na nikisema kufungua fursa maana yake ni kuwajenga kiuwezo, taaluma na namna ya kuwasaidia pembejeo na mambo mengine ambayo yanaweza kuwasaidia wao kuzalisha na lengo la kufanya hivyo nikuongeza wingi na ubora wa bidhaa zinazokwenda sokoni’’, alisema.

 

Mtarika alieleza,  miongoni mwa matatizo yanayowakabili wazanzibar ni ukosefu wa upatikanani wa vyakula bora, hivyo basi aliahidi kuwa kupitia mradi huo wa viungo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa vyakula bora visivyo na kemikali.

 

“Wazanzibar tunashida ya lishe na upatikanaji wa chakula kwamba tunalima lakini hatuli chakula ambacho kinalinda miili yetu na kuna utafiti ulifanywa na US AIDS wanasema kwamba asilimia 58 ya wanawake wazanzibar wana tatizo la lishe na hiyo ina matokeo ya takriban asilimia 48 ya watoto wa Zanzibar wana tatizo la udumavu’’ alisema.

 

Nao baadhi ya  wakulima na wafanya biashara  walioshiriki katika mkutano huo walisema, wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo wingi wa Kodi na tozo pindi wanapohitaji kusafirisha bidhaa zao, ukosefu wa maeneo toshelezi ya kufanyia shughuli za kilimo, ukosefu wa maji, kukosa elimu ya kilimo, ukosefu wa nishati ya umeme, kukosa mikopo pamoja na uchache wa mabwana shamba.

 

‘’Nimeshawahi kufanya biashara ya ndizi katika kutafuta maisha unaanzia kwa sheha unaambiwa bidhaa hii unatakiwa ulipie shilingi elfu mbili njiani nako traffic ambaye yeye anajukumu la kuangalia usalama wa abiria na mali zao nae anataka chochote unafika bandarini kuna risiti zaidi ya tano unapewa lakini hujui zinachapwa wapi hizo risiti”, alisema Ali Hamad Ali mkaazi wa shengejuu Wilaya ya Wete.

 

Akitoa ufafanuzi juu ya changamoto hizo za masoko Mtarika, aliwataka wakulima kukifanya kilimo kuwa sehemu ya biashara kwa kujitolea kwa hali na mali katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo kutumia fedha kwa ajili kuwalipa mabwana shamba pamoja na kununua dawa na pembejeo, ili kuboresha kilimo.

 

“Tahadhari ambayo nataka niiseme hapa kwa ujumla wake imesemwa hapa kuna tatizo la mbegu, mabwanashamba ukosefu wa mbegu, hivyo changamoto hizi ziwe fursa ya kusonga mbele”, alisema.

 

Mradi huo wa miaka minne wenye lengo la kuboresha maisha ya wakulima wa mboga, matunda na viungo visiwani Zanzibar unaotekelezwa na  PDF, CFP pamoja na TAMWA unaosimamiwa na Serikali chini ya ufadhili wa Umoja wa Ulaya.